January 10, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Ufadhili wa NMB wafikia Sh. trilioni 1.56 sekta ya kilimo

Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online

Serikali imezichangisha benki nchini kwa lengo la kuongeza wigo kwa wakulima, wafugaji na wavuvi kukopa ili kuongeza uwekezaji kwenye sekta ya kilimo ili waweze kuchangia zaidi juhudi za ujenzi wa Taifa.

Akizungumza kwenye ufunguzi rasmi wa maonyesho ya Nanenane 2022 yanayofanyika Kitaifa mkoani Mbeya, Makamu wa Rais,Dk. Philip Mpango, alizitaka taasisi za fedha kuchangia zaidi shughuli za kilimo cha mazao,ufugaji na uvuvi.

Kwa mujibu wa Dk. Mpango, wakulima, wafugaji na wavuvi wanahitaji mikopo zaidi ili kuongeza uwekezaji na uzalishaji kwa ajili ya kupunguza changamoto ya ajira nchini.

Aliendelea kueleza kuwa maendeleo ya kilimo yanahitaji ufadhili mkubwa kitu ambacho Benki ya NMB imesema imekuwa ikifanya kwa muda mrefu na kuwekeza zaidi ya Shilingi trilioni 1.56 katika miaka mitano iliyopita.

Akizungumzia mikopo hiyo, Meneja wa NMB Nyanda za Juu,Straton Chilongola, alisema ukopeshaji unaofanywa na benki hiyo umekuwa na tija kubwa katika mnyororo wa thamani wa kilimo nchini.

“Mikopo ya NMB imewawezesha wakulima, wavuvi na wafugaji kuchangia ukuaji wa pato la taifa na maendeleo ya nchi kwa ujumla.” alisema Chilongola

Akielezea ufadhili wa NMB kwenye sekta hiyo, alisema mikopo ambayo imetolewa na benki hiyo ni pamoja na zaidi ya Shilingi bilioni 300 mwaka huu kwa ajili ya kilimo cha kahawa, tumbaku, parachichi, mpunga, ufuta, soya na mahindi na Shilingi bilioni 20 kwa ajili ya ujenzi wa maghala.

Pia, kupitia NMB Foundation, benki hiyo imetoa elimu ya fedha na mafunzo ya biashara kwa vyama vya ushirika wa wakulima (AMCOS) 1,550 nchi nzima, ili kuwajengea uwezo wa namna bora ya kusimamia mapato yao. 

Kubwa zaidi, Benki ya NMB imekuja na Suluhisho kwenye masuala ya utatuzi wa kifedha kwa kuja na NMB Mshiko Fasta ambapo mkulima kupitia simu yake ya mkononi, anaweza kupata mkopo wa hadi 500,000 papo hapo bila dhamana akiwa na NMB Mkononi.

Meneja wa NMB Nyanda ya Juu, Straton Chilongola akimkabidhi risala kuhusu utendaji wa NMB kwenye Sekta ya Kilimo, Ufugaji na Uvuvi Makamu wa Rais, Mhe. Dkt. Philip Mpango katika ufunguzi rasmi wa maonesho ya NaneNane mjini Mbeya.