March 7, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

UDSM waibuka na ubunifu wa teknolojia maonesho ya sabasaba

Na Agnes Alcardo, Timesmajira Online.

MKUU wa Kitengo cha Mawasiliano na Masoko wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) Dkt. Dotto Kuhenga, amewaomba wananchi kutembelea banda la chuo hicho, katika maonesho ya Sabasaba, ili kujifunza na kujionea ubunifu unaofanywa katika chuo hicho.

Akiongea na mwandishi wa gazeti hili katika maonesho ya Saba Saba yanayofanyika jijini Dar-es-Salaam, katika banda hilo, Dkt. Kuhenga amesema hadi sasa muitiko wa watu ni mkubwa, ambao wameendelea kufika katika banda la chuo hicho kuona na kupata elimu juu ya masuala mbalimbali hususani ya kitaaluma.

Amesema, UDSM wamejipanga vyema kupokea na kutoa elimu kwa watu mbalimbali wanaofika katika banda hilo, huku akisisitiza juu ya kujionea ubunifu unaofanywa na watendaji na wanafunzi kutoka chuo hicho, ikiwa pamoja na kuwepo kwa mradi wa teknolojia mpya ya uchenjuaji wa madini (Hybrid Vat Teaching Technology).

Mradi wa uzalishaji pombe aina ya wine iliyotengenezwa na mnazi pamoja na utoaji wa elimu ya adhabu gandamizi kwa watoto na mambo mengine.

Aidha ameelezea ufanyaji kazi wa mradi huo mpya uliofanywa na shule kuu ya Madini (SOMG) kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Joseph Malemi ambaye ni mwanafunzi,amesema, teknolojia hiyo mpya ya uchenjuaji wa dhahabu inaenda kutatua changamoto za wachimbaji wadogo wa dhahabu, ikiwa pamoja na kwenda kuongeza kiwango cha uvunaji kutoka asilimia 50 hadi 70 mpaka asilimia 90.

Matumizi ya muda mchache katika uvunaji kutoka siku saba mpaka 14, ambapo kwa kutumia teknolojia hiyo muda wa uvunaji utakuwa wa masaa 12 hadi 24, pia kupunguza kiwango cha kemikali, ambapo hivi sasa wachimbaji hao wamekuwa wakitumia kemikali nyingi.

“Teknolojia hii ni nzuri sana na inaenda kutatua changamoto za wachimbaji wadogo wa dhahabu, hivi sasa mradi huu upo katika hatua nzuri na tunashukuru mapokeo ya watu hususani wachimba madini wenyewe wameupokea vizuri mradi huu na kuona kuwa unaenda kuwa mkombozi wao”, amesema Malemi.