Na Mwandishi Wetu, Timesmajira Online
UBORESHAJI wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura Mkoa wa Singida, sehemu ya mkoa wa Dodoma na sehemu ya mkoa wa Manyara utaanza tarehe 25 Septemba, 2024 hadi tarehe 01 Oktoba, 2024.
Makamu Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Jaji wa Mahakama ya Rufaa Mstaafu, Mbarouk Salim Mbarouk ameyasema hayo leo Septemba 13, 2024 jijini Dodoma, wakati akifungua mkutano wa wadau wa uchaguzi ikiwa ni maandalizi ya zoezi hilo.
“Mzunguko wa tano wa uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura utajumuisha mkoa huu wa Dodoma katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Halmashauri za Wilaya ya Bahi, Chamwino na Kongwa.
“Mkoa wa Manyara katika Halmashauri ya Mji wa Mbulu na Wilaya ya Kiteto na Simanjoro na mkoa wa Singida ambapo uboreshaji utaanza tarehe 25 Septemba, 2024 hadi tarehe 01 Oktoba, 2024 na vituo vitakuwa vinafunguliwa kuanzia saa 2:00 asubuhi na kufungwa saa 12:00 jioni,” amesema.
Amefafanua kuwa uboreshaji wa Daftari utahusu kuwaandikisha raia wa Tanzania waliotimiza umri wa miaka kumi na nane na zaidi au watakaotimiza umri huo wakati au kabla ya tarehe ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2025 na ambao hawajapoteza sifa kwa mujibu wa sheria ya uchaguzi au sheria nyingine yeyote.
Katika hatua nyingine, akifungua mkutano wa wadau mkoani Singida, Mjumbe wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi ambaye pia ni Jaji wa Mahakama Kuu, Asina Omari amesema Tume katika kuhakikisha kwamba inaenda sambamba na mabadiliko ya teknolojia ikiwa ni pamoja na kurahisisha zoezi hili la uboreshaji wa Daftari, imeboresha mfumo wa uandikishaji ambao kwa mara ya kwanza utamuwezesha mpiga kura aliyepo kwenye Daftari kuanzisha mchakato wa kuboresha taarifa zake au kuhama kituo kwa kutumia aina zote za simu au kompyuta.
“Wanaotumia simu za kawaida (maarufu kama kitochi au kiswaswadu) nao wanaweza kutumia huduma hii kwa kupiga namba 15200# na kisha watabonyeza namba 9 halafu wataendelea na hatua zingine kama itakavyokuwa inaelekezwa kwenye simu husika,” amesema.
Jaji. Asina amefafanua kuwa mtumiaji wa huduma hii, atatakiwa kufika kituo anachokusudia kujiandikisha ili akamilishe hatua za kupigwa picha, kuweka saini na kupatiwa kadi yake ya mpiga kura.
Uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura ulizinduliwa mkoani Kigoma tarehe 20 Julai, 2024 sambamba na kuanza kwa uboreshaji kwenye mikoa mitatu ya Kigoma, Tabora na Katavi na kufuatiwa na mikoa ya Geit, Kagera, Mwanza, Shinyanga, Mara, Simiyu na Manyara katika Halmashauri za Wilaya ya Babati, Hanang, Mbulu na Mji wa Babati.
Kwa mujibu wa ratiba iliyotolewa na Tume awamu ya kwanza ya uboreshaji wa Daftari inatarajiwa kukamilika mwezi Machi, 2025.
More Stories
Tanzania kuwa mwenyeji Mkutano wa Kimataifa matumizi bora ya Nishati
Madiwani Ilala watoa chakula kwa watoto yatima
Waziri Mkuu: Tumieni matokeo ya tafiti za kisayansi katika utekelezaji wa mipango ya kitaifa