January 23, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Uchaguzi SOREFA bado hakijaeleweka

Na Moses Ng’wat, TimesMajira Online, Songwe

HADI sasa haijafahamika Uchaguzi wa Chama cha Soka Mkoa wa Songwe (SOREFA) utafanyika lini baada ya taarifa za awali kudai kuwa uchaguzi huo umezuiliwa kutokana na wajumbe wa mkutano Mkuu kutokuwa halali kwa kuwa hakuna Wilaya iliyofanya uchaguzi wa kuwapata viongozi ambao ndio wajumbe wa Mkoa.

Jana uchaguzi huo ulizuiliwa na Mamlaka ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Songwe, baada ya kuwashikilia Kaimu Mwenyekiti wa Chama cha Soka Mkoa wa Songwe (SOREFA), George Msyan na Kaimu Katibu wake, Emmanuel Mgala, kwa tuhuma za ubadhirifu wa shilingi 800,000.

Tukio la kukamatwa kwa Viongozi hao lilitokea saa 12:17 mchana wakati viongozi hao wakiwa ndani ya ukumbi wa mkutano wa uchaguzi wa kuwapata viongozi wapya wa chama cha soka Mkoa huo, mbele ya Rais wa Shirikisho la soka nchini (TFF) Wallece Karia aliyekuwa ukumbini hapo ambapo inadaiwa alipita kusalimu wajumbe akitokea Mkoani Rukwa kwa ajili ya mchezo wa fainali wa Kombe la Shirikisho la Azam (Azam Sports Ferderation Cup) na Simba kuibuka mabingwa baada ya kuwafunga Namungo goli 2-1.

Hali hiyo iliibua sintofahamu na kusababisha kusimamishwa kwa uchaguzi
huo, huku vikifanyia vikao kadhaa kati ya TAKUKURU, viongozi wa TFF na ofisi ya Mkuu wa Mkoa kwa ajili ya kunusuru uchaguzi huo huku Mtandao huu ukishuhudia viongozi kadhaa wa kamati ya uchaguzi kutoka TFF wakiwa wameambatana na viongozi wa TAKUKURU wakiingia ofisi za
Mkuu wa mkoa Songwe, Brigedia Jenerali Nikodemas Mwangela.

Akizungumza tukio la kukamatwa kwa viongozi hao wa soka Mkoa wa
Songwe, Kaimu Kamanda wa Takukuru Mkoa wa Songwe, Edings Mwakabonja, amesema fedha hizo zilitolewa na TFF kwa ajili ya kuendesha mashindano ya vijana chini ya miaka 15(U-15).

“Bado tunaendelea kuwashikilia na uchunguzi ukikamilika tutatoa
taarifa zaidi ila kwa sasa tunaendelea na mahojiano na taratibu
nyingine za kisheria zinaendelea na watu watahamishwa kile kinachoendelea,” amekema Kamanda huyo.

Alipoulizwa juu ya taarifa kuwa wao TAKUKURU wamezuia uchaguzi
usifanyike, Mwakabonja alisema suala hilo liko nje ya uwezo wake kwa
kuwa mamlaka yake hayamruhusu kuzungumzia suala hilo.

Hata hivyo, taarifa ambazo hazikiweza kuthibitishwa na mamlaka za soka
kwa ngazi ya TFF zinaeleza kuwa uchaguzi huo umezuiliwa kwa kuwa
wajumbe wa mkutano huo hawakuwa halali kwa kuwa hakuna Wilaya
iliyofanya uchaguzi wa kuwapata viongozi ambao ndio wajumbe wa Mkoa.

Awali mtandao huu ulizungumza na rais Karia ambaye alisema licha ya
changamoto hiyo iliyojitokeza bado uchaguzi ni muhimu hivyo ufanyike na
kuwaasa wana Songwe kuwa wakiendelea kuchagua viongozi wa namna hiyo Songwe haitawezi kukua kimichezo.