December 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Ugawaji maeneo ya biashara soko la kariakoo kuwa la uwazi

Na Mwandishi wetu, timesmajira

MWENYEKITI wa Bodi ya Wakurugenzi ya Shirika la Masoko ya Kariakoo Hawa Ghasia amesema bodi hiyo imejipanga kuhakikisha mradi wa ukarabati na ujenzi wa soko la Kariakoo utakamilika ndani ya muda wa mkataba na kwa ubora ambapo ugawaji wa maeneo ya biashara utakuwa wa uwazi.

Akiwa kwenye eneo la mradi huo leo Aprili 12,2023 jijini Dar es Salaam,Ghasia ameelezea kuridhishwa kwake na kazi inayoendelea kufanya na mkandarasi kampuni ya ESTIM ambapo serikali ya awamu ya sita imetoa shilingi Bilioni 28.03 .

Akizungumzia kuhusu mchakato wa ufanyaji biashara mara baada ya mradi kukamilika, Ghasia amesema ugawaji wa maeneo ya kufanyia biashara ikiwemo maduka na vizimba kuwa utakuwa wa wazi .

“Mchakato wa ugawaji maduka ,vizimba na meneo mengine ya biashara utafanyika kwa uwazi ili kila mwananchi mwenye sifa apate” amesema Ghasia.

Serikali ilianza kutekeleza mradi huo wa ukarabati na ujenzi wa soko la Karikaoo Januari 2022 na utakamilika Oktoba 2023 ambapo Shirika la Nyumba la Taifa ( NHC) ni Mshauri Elekezi na ujenzi ukifanywa na kampuni ya ESTIM Contraction Company Ltd.