Na Mwandishi Wetu, TimesMajira Online
LEO Tanzania imeshirikiana na mataifa mengine duniani kuadhimisho ya Siku ya Chakula Salama Duniani (World Food Safety Day).
Maadhimisho hayo yaliridhiwa na Mkutano Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN) uliofanyika Desemba 20, 2018.
Mkutano huo ulipitisha Azimio Namba 73/250 lililotangaza Siku ya Chakula Salama Duniani kuadhimishwa kila kila mwaka Juni 7 na hivyo maadhimisho haya yamefanyika duniani kote kwa mara ya kwanza mwaka huu jana (2019) yakiwa na kauli mbiu isemayo; “Chakula salama, jukumu la kila mmoja wetu”. Kwa mwaka huu maadhimisho hayo yameendelea kauli mbiu hiyo.
Pamoja na mambo mengine maadhimisho haya yanalenga kukumbusha, kuelimisha na kuongeza uelewa wa jamii katika masuala ya chakula salama (kutoka shambani/majini hadi kwa mlaji).
Vilevile, maadhimisho haya yanatoa fursa ya kuhamasisha wadau wote wa chakula kujitathmini juu ya wajibu wa kila mmoja katika kuhakikisha chakula salama.
Akizungumzia maadhimisho hayo Ofisa Usalama wa Chakula wa Shirika la Viwango Tanzania (TBS) Dkt. Analice Kamala, anasema maadhimisho hayo yana umuhimu mkubwa kitaifa na kimataifa, kwani usalama wa chakula ni kitu kisichoepukika.
Maana ya Chakula na chakula salama, vihatarishi vya chakula salama na vyanzo vyake
Dkt. Kamala anasema chakula ni kitu chochote, kilichosindikwa au kisichosindikwa, ambacho kimekusudiwa kuliwa na binadamu ikiwa ni pamoja na vinywaji, pipi na kitu chochote kinachotumika katika usindikaji au utayarishaji wa “chakula” na ambacho siyo kipodozi, tumbaku au dawa.
Kwa upande mwingine, anasema chakula salama ni uhakika kuwa chakula kikitayarishwa na kuliwa kama kilivyokusudiwa hakitaleta madhara kwa mlaji.
Viahatarishi na vyanzo vyake
Kwa mujibu wa Dkt. Kamala vihatarishi vya usalama wa chakula ni vile ambavyo kwa njia moja au nyingine vinaweza kufanya chakula kisiwe salama kwa matumizi ya binadamu. Vihatarishi hivyo vimegawanyika katika makundi matatu.
Dkt. Kamala anataja kundi la kwanza kuwa ni vihatarishi vya Kibailojia (biological hazards)
Anasema viahatarishi hivi vinajumuisha vimelea vya magonjwa kama bakteria, virusi, minyoo (parasites) na prion (a type of protein that can trigger normal proteins in the brain to fold abnormally ).
Anasema mara nyingi vinaingia katika chakula kupitia malighafi zinazotumika viwandani, mazingira ambayo chakula uandaliwa, binadamu au wanyama.
“Hupatikana katika mazingira ambayo vyakula hivi hulimwa, kuvunwa, kuhifadhi na wakati wa usindikaji na maandalizi wakati wa kula,”anasema Dkt. Kamala na kuongeza;
“Wingi wa vimelea hivi hupunguzwa au kuondolewa kabisa wakati wa kupika au kusindika na pia kwa kudhibiti mfumo mzima wa uzalishaji, usindikaji na uhifadhi wa chakula (Usafi, joto na muda).”
Kundi la pili kwa mujibu wa Dkt. Kamala ni vihatarishi vya Kikemikali (chemical hazards). Anasema vihatarishi vya kikemikali vinaweza kupatikana ndani ya chakula chenyewe au kuingia wakati wa uhifadhi au usindikaji.
Anasema kemikali zimegawanyika katika makundi yafuatayo tofauti. Anataja makundi hiyo kuwa ni kemikali za sumu zinazopatikana ndani ya chakula husika.
“Sumu hizi zinakuwepo kwa sababu mbalimbali ikiwa ni pamoja na kutoa kinga dhidi ya uharibifu. Sumu zinazotumika kama kinga ni kama vile cyanide katika muhogo, sumu kwenye samaki aina ya bunju,”anasema.
Nyingine anasema ni uchafuzi wa kemikali za sumu katika mazao ya chakula mfano sumukuvu na madini tembo.
Eneo jingine la vikolezo katika chakula ambavyo husaidia katika usindikaji ikiwa vitaongezwa katika kiwango kisichokubalika na mabaki ya kemikali ambayo hutokana na kemikali zilizotumika kwenye kilimo, mifugo, au usafi wa sehemu za uzalishaji.
Anataja eneo lingine kuwa ni uchafuzi wa kemikali zilizopo kwenye kitu chochote kinachogusana na chakula (food contact materials), mfano vifungashio, vifaa vya majumbani vinavyotumika kuandaa chakula (sufuria, sahani, n.k).
Dkt. Kamala anataja kundi lingi lingine kuwa ni vihatarishi vya kimaumbo (phyisical hazards).
Anasema vihatarishi hivi vimegawanyika katika makundi yafuatayo mbalimbali.
Makundi hayo ni ya vitu vigumu vinavyoweza kusababisha majeraha ambavyo hupatikana ndani ya chakula chenyewe, mfano vipande vya mifupa ya nyama au samaki.
Anasema uchafuzi huu utokea wakati wa usindikaji, mfano vipande vya chuma, glasi ambapo mionzi inayotumika katika kuhifadhi chakula inapoingia kwenye chakula kwa bahati mbaya.
Athari zitoakazo na chakula kisichokuwa salama
Kwa mujibu wa Dkt. Kamala kuna athari mbalimbali zitokanazo na chakula kisichokuwa salama.
Athari hizo ni pamoja na za kiafya. Dkt. Kamala anasema athari hizo huweza kujitokeza ndani ya muda mfupi (food poisoning) mfano; kuumwa tumbo, kutapika, kuhara na kuhara damu au baada ya muda mrefu mfano; kansa, upungufu wa kingamwili na udumavu kwa watoto chini ya umri wa miaka mitano (5).
Mtaalam huyo anasema kila mtu yuko kwenye hatari ya kupata madhara ya kiafya. Hata hivyo hivyo Dkt, Kamala anataja makundi maalum ya wagonjwa, wajawazito, watoto na wazee kwamba yapo katika hatari zaidi ya kuathirika na chakula kisicho salama.
Kwa upande wa kiuchumi, Dkt. Kamala anasema katika biashara za ndani, za kikanda na za kimataifa, chakula kisichokuwa salama husababisha athari mbalimbali.
Anataja athari hizo kuwa ni pamoja na kukataliwa kwa bidhaa za chakula zilizozidi viwango vinavyokubalika katika soko na hivyo kukosa mapato.
Eneo lingine ni kupungua kwa akiba ya chakula, (chakula kilichochafuliwa zaidi ya kiwango kinachoruhusiwa hakifai kwa matumizi ya binadamu hivyo hutakiwa kuharibiwa).
Pia anataja athari nyingine kuwa ni kuongezeka kwa gharama za matibabu na kupungua kwa nguvu kazi na uzalishaji mali kutokana na wato wengi kuwa wanaumwa na ndugu wa karibu kutumia muda mwingi kuwahudumia.
Nini kifanyike ili chakula kiwe salama
Ili kuwa na chakula salama, Dkt. Kamala anasema unatakiwa mfumo thabiti wa usimamizi na udhibiti wa uzalishaji, usindikaji, usambazaji na uhifadhi wa chakula unahitajika.
Anasema lengo kuu la kuwa na mfumo imara wa chakula salama ni kujenga mazingira ambayo yatatoa uhakika wa uzalishaji chakula ambacho ni salama ili kulinda afya ya mlaji na kukuza biashara.
Anasema misingi imara ya usimamizi wa usalama inahusisha mambo yafuatayo; uwepo wa sheria, muundo wa kitaasisi (usimamizi), mfumo wa ukaguzi na ufuatiliaji, huduma za maabara na elimu kwa umma.
More Stories
Boost ilivyoboresha miundombinu ya elimu Ilemela
Samia apongeza walimu 5,000 kupatiwa mitungi ya gesi, majiko kutoka Oryx
Uwekezaji kwenye kilimo utatimiza ndoto ya Samia ya nchi kuwa ghala la chakula Afrika