January 10, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Uchaguzi NaCoNGO wafanyika ,Lilian Badi anyakua nafasi ya uenyekiti

Na Joyce Kasiki,Timesmajira online,Dodoma

HATIMAYE Baraza la Taifa la Mashirika yasiyokuwa ya Kiserikali (NaCoNGO) limepata viongozi wapya huku Lilian Badi akijinyakulia nafasi ya uenyekiti wa baraza hilo .

Akitangaza matokeo ya uchaguzi hu,Mwenyekiti wa Kamati ya mpito iliyosimamia uchaguzi huo,Flaviana Charles amesema Badi ameibuka na ushindi huo baada ya kupata kura 21 dhidi ya mpinzani wake Jane Magigita aliyeambulia kura nane.

Nafasi ya Katibu Mkuu,imechukuliwa na Revocatus Sono aliyepata kura 22 huku Gift Kilasi akiambulia kura saba ,aliyeshinda nafasi ya Mweka hazina ni John Kiteve kwa kura 15 huku Miraji Malinda akipata kura 13 na nafasi ya Kamati ya Fedha na Utawala wajumbe hao wamempigia kura za ndio Gaidon Haule ambaye alikuwa peke yake katika nafasi hiyo.

Waliochaguliwa kuwa wajumbe wa kamati ya maadili amati ya maadili wajumbe hao wamemchagua Novatus Marandu ambaye amepata kura 15 na Kamati ya Maendeleo na Uwezo akichaguliwa Rhobi Samweli,Kamati ya Utandaa na Mawasiliamo akichaguliwa Asifiwe Mallya huku wajumbe wanne wa Bodi wakiwa ni Jane Magigita,Revocatus Sono,Paulina Majogoro na Baltazari Komba.

Akizungumza mara baada ya kutangazwa kwa matokeo Mwenyekiti mpya Baraza hilo,Badi ameomba ushirikiano huku akiahidi kutekeleza yale ambayo aliahidi wakati wa kuomba kura.

“Mengi tumezungumza tumetoa ahadi nyingi kwa pamoja tutaenda kuyafanyia kazi yale tuliyoaahidi kikubwa naomba ushirikiano,”amesema.

Katibu mpya wa Baraza hilo,Sono amewashukuru wote waliomwamini kwa kumpigia kura ambapo amedai kwamba mchakato huo haukuwa mdogo.

Naye,Mwekahazina mpya Kiteve amesema watakuwa wasiri wa vikao kwa kutokutoa siri huku akidai kwamba watatoa ushauri sahihi kwa viongozi wa juu.

“Tutaendelea kumshauri Mwenyekiti pamoja na wengine tutakupa ushauri unaofaa (Mwenyekiti) sisi hatutoi siri na tutakuwa wasiri wa vikao,’’amesema.

Naye Mbunge wa Viti Maalum kupitia Asasi za Kiraia Tanzania Bara (NGOs) Neema Lugangira amewataka viongozi wapya kutokufanya kazi kwa kificho na badala yake wanatakiwa kuwa wawazi katika mambo yao pamoja na kufanya kazi kwa bidii ili waweze kuonekana.

Pia,amewataka kuwa wawakilishi wa NGOs zote kubwa na ndogo bila ya kuweka matabaka huku akisisitiza uchaguzi umeisha sasa ni wakati wa kuchapa kazi.

“Uchaguzi umeisha sasa tuwe pamoja.Rai yangu kamati ya mpito iendelee kuwa walezi wa hawa viongozi wapya,”amesema.

Naye,Mwenyekiti wa Bodi ya Uratibu wa Mashirika yasiyo ya Kiserikali,Dkt.Richard Sambaiga amewataka viongozi hao wapya kufanya kazi kwa tija,kuimarisha uhusiano wa NGOs ndani ya sekta huku akidai Bodi itatoa ushirikiano kwa baraza hilo.

Uchaguzi wa Baraza hilo ulipaswa kufanyika yangu mwaka 2019 na baada ya kuonekana kusuasua kufanyika kwa uchaguzi huo hivi karibuni Waziri wa Afya,Maendeleo ya Jamii,Jinsia ,Wazee na Watoto alitoa agizo kufanyika kwa uchaguzi huo na kuunda kamati ya mpito ya kusimamia na kuhakikisha uchaguzi huo unafanyika haraka.