December 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Ufaransa yaridhishwa na mazingira ya Biashara, Uwekezaji nchini

Na Mwandishi wetu, Dar

Ufaransa imeonesha kuridhishwa na hatua zilizochukuliwa na zinazochukuliwa na Serikali ya Awamu ya Sita katika kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji nchini Tanzania.

Kauli hiyo imetolewa na Seneta wa Ufaransa anayeshughulikia masuala ya Wafaransa waishio Nje ya Ufaransa, Mhe. Olivier Cadic wakati alipokutana kwa mazungumzo na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula (Mb) katika Ofisi ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam.

Seneta, Cadic amesema kuwa kwa sasa mazingira ya kufanya biashara na uwekezaji nchini Tanzania yameboreshwa sana na yanashawishi wafanyabiashara wengi kuja kufanya biashara nchini.

“Tumepata wasaa mzuri wa kujadili fursa za biashara na uwekezaji ambazo zinapatikana nchini Tanzania ambapo wafanyabiashara na wawekezaji kutoka Ufaransa wanaweza kuja kuwekeza……kwangu mimi imekuwa fursa ya kuona mazingira haya ya uwekezaji ambayo yanapatikana hapa Tanzania,”

“Serikali ya Tanzania imejiwekea mazingira rafiki ya biashara na uwekezaji kwa sasa, haya ni mabadiliko makubwa ambayo yataendeleza urafiki wa Tanzania na mataifa mbalimbali ikiwemo Ufaransa. Kwangu mimi imekuwa fursa kubwa ya kujionea mazingira haya mazuri ya biashara na nitawaelezea wafanyabioashara na wawekezaji kutoka Ufaransa kuja kuwekeza hapa,” amesema Seneta Cadic

Kwa Upande wake Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula amesema kuwa ziara ya Seneta Olivier Cadic hapa nchini ni matunda ya ziara ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan aliyoifanya nchini Ufaransa hivyo Seneta Olivier amekuja nchini kuangalia maeneo ambayo wanaweza kuhamasisha wafanyabiashara na wawekezaji kutoka Ufaransa kuja kuwekeza Tanzania katika sekta za Uchukuzi, Nishati, Utalii, Elimu na Kilimo.

“Seneta amefurahishwa na juhudi zinazofanywa na Serikali ya Awamu ya Sita katika kuboresha zaidi na kuendeleza mazingira bora ya biashara nchini,” amesema Balozi Mulamula

Balozi Mulamula pamoja na mambo mengine, amemhakikishia Seneta Cadic kuwa Serikali bado inaendelea kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji ikiwa ni pamoja na kuondoa vikwazo vilivyokuwa vinahatarisha ukuaji wa biashara kati ya Tanzania na mataifa mengine.