December 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

UCSAF kujenga Minara ya mawasiliano 1087 kurahisisha matumizi ya mtandao nchini

Na Zena Mohamed,Timesmajiraonline,Dodoma.

MFUKO wa Mawasiliano  kwa wote (UCSAF) umesema Serikali  imetoa ruzuku ya sh.bilioni 199 kwa ajili ya kuwezesha kampuni za mawasiliano  kujenga minara ya mawasiliano 1,087 katika kata 1242 zenye vijiji 3654 vyenye wakazi 15,130,750.

Hayo yameelezwa jijini hapa leo,Februari 13,2023 na Mtendaji Mkuu wa UCSAF, Justina Mashiba wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu utekelezaji wa miradi ya mfuko huo ambapo amesema utaekeleza unaendelea katika Minara 155 yenye vijiji 276 na wakazi 1,809,500 ili kurahisisha matumizi ya mtandao.

Aidha Mashiba ameeleza  kuwa kwa kuhakikisha mfuko huo  unafikisha mawasiliano kwa watanzania waishio vijijini wameona vyema kujenga minara hiyo na ikikamilika watanzania waishio vijijini wapatao zaidi ya milioni 15 wataweza kupata mawasiliano ya intaneti kwa uhakika.

“UCSAF imeingia mikataba kufikisha huduma katika kata 1242 zenye vijiji 3,654,wakazi 15,130,250 minara 1087 yenye vijiji 3378 na wakazi 13320750 utekelezaji unaendelea katika minara 155 yenye jijiji 276 na wakazi 1,809,500 na tayari  Ruzuku iliyotolewa ni sh bilioni 199,

“Pia tayari ruzuku ya sh.bilioni 6.9 imeshatolewa  katika mradi wa kimkakati wa Zanzibari ,ambapo minara 42 katika shehia 38.

Pia amesema  kuwa mfuko huo umetekeleza mradi wa kupeleka vifaa vya tehama katika shule 811 na kwa wastani wa shule upewa kompyuta 5,printa 1 na projekta 1.

Aidha amesema kuwa kwa mwaka wa fedha 2022/2023 shule 150 zitafikishiwa vifaa vya tehama huku bajeti kwa mwaka ikiwa ni sh 1,950,000,000.

Pia amezungumzia utoaji wa elimu kwa walimu juu ya uboreshaji wa matumizi ya TEHAMA ambapo mwaka 2016 mafunzo yalianza ambapo walimu 3,465 wamepatiwa mafunzo na walimu wapatao 3,139 wanatoka Tanzania bara na walimu 326 wanatoka Tanzania Zanzibar.

Hata hivyo UCSAF imeeleza kuwa katika mkakati wa kuhakikisha kila mtanzania anatumia huduma ya tehama wameanzisha mpango wa kufunga mitandao ya WiFi katika sehemu za wazi kama vile vyuo vikuu,mahosipitali pamoja na kwenye masoko ili kila mmtanzania aweze kutumia mtandao nakupata huduma kwa wepesi.