March 29, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

UBALOZI wa Ufaransa Nchini Tanzania, Wepresent Tanzania waandaa Tamasha la Hip Hop Asili

Na David John, Timesmajira Online

UBALOZI wa Ufaransa Nchini Tanzania kwa kushirikiana na Wepresent Tanzania wameandaa Tamasha la Hip Hop Asili ambalo linatarajia kufanyika kwa siku tatu kuanzia Juni 23 hadi 25 katika ukumbi wa Alliance Francaise Jijini Dar es salaam.

Tamasha hilo ambalo ni la awamu ya pili linatarajia kuwauganisha wasanii mbalimbali ambao watapata fursa ya kuonesha vipaji vyao sambamba na kutoa burudani ya aina yake kwa waudhuriaji.

Akizungumza na waandishi wa habari Jijini Dar es salaam jana Balozi wa Ufaransa Nchini Tanzania, Nabil Hajlaoui alisema Tamasha hilo limelenga kusherekea utamaduni wa Hip Hop Afrika Mashariki ikiwa ni pamoja na sanaa mbalimbali ikiwa ni pamoja na uchoraji, uimbaji.

Amesema Tamasha hilo ni muendelezo wa tamasha lililofanywa na baadhi ya wana Hip Hop 30 wa Afrika Mashariki na Ufaransa Octoba Mwaka jana.

Balozi Hajlaoui amesema Tamasha hilo litapambwa na wasanii Octipizzo kutoka Kenya, Tina Mweni (Kenya, Denmark), Rise up Band(Tanzania, Ufaransa), Jay Moe(Tanzania), The Mc 225 (Tanzania), Mic Crenshaw .(US), Lord Eyes( Tanzania) .

“Wasanii kutoka nchi ya Kenya, Uganda, Rwanda , burundi, Kongo, Ghana, Mayotte, Ufaransa na Marekani wataungana na wasanii wengine 36 waliochaguliwa katika mashindano ya Hip Hop Asili kutoka katika mikoa sita”amesema Balozi Hajloui

Ameongeza kuwa Juni 24 kupitia tamasha hilo kumeandaliwa shindano la Break Dance la Afrika Mashariki ili kupata bingwa wa Tanzania ambaye atakwenda kwenye Battle of the year 2022 Tokyo Japan.

Aidha amesema kupitia tamasha hilo watarajia zaidi ya watu 1500 kuhudhuria ili kupata burudani kutoka kwa wasanii mbalimbali wenye vipaji vya asili.

Naye Mkurungezi wa miradi wa Tamasha la Festival Hip Hop Asili , Matei Babu amesema walifanya usaili wa kutafuta vijana wenye vipaji katika mikoa sita ambapo walifanikiwa kupata wasanii 36.

Akitaja mikoa hiyo ni pamoja na Mwanza, Arusha, Mbeya, Dodoma, Dar es salaam pamoja na Zanzibar.

Amesema wasanii hao waliopatikana katika usaili watapewa mafunzo ya siku tatu ambayo tayari yameishaanza na yanatarajia kukamilika Juni 22.

“Kupitia warsha hizo wasanii watapata maudhui ya historia ya Hip Hop Tanzania, Sanaa ya Emcee, Breakdance pamoja na Beat box na muwezeshaji atakuwa Bbyo Lilou kutoka Ufaransa ambaye ni Bingwa wa dunia wa breakdance, mwingine Deejay PH kutoka Ufaransa, Mejah Mbuya kutoka Tanzania”amsema Babu

Mkuki Byoga ni Mwenyekiti wa Alliance Francise ambao ni wenyeji wa Tamasha alisema Tamasha hilo linajumuisha umuhimu mkubwa kwa kuonesha mitindo mbalimbali .

Amesema kutakuwa na tiketi za aina mbili ambazo ni tikiti ya pass ya Tamasha kamili na tikiti ya siku kwa bei ya shilingi 20,000, na elfu 10000.

Balozi wa Ufaransa Nchini Tanzania, Nabil Hajlaoui akizungumza na waandishi wa habari awapo pichani kuhusu tamasha la awamu ya pili la Hip Hop Asili linalotarajia kuanza kesho
Mwenyekiti wa bodi ya Alliance Mkuki Byoga akizungumza kuhusu umuhimu wa tamasha hilo kwa vijana
Mkurugenzi wa kituo cha utamaduni cha Alliance Francaise Frola Valleur (katikati) akizungumza wakati wa hafla hiyo ya kuzindua Tamasha la Hip hop Asili 2022