Na Mwandishi Wetu, Timesmajira Online
MIAKA ya hivi karibuni kuliibuka mvutano mkubwa katika masuala ya kiutalii kati ya nchi ya Tanzania na Kenya, jambo ambalo lilitishia kwa kiasi kikubwa Sekta ya Utalii nchini kwa baadhi ya watalii kutoka mataifa ya Ulaya kubakia njia panda.
MWAKA 2020 hadi 2021 wakati wa mlipuko wa ugonjwa wa UVIKO-19, idadi ya watalii nchini ilishuka na kusababisha kuporomoka kwa pato katika sekta ya utalii nchini.
Idadi ya watalii ilipungua hadi kufikia 485,827 mwaka 2020 na hiyo ilitokana na UVIKO-19,huku mwaka 2021/2022 idadi ya watalii ilianza kupanda na kufikia watalii 997,87,na hali hiyo ya kuimarika kwa utalii nchini iliendelea kupanda ambapo mwaka 2022/2023 idadi ya watalii waliongezeka na kufikia 1,670,437.
Hivyo Serikali kupitia Wizara ya Utalii na Maliasili,ilikuja na mkakati wa kurudisha hadhi ya utalii nchi kuanzia utalii wa ndani hadi wa kimataifa kwa kuwa na kampeni nyingi za kuhamasisha na kutangaza vivutio vya utalii hapa nchini.
Katika kushinda vita hivi ya kupungua kwa watalii nchini Rais Samia Suluhu Hassan,akaja na filamu iliyopewa jina la Royal Tour,ambapo inakadiriwa kwa mara ya kwanza kuzinduliwa ilitazamwa, kufuatiliawa na watu bilioni 1.2,nakufanya hifadhi za taifa kuvunja rekodi kwa kupata jumla ya watalii 1,412,719 kwa kipindi cha miezi tisa, idadi ambayo haijawahi kutokea.
Kutokana na maono hayo ya Rais Dkt. Samia kumekuwa na ongezeko la mapato ya utalii maradufu ambapo mapato ya jumla ya sekta yameongezeka kutoka Dola za Marekani zaidi ya bilioni 1.3(sawa na trilioni 3.01) mwaka 2021 hadi dola za Marekani bilioni 2.527.77 (sawa la Sh trilioni 5.82).
Mafanikio ya TANAPA kwa kipindi cha miaka mitatu ya Rais Samia
Kwa mujibu wa Shirika la Taifa la Uhifadhi (TANAPA),limepata mafanikio kwa hifadhi za taifa kutembelewa kwa idadi kubwa ya watalii katika kipindi cha kuanzia Julai 2023 hadi Machi 19, 2024,ambapo watalii 1,514,726 walitembelea vivutio na hifadhi za wanayama, Watalii wa ndani wakiwa 721,543 na wa nje wakiwa 793,183, sawa na ongezeko la asilimia 5,ikiwa ni zaidi ya lengo la kupokea watalii 1,387,987, wa nje 827,713 na watalii wa ndani 726,676 katika kipindi husika.
Shirika linasimamia hifadhi za taifa 21 zenye eneo la ukubwa wa kilomita za mraba 96,908.88 ambalo ni sawa na asilimia 10 ya eneo lote la nchi.
Kamishina Mkuu wa Uhifadhi, Mussa Kuji, ameyataja mafanikio ya shirika hilo kwa kipindi cha miaka mitatu ya Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan chini ya uratibu wa Ofisi ya Msajili wa Hazina jijini Dar es Salaam.
Mafanikio hayo ni ongezeko la siku za kukaa wageni kutoka wastani wa siku 1,749,194 katika mwaka wa fedha 2021/2022 hadi kufikia wastani wa siku 2,669,586 kufikia Februari 2024 ambalo ongezeko hilo limechangia mapato.
Kuongezeka kwa uwekezaji ambapo kwa mujibu wa ripoti ya Kituo cha Biashara nchini (TIC), hamasa na mguso wa filamu ya Royal tour imeongeza idadi ya wawekezaji nchini ikiwemo uwekezaji wa jumla.
“TANAPA imeendelea kupata tuzo zinazotolewa na taasisi ya ESQR kwa kipindi cha miaka minne mfululizo, ambazo kati ya hizo tuzo za miaka mitatu mfululizo zimepatikana katika kipindi cha uongozi wa Serikali ya Awamu ya Sita kwa kiwango cha “Platinum category” mwaka 2021, “Gold category” mwaka 2022 na “Diamond category” mwaka 2023,”amesema Kamishina Kuji.
Kamishina huyo anasema Hifadhi ya Taifa Serengeti imepata tuzo itolewayo na shirika la “World Travel Awards (WTA)” ya kuwa hifadhi bora barani Afrika kwa miaka mitano mfululizo (2019 hadi 2023). Tuzo tatu (3) kati ya hizo tano (5) zimepatikana chini ya uongozi wa Serikali ya Awamu ya Sita (tuzo za mwaka 2021 hadi 2023).
Hifadhi ya Taifa Tarangire na Kilimanjaro zilipata tuzo mara mbili mfululizo kwa mwaka 2021 na 2022 ya kuwa vituo vyenye mvuto katika utalii,na tuzo hizo hutolewa na jukwaa la kimataifa lijulikanalo kwa jina la “Trip Advisor”.
Pia kampuni ya Explore Worldwide yenye makao yake makuu nchini Uingereza mwaka huu 2024 imeutambua Mlima Kilimanjaro kuwa namba moja ya Alama za Asili za kudumu na zinazokumbukwa zaidi ulimwenguni (World’s topmost unforgettable natural landmarks).
Amesema Tuzo hizo zimeliongezea Shirika kuaminiwa na wateja mbalimbali na kutoa uhakika kwao kuhusu aina ya huduma zitolewazo, kutambulika zaidi na kuongeza idadi ya watalii pamoja na kutoa uhakika kwa watalii na wadau wa utalii kuhusu ubora wa hifadhi.
Alisema kuwa, katika mafanikio hayo ni pamoja na kuwepo na ongezeko la wawekezaji kwenye maeneo ambayo yaliyokuwa hayana mvuto kwa wawekezaji zikiwemo Hifadhi za Ruaha, Saadani na Mikumi ikiwa na Jumla ya maeneo mapya ya uwekezaji 176 (34 ni loji na 142 ni kambi) yameainishwa katika Hifadhi zote kwa kuzingatia mipango ya uendeshaji wa kila Hifadhi na yametangazwa kwenye tovuti ya Shirika.
Kuji aliendelea kuyataja mafanikio ya Royal Tour kuwa ni kuongezeka kwa wigo wa shughuli za utalii wa puto (balloon) kutoka kufanyika katika Hifadhi ya Taifa Serengeti kwenda hifadhi za Tarangire, Ruaha na sasa maandalizi yanaendelea kwa hifadhi ya Mikumi; Utalii wa faru (Hifadhi ya Taifa Mkomazi), utalii wa baiskeli (Hifadhi ya Taifa Kilimanjaro na Arusha.
Kutambuliwa kwa TANAPA mwaka 2021 na International Standard Organisation (ISO) kumepelekea wateja kuamini na kuchagua huduma zinazotolewa na TANAPA na hifadhi zake hivyo kuongeza idadi ya watalii na mapato.
Katika miaka mitatu ya Rais Dkt Samia Suluhu Hassan, Shirika limeendelea kutekeleza shughuli za utalii na uhifadhi kwa kuzingatia matakwa ya kiwango cha ubora cha ISO 9001:2015 kinachohusu utoaji wa huduma bora kwa wateja.
“TANAPA imeendelea kuimarisha miundombinu ya ukusanyaji wa mapato ikiwemo kukamilisha ujenzi wa lango la kisasa la Naabi lenye uwezo wa kupokea zaidi ya magari 600 na wastani wa wageni zaidi ya 1,500 kwa siku. Katika kipindi cha miaka mitatu TANAPA pia imeweza kujenga malango mapya 10 na ya kisasa katika Hifadhi za Taifa Tarangire (2), Mkomazi (3), Serengeti (2) na Nyerere (3), “
Hata hivyo amesema kuwa “kupitia mradi wa REGROW, Shirika limewezesha mafunzo kwa askari wa vijiji (Village Game Scout – VGS) 354 kutoka vijiji 39 ili kuwezesha kukabili kwa wakati matukio ya wanyamapori wakali na waharibifu kutambua mienendo yao ili kurahisisha udhibiti wanapotoka nje ya maeneo ya hifadhi.”
Aidha, Shirika linaendelea na ujenzi wa vituo 8 vya Askari Uhifadhi katika maeneo ya kimkakati yaliyopo katika vijiji vinavyoathirika zaidi katika wilaya za Mbarali, Kalambo, Kilwa, Namtumbo, Ruangwa, Serengeti, Bunda na Bariadi. Vituo hivi vitasaidia askari kudhibiti kwa wakati wanyamapori wakali na waharibifu, yote ni mchango wa Rais wa kuwathamini wananchi na wanyama wetu.
Mafanikio mengine ya TANAPA ni kufanya jitihada mbalimbali za kuhakikisha kuwa linabuni vyanzo mbalimbali vya mapato ambavyo vitaliingizia Shirika fedha na kuongeza ukusanyaji wa mapato.
Miongoni mwa vyanzo bunifu vya mapato ambavyo vimeendelea kuibuliwa na Shirika ni pamoja na kuanzishwa kwa Kampuni Tanzu ya Uwekezaji ya Shirika (TANAPA Investment Limited – TIL) inayolenga kuimarisha usimamizi na utekelezaji wa miradi ya kimkakati na pia kuwa chanzo kikubwa cha mapato kwa Shirika kwa kutekeleza miradi mbalimbali Kuanzishwa kwa Kiwanda cha Ushonaji wa sare za watumishi na kupokea zabuni kutoka taasisi nyingine.
Ujenzi wa hoteli yenye hadhi ya nyota tatu katika eneo la Rubambagwe Wilaya ya Chato yenye vyumba 30 vya kulala; na Ujenzi wa Uwanja wa Gofu wa hadhi ya kimataifa wenye mashimo 18 uliopo eneo la Forti Ikoma – Hifadhi ya Taifa Serengeti.
Shirika limeendela kuimarisha uhifadhi wa wanyamapori walio katika hatari ya kutoweka na kuwezesha kuongezeka kwa idadi ya Wanyama hao wakiwemo faru, mbwa mwitu na sokwe.
“Serikali ya awamu ya sita imeweka mazingira wezeshi kwa Shirika kusimamia maliasili zilizopo katika Hifadhi za Taifa hapa nchini pamoja na upatikanaji wa rasimilimali fedha, rasilimali watu na vitendea kazi kama magari, mitambo ya kutengeneza barabara na mafunzo kwa watendaji.” alisema Kuji.
Miongoni mwa mafanikio yaliyopatikana ni pamoja na Kudhibiti uwindaji wa wanyama adimu ambapo hakukuwa na tukio la kuuawa kwa Faru, Sokwe au Mbwa mwitu.
Kwa upande wake Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii, Dkt. Hassan Abbasi anasema kuwa, kumekuwa na mafuriko katika viwanja vya ndege ambapo Uwanja wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA) Ndege za kimataifa zimeongeza ruti Tanzania; miruko ya jumla ya ndege za kimataifa KIA iliongezeka kwa asilimia 28 kutoka miruko 6,115 Aprili 2021 hadi 7,850 Aprili, 2023; Qatar Air,
Na ndege ya KLM wameongeza miruko kwa siku; mashirika haya mawili yameongeza miruko kutoka tisa hadi 12 (ndege mbili kwa siku) na miruko mitano hadi sita mtawalia kutokana na kuongezeka abiria baada ya kutazama filamu ya Royal Tour.
“Ndege ya Eurowings Discover (Lufthansa Group) ilianza Juni 2022 kuja Tanzania mara mbili kwa wiki moja kwa moja kutoka Frankfurt, Ujerumani kuleta watalii wa Ujerumani na Ulaya kwa ujumla,” alisema Dkt. Abbas.
Alisema kuwa kupitia mafanikio haya Tanzania sasa imepata morali ya kwenda kimataifa zaidi kuitangaza Tanzania.
***Changamoto
Anasema mbali na mafanikio, lakina pia Shirika linakabiliwa na changamoto mbalimbali zikiwemo Mabadiliko ya tabia nchi; (ukame, mafuriko, uwepo wa mimea vamizi inayoathiri upatikanaji wa chakula na mizinguko ya wanyamapori, uwepo wa ujangili ,matukio ya uingizwaji wa mifugo ndani ya hifadhi,Matukio ya wanyamapori wakali na waharibifu katika maeneo ya jamii.
Shirika limeendelea kujiimarisha katika jitihada za utatuzi wa changamoto miongoni mwa mikakati inayoendelea kutekelezwa kama sehemu ya kukabiliana na baadhi changamoto zilizopo za uhifadhi na utalii ni pamoja Kutoa elimu ya uhifadhi kwa jamii.
Naye Waziri wa Maliasili na Utalii , Balozi Dkt Pindi Chana amezitaka taasisi zilizoko chini ya wizara ya Maliasili na Utalii kufanya kazi kwa kushirikiana ili kuboresha utendaji kazi wa taasisi hizo na kuleta tija kwa nchi.
Balozi Chana alitoa kauli hiyo Oktoba 16,2024 wakati akizungumza na menejimenti ya mamlaka ya hifadhi ya Ngorongoro (NCAA) katika kikao kilichofanyika jengo la kitega uchumi la Ngorongoro jijini Arusha.
Ambapo amesisitiza kuwa kama kuna huduma ambazo zinatolewa na taasisi moja wapo zilizopo ndani ya Wizara hiyo ni muhimu kushirikiana ili kurahisisha utendaji kazi na hivyo kuongeza ufanisi katika utendaji kazi katika Sekta ya uhifadhi na utalii.
“Fuateni sheria na taratibu zilizopo ili kuongeza ushirikiano wa taasisi zote, nawasisitiza pia kujenga utamaduni wa kutembeleana kwa lengo la kujifunza, na kama kuna uwezekano wa kusaidiana vifaa vya kufanyia kazi katika maeneo mbalimbali saidianeni ili kuondoa changamoto katika taasisi fanyeni hivyo .” akisema Waziri Chana.
Aidha, balozi dkt Pindi Chana imeipongeza mamlaka ya hifadhi ya Ngorongo kwa kuweza kukusanya jumla ya shilingi bilioni 96.7 katika robo ya kwanza ya mwaka 2024/25 ukilinganisha na robo ya kwanza ya mwaka wa fedha 2023/2024 ambapo mamlaka hiyo ilikusanya shilingi bilioni 68.
Huku, Kamishna wa Uhifadhi wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro Dkt. Elirehema Doriye alimweleza Waziri Chana kwamba mamlaka inaendelea kutekeleza majukumu yake kwa umakini ili kuhakikisha kuwa inafikia malengo iliyojiwekea ya kuboresha shughuli za uhifadhi na kuongeza idadi ya watalii ili kufikia malengo yaliyowekwa na serikali ya awamu ya Sita (6) inayoongozwa na Rais Dkt Samia.
Kijana wa kitanzania, Allen ameamua kuunga mkono juhudi na mafanikio ya Rais Dkt Samia kwa kufanya utalii wa ndani na kutembelea vivutio vya utalii ndani na kuamamua kuanziasha ukurasa wake katika mtandao wa Facebook na Instagram uitwao All about Tanzania Life katika kuvutia watalii wa nje na ndani.
Kijana huyu mwenye ndoto na hali ya kuzunguka kona zote za nchi na kuhamasisha watanzania kufanya utalii wa ndani kwa kuwaonyesha maeneo mbalimbali na vivutio vilivyopo Tanzania ameweza kutembelea zaidi ya nusu ya mikoa kote Tanzania (mikoa 24) na kufika katika wilaya nyingi hapa Tanzania.
“Kutokana na jitihada za Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kuhamasisha na kutangaza vivutio vyetu vya utalii niliamua kuanza kuzunguka nchini kutanganza, kuahasisha na kutembelea vivutio vya utalii, na nimezunguka zaidi ya mikoa 24 hapa nchi na lengo langu ni kufikia mikoa yote nchini,
Na kuuwafanya watanzania kuwa watu wa kwanza kabisa kutembelea vivutio vyao na maeneo yao ya kitamaduni na urithi wa kitaifa nimeweza kuonyesha mfano na kuyatembelea maeneo mengi nchini yenye historia pana na maisha ya watanzania tokea zama za kale na hata sasa na kuonyesha kuwa inawezekana na ni rahisi watu kufikia matamanio yao na kusaidia kukuza uchumi wa nchi yetu, ” anasema kijana Allen.
Katika kuunga mkono juhudi za Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan karika Utalii nchini Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Paul Makonda aliaandaa tamasha la magari 1000 aina ya Land Rover kutoka nchi mbalimbali lililofanyika kwa siku tatu (3) lenye lengo la kutangaza utalii pamoja na kufungua fursa mbalimbali za kiuchumi kwa wakazi wa mkoa wa Arusha kwa kuwa na matukio mbalimbali yatakayokusanya idadi kubwa ya watu na hivyo kuchangia kukuza pato la mwananchi mmoja mmoja, mkoa na nchi kwa Ujumla.
Tamasha hilo la siku tatu, lilianza Oktoba 12 na kutamatika siku ya Oktoba 14, huku shughuli za tukio hilo zikianzia eno la Kingori nje kidogo ya jiji la Arusha kwa mkusanyiko mkubwa wa magari ambapo kila gari lilibandikwa namba yake ya ushiriki.
Msafara huo ulianza polepole ukikatiza maeneo mbalimbali ya jiji hilo ambapo wakazi walifurika kushuhudia, kwa mujibu wa kitabu cha Guinness rekodi ya sasa ya dunia ya mkusanyiko wa magari mengi ya Land Rover ni ya mwaka 2018 ikishikiliwa na jimbo la Bavaria nchini Ujerumani ambapo magari 632 yalijitokeza na kutengeneza msafara uliofika umbali wa kilometa 7.4.
Tamasha hilo la Land Rover Festival, liliratibiwa na Mkuu wa Mkoa wa Arusha Paul Makonda lina lengo la kuutangaza utalii na vivutio vilivyopo Tanzania, mbali na Land Rover Festival pia baadhi ya wageni kama wacheza filamu kutika Hollywood, wacheza mpira na watu maarufu duniani wamefuka nchini na kutembekea mbuga ya Serengeti na Mlima Kilimanjaro pia Wanachma wa Klabu ya mpira ya Manchester United kupitia taasisi yao wamefuka nchini na kupanda Mlima kilimanjaro kwa lengi la kuchangisha fedha, haya yote ni mafanikio ya Rais Dkt. Samia kupitia filamu ya Royal Tou
More Stories
Siri ya Rais Samia kutembea kifua mbelea kijivunia Mapinduzi Matukufu ya Z,bar
Rais Samia anavyotimiza ahadi yake ya kumtua ndoo ya maji mwanamke
Rais Samia anavyozidi kusogeza karibu watoto wa kike na kasi ukuaji teknolojia