November 25, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

UDOM kutengeneza vyakula lishe dhidi ya magonjwa yasiyoambukiza

Na Joyce Kasiki,Timesmajira online

MAKAMU Mkuu wa Chuo cha Dodoma (UDOM) Profesa Lugano Kusiluka amesema Chuo hicho kina   mpango wa kutafuta wadau na wabia ili kianze kutengeneza vyakula lishe ambayo ni Tiba dhidi ya magonjwa yasiyoambukiza  ili vipatikane kirahisi sokoni. 

Profesa  Kusiluka,ameyasema hayo kwenye maonesho ya 48 ya Kikataifa ya Biashara (Sabasaba) jijini Dar Es Salaam alipotembelea banda la UDOM.

Amesema chuo hicho kina wataalam ambao hutumika kanuni katika utengenezaji wa tibalishe za kukabiliana na magonjwa yasiyoambukiza.

Amesema chuo hicho ndio kilikuwa cha kwanza kutoa shahada katika lishe tiba na chakula hivyo uzoefu huo umesaidia wataalam kutengeneza vyakula mbalimbali dhidi ya magonjwa hayo.

“Watu waje tushirikiane tutengeneze tiba lishe, Tanzania yenye afya ndiyo itakayotupeleka kwenye dira ya maendeleo ya mwaka 2050, tunataka watu wavipate kutoka sehemu mbalimbali,” amesema Profesa Kusiluka.

Profesa Kusiluka ametaja mafunzo mengine yanayotolewa chuoni hapo ni katika fani za udaktari, wauguzi, wataalam wa lishe tiba, afya ya jamii .

” Tanzania imejitangaza vizuri na ni nchi inayovutia kwa wawekezaji kutokana na juhudi zilizofanywa na Rais Samia Suluhu Hassan na kwamba wanaunga mkono juhudi hizo za Serikali kwa kuandaa wataalam katika sekta mbalimbali,

“Tunafundisha wataalam katika maeneo mbalimbali kama vile biashara, uchumi, ujasiriamali, masoko na mambo yote yanayohusiana na biashara, lakini biashara katika miaka ya siku hizi ni lazima uwe unajua kuifanya kisomi,” amesema.

Aidha ametumia nafasi hiyo kuwakaribisha Watanzania kwenda kusoma katika chuo hicho kwa sababu programu zote zinazofundishwa vyuo vingine wanazo.