May 3, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Zao lililshmbuliwa na sumukuvu

Fahamu Sumukuvu na madhara yake na jinsi ya kudhibiti

Na Dkt. Analice Kamala

SHIRIKA la Viwango Tanzania kama Taasisi yeney dhamana ya kusimamia na kudhibiti usalama wa chakula nchini, limejumuika na mataifa katika kuadhimisha Siku ya Chakula Salama Duniani, ambayo hufanyika tarehe 7 Juni  ya kila mwaka. Makala hii imejikita katika kutoa elimu juu ya sumukuvu kwani sumu hiyo uhathiri sana vyakula aina ya nafaka na mbegu za mafuta hasa mahindi na karanga ambavyo huliwa sana katika jamii ya Kitanzania na ambayo hutumika kama mazao ya biashara na hivyo kuweza kuleta madhara ya kiafya na kuhathiri biashara ya mazao hayo

Sumukuvu ni nini?

Sumukuvu (mycotoxins) ni sumu zinazozalishwa na kuvu/fangasi (fungus) wa makundi mbalimbali) wanaoota zaidi kwenye mazao ya chakula kama vile mahindi na karanga. Sumukuvu huweza kuzalishwa kwenye mazao yakiwa katika hatua mbalimbali kama vile:

  • shambani,
  • baada ya kuvunwa
  • wakati wa kusafirisha au
  •  kuhifadhi

Kumbuka: Sumukuvu zinapokuwepo kwenye mazao au bidhaa huendelea kubaki hata baada ya chakula kupikwa au kusindikwa.

Aina ya kuvu wanaosababisa sumukuvu

Kuna aina nyingi za kuvu wanaoweza kushambulia mazao. Aidha kuvu wa makundi matatu yaani Aspergillus, Penicillium na Fusarium ndio hasa wanahusika na kuzalisha sumukuvu kwenye mazao ya nafaka na mbegu za mafuta.

Aina za sumukuvu

Zipo aina nyingi za sumukuvu ambazo huzalishwa na kuvu tofauti.  Kwa kulinganisha kiwango cha uchafuzi wa sumukuvu katika mazao ya chakula pamoja na kiwango cha madhara ya kiafya kwa binadamu yatokanayo na sumukuvu, kwa hapa Tanzania sumukuvu aina ya aflatoxins na fumonisins ndiyo tatizo zaidi.

Kumbuka: Uwepo wa kuvu na kuzalisha sumukuvu unategemea na hali ya hewa ya mahali husika, hivyo maeneo tufauti huweza kuwa na kiwango na aina tofauti za kuvu.

Dalili za uchafuzi wa sumukuvu kwenye mazao ya chakula

Sumukuvu zinapokuwepo kwenye mazao au bidhaa, hazionekani kwa macho. Pia huendelea kubaki hata baada ya chakula kupikwa au kusindikwa. Dalili ya mazao yaliyochafuliwa na sumukuvu ni pamoja na:

  • Ukungu/kuvu
  • Harufu ya uvundo
  • Nafaka kutengeneza vumbi
  •  Nafaka kugandamana
  •  Nafaka kubadilika rangi, kuwa na weusi

Mahindi na karanga ni mojawapo ya mazao muhimu ya chakula ambayo hushambuliwa na fangasi wanaozalisha sumukuvu kwa wingi

Sumukuvu inavyoweza kumfikia mlaji

Mlaji huweza kupata sumukuvu endapo:

  • Atakula chakula kilichochafuliwa na sumu hiyo.
  • Atakula mazao yanayotokana na mifugo kama vile maziwa endapo mifugo italishwa chakula kilichochafuliwa na sumukuvu. (Mfano mashudu ama nafaka mbovu).
  • Mtoto atanyonya maziwa ya mama aliyekula chakula kilichochafuliwa na sumukuvu.

Madhara yatokanayo na sumukuvu

Madhara ya kiafya

Ulaji wa vyakula vilivyochafuliwa na sumukuvu huweza kusababisha madhara mbalimbali ya kiafya. Madhara hayo huweza kujitokeza ndani ya muda mfupi au baada ya muda mrefu kutegemeana na; kiasi cha sumukuvu kilichopo kwenye chakula kilicholiwa, kiasi cha chakula na idadi ya milo ya chakula kilichochafuliwa, pamoja na umri na hali ya afya ya mlaji.

Madhara yanayotokea ndani ya muda mfupi

Madhara ya sumukuvu kiafya ambayo huweza kutokea ndani ya muda mfupi husababishwa na ulaji wa kiasi kikubwa cha sumukuvu. Madhara hayo ni pamoja na kuathirika kwa ini, figo, mfumo wa fahamu pamoja na kupunguza uwezo wa damu kuganda na hata kifo. Dalili zake ni pamoja na:

  • Maumivu ya tumbo
  • Kutapika
  • Kuvimba tumbo, miguu na viganja
  • Kuharisha
  • Kuwa manjano sehemu mbalimbali za mwili (mfano viganja, nyayo, macho)
  • Degedege
  • Kupungua kwa wingi wa damu

Madhara yanayotokea baada ya muda mrefu

Madhara ya sumukuvu kiafya ambayo huweza kutokea baada ya muda mrefu husababishwa na ulaji wa sumukuvu kwa kiasi kidogo kwa muda mrefu (chronic exposure). Madhara hayo ni pamoja na:

  • Saratani ya ini, figo na koo
  • Kupungua kingamwili
  • Udumavu kwa watoto chini ya miaka mitano
  • Watoto kuzaliwa mgongo wazi
  • Kuathirika kwa mfumo wa uzazi

Athari za sumukuvu kiuchumi

Katika biashara za ndani, kikanda na kimataifa, uchafuzi wa sumukuvu husababisha athari zifuatazo;

  1. Kukataliwa kwa bidhaa za chakula zilizozidi viwango vya sumukuvu vinavyokubalika katika soko na hivyo kukosa mapato.
  2. Kupungua kwa akiba ya chakula, (chakula kilichochafuliwa zaidi ya kiwango kinachoruhusiwa, hakifai kwa matumizi ya binadamu na mifugo hivyo hutakiwa kuharibiwa).
  3. Kuongezeka kwa gharama za matibabu
  4. Kupungua kwa nguvu kazi na uzalishaji mali.

Jinsi ya kudhibiti sumukuvu

Udhibiti wa sumukuvu kwenye mazao Kabla na wakati wa kuvuna

Kanuni bora za kilimo ni mbinu za msingi katika kudhibiti mashambulizi ya kuvu na uchafuzi wa sumukuvu ili kupata mazao bora na salama kwa mlaji. Kanuni hizi ni pamoja na,

  • Panda kwa wakati mbegu zilizothibitishwa na taasisi za udhibiti wa viwango wa ubora wa mbegu
  • Hakikisha shamba lako ni safi wakati wote
  • Tumia viuatilifu mara uonapo dalili za visumbufu (wadudu, magonjwa) kwenye mazao
  • Vuna kwa wakati
  • Ondoa mazao shambani mara baada ya kuvuna

Kumbuka: Kuchelewa kuvuna au kulundika mazao muda mrefu shambani huchochea uzalishaji wa sumukuvu.

Udhibiti wa sumukuvu kwenye mazao baada ya kuvuna

Baada ya kutoa mazao shambani, taratibu nyingine zote zinazofuata zifanywe kwa umakini ili kuzuia mazao kupata mashambulizi ya kuvu na kuchafuliwa na sumukuvu. Jinsi ya kudhibiti uchafuzi wa sumukuvu baada ya mazao kutoka shambani ni kama ilivyoainishwa katika hatua zifuatazo,

  • Chambua mahindi na karanga kuondoa taka, mbegu hafifu, zilizopasuka, zilizooza, zilizobadilika rangi na zilizoharibiwa na wadudu

Kumbuka: Mazao yaliyoharibika yasitumike kama chakula au/na kutengeneza pombe. Pia yasiuzwe na yasilishwe wanyama.

  • Anika kwenye kichanja au vifaa vingine vya kuanikia mfano mkeka, turubai au jamvi ili kuepuka mazao yasiguse udongo au sakafu.
  • Kausha mahindi na karanga ipasavyo kabla ya kuhifadhi

Kumbuka: Mazao ya mahindi na karanga yasipokaushwa vizuri kabla ya kuhifadhi huchochea uzalishwaji wa sumukuvu

Udhibiti wa sumukuvu kwenye mazao Wakati wa kuhifadhi

  • Hakikisha kuwa ghala au chumba cha kuhifadhi mazao ni safi
  • Hifadhi kwenye ghala au chumba kinachoruhusu mzunguko wa hewa
  • Tumia vifaa vyenye ubora kama vile magunia, mifuko au mapipa kuhifadhia mazao
  • Usichanganye mazao ya zamani na mazao  mapya
  • Weka mazao kwenye sehemu zilizoinuka au juu ya vichanja
  • Hakikisha sehemu ya kuhifadhia haiingii maji au mvua
  • Zuia wadudu waharibifu kwa kuweka viuatilifu vinavyopendekezwa na wataalam na kwa vipimo sahihi
  • Zuia wanyama waharibifu kama vile panya, vicheche, nguchiro

Kumbuka:

  • Wadudu wasipodhibitiwa huongeza unyevu na joto katika ghala ambavyo huchochea kuvu kuzaliana na kuzalisha sumukuvu
  • Viuatilifu visipotumiwa kwa usahihi vinaweza kuathiri afya ya mlaji. Hivyo zingatia matumizi ya viuatilifu kwa kiwango sahihi na muda ambao mazao yaliyowekwa viuatilifu yanahifadhiwa kabla ya kuruhusiwa kwa matumizi.

Udhibiti wa sumukuvu Wakati wa kuandaa mazao kwa ajili ya chakula

  • Peta na chambua kuondoa taka, mbegu hafifu, zilizopasuka, zilizooza, zilizobadilika rangi na zilizoharibiwa na wadudu
  • Osha kundoa vumbi, udongo na  punje dhaifu
  • Koboa mahindi kabla ya kusaga
  • Baada ya kusaga mahindi, hifadhi unga kwenye chombo safi kisichoruhusu unyevu

Kumbukuka: Kupungua kwa sumukuvu kwa njia ya kukoboa hutegemea na kiwango cha punje za mazao zilizoharibika au kuoza.