April 28, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Ubakaji,ulawiti wa watoto vyawachukiza wabunge,wataka hatua kali zaidi zichukuliwe kwa wahalifu wa vitendo hivyo

Na Joyce Kasiki,Timesmajira online,Dodoma

BAADHI ya wabunge wameonyesha kuchukizwa na vitendo vya ukatili vinavyoendelea hapa nchini hususan matukio ya ulawiti na ubakaji wa watoto ambapo wametoa maoni tofauti huku baadhi yao wakitaka wanaume wanaofanya vitendo hivyo wahasiwe ili kuwanusuru watoto dhidi ya vitendo vya ubakaji na ulawiti.

Wakichangia mjadala wa Bajeti ya Wizara ya Maendeleo ya Jamii ,Jinsia,Wanawake na Makundi Maalum ambayo imeomba shilingi bilioni 43.403 kwa mwaka wa Fedha wa 2022/23 bungeni jijini Dodoma,wabunge hao wamesema matukio hayo ni miongoni mwa mambo ambayo yanaathiri malezi na makuzi ya watoto wadogo na hivyo kuathiri makuzi  katika maisha yao.

Mbunge wa Viti Maalum Subira Mgalu amesema, takwimu za matukio ya ukatili zinatisha huku akisema kwa kipindi cha Januari 2019 mpaka sasa matukio hayo jumla yake ni takribani 29,000 lakini miongoni mwao kubakwa ni takribani 19,000 sawa na asilimia 70 huku yaliyofikishwa mahakamani yakiwa ni asilimia 75 na yaliyohukumiwa ni kama asilimia 67.

“Tatizo hili ni kubwa na katika moja ya changamoto ni matukio ya kulawiti ambapo watoto wa kiume zaidi ya 3000 kati ya 3,260 sawa na asilimia 64 wamelawitiwa,hali hii inatisha mpaka tunatamani kama adhabu iongezwe ,au tuseme wanaume wahasiwe ,hii yote ni kuona namna gani tuanweza kuondoa ukatili huu wa ulawiti na ubakaji wa watoto,

“Serikali inafanya maendeleo kwa ajili ya kizazi cha sasa na kijacho lakini maendeleo haya yatakuwa hayana maana kama tunaandaa kizazi cha watoto wanaobakwa ,watoto wa kiume wanaolawitiwa,

“Kwa hiyo naiomba Serikali kupitia Wizara mtambuka zinazohusika katika eneo hilo ,kuangalia sheria kwani pamoja na kwamba zipo lakini haipiti wiki yanasikika matukio ya ubakaji,ulawiti wa watoto,

“Na kinachosikitisha zaidi matukio yameambukiza ndani ya familia,unakuta baba anabaka watoto wake ,baba analawiti watoto wake,tumnwombe mwenyezi Mungu atuongoze tuondokane na haya matukio.”

Mbunge huyo aliwaasa watanzania kutahimini kwa matukio hayo ambayo yamekuwa yakijiotokeza  kila siku huku akiiomba mahakama mahakama iendelee kutenda haki katika kuhakikisha walawiti na wabakaji wa watoto wanachukuliwa hatua stahiki.

Kwa upande wake Mbunge wa Viti Maalum Fatma Toufiq (CCM)  amepongeza mikakati mbalimbali  ya serikali iliyopo ambayo inalenga kuhakikisha ukatili unatokomezwa kupitia Mpango wa Mpango Kazi wa Taifa wa Kutokomeza Ukatili dhidi ya Wanawake na Watoto (MTAKUWWA)  ambao una dhamira ya kuhakikisha ukatili dhidi ya wanawake na watoto unatokomezwa kwa asilimia 50 ifikapo Juni 2022.

Hata hivyo amesema,kumekuwa na ukatili mwingi hapa nchini ukiwemo wa kingono ,vipigo ,kuuawa,kuchomwa moto watoto,usafirishaji watoto,ubakaji wa watoto,ulawiti wa watoto,huku akisema,kwa matukio hayo inaonyesha ukatili umekithiri kupita kiasi .

“Na pia kwa kuwa vyombo vya habari vimekuwa vikitoa taarifa mbalimbali vimekuwa vikiripoti kuwa wahusika wa matukio ya ukatili hususan wa ubakaji wa watoto ni pamoja na ndugu wa karibu ambao ni baba ,ndugu wa karibu wanabaka na kulawiti watoto vitendo ambavyo vina athari kubwa katika Malezi ,Makuzi na Maendeleo ya mtoto,

“Nitoe mfano wa matukio ambayo yameripotiwa hivi karibuni Mkoa wa Kilimanjaro kuna mume amemuua mkewe mbele ya mtoto wake wa miaka miwili,sasa huyu mtoto akikua akili yake itakuwaje hilo ni tatizo,kuna mtoto alinyongwa Machi mwaka huu ,kuna tukio la baba kumuua mtoto wake kwa kushindwa kusoma ,kuna mama mkubwa naye amemuua mtoto wa mdogo wake,kwa hiyo mambo haya yanatisha ,.”amesema Toufiq

Mbunge huyo pia ameiasa Serikali kutupia macho shuleni huku akisema kuna matukio ya ubakaji na ualwiti yamekuwa yakifanyika huko kwa watoto walio katika madarasa ya juu kuwafanyia vitendo hivyo watoto wenzao wa madarasa ya chini .

“Baadhi ya shule zetu nazo siyo salama,baadhi ya watoto wa madarasa ya juu wamekuwa wakiwalawiti watoto wa madarasa ya chini na hili jambo nalo inapaswa tuliangalie kwa kuona jinsi tunavyoielimisha jamii,maana inawezekana baadhi ya tabia za watoto wanazirithi kutoka katika nyumba na familia zao.”

Kufuatia changamoto hizo za ukatili Toufiq ameishauri Serikali kuiangalia upya sheria ya kanuni ya adhabu kuhusu mimba zinazotokana na kubakwa na ndugu wa damu  ili iwaondolee sonona walengwa (wasichana) na kama itafaa ujauzito utolewe na wataalam.

Ameiomba Serikali kuchukua hatua kwa wazazi wa kiume wanaotelekeza watoto wao kwa sababu baadhi ya akina mama wanashindwa kuwalea watoto na hivyo kuathiri Malezi na makuzi yao na hatimaye kushindwa kukua hadi kufikia utimilifu wao.

Awali Waziri wa Maendeleo ya Jamii ,Jinsia,Wanawake na Makundi Maalum Dkt.Dorothy Gwajima alisema, pamoja na hatua za kila siku za Serikali na wadau mbalimbali kupambana na ukatili kupitia MTAKUWWA, Wizara inaratibu utekelezaji wa kampeni kubwa ya kupambana na ukatili sambamba na kuimarisha mifumo ya kubaini viashiria vya ukatili na kuchukua hatua za kuzuia.
Aidha alisema,kwa kuwa utekelezaji wa MTAKUWWA unafikia ukomo mwezi Juni mwaka huu, Wizara imeanza mchakato wa kufanya tathmini ya Mpango huo kwa lengo la kubaini mafanikio  yaliyopatikana katika utekelezaji kwa kipindi cha miaka mitano, changamoto na upungufu wa kimuundo na kiutendaji ulioathiri kufikiwa kwa malengo ya Mpango.

“Tathimini inatarajiwa kubainisha masuala ya kuigwa  na kutoa mapendekezo ya namna bora zaidi ya kukabiliana na changamoto
na upungufu uliobainika,matokeo au mapendekezo  yatakayobainishwa katika taarifa ya Tathmini ya Mpango yatawezesha kuanza kwa maandalizi ya MTAKUWWA awamu ya pili itakayotoa mikakati mahsusi ya kutokomeza aina zote za ukatili dhidi ya  wanawake na watoto kwa miaka mitano ijayo.”amesema Dkt.Gwajima

Kwa mujibu wa Dkt.Gwajima ,tathmini na Maandalizi ya MTAKUWWA II yanatarajiwa kukamilika ifikapo mwezi Septemba, 2022.

Akizungumzia kuhusu uratibu na utekelezaji wa MTAKUWWA Waziri huyo alisema,Wizara imeendelea kuratibu utekelezaji wa Mpango  huo kupitia maeneo nane ya utekelezaji.

Amesema mpango huo ambao utekelezaji wake  ulianza Julai, 2017 na kutarajiwa kufikia  ukomo Juni mwaka huu, baadhi  ya mafanikio yake ni  Matukio ya ukatili wa kijinsia yaliyoripotiwa katika Dawati la Jinsia na Watoto la Polisi yamepungua kwa asilimia kutoka matukio 42,414 mwaka 2020 hadi matukio 29,373 mwaka 2021.

Aidha, matukio ya ukatili wa kijinsia kwa watoto yaliyoripotiwa
kwenye Dawati hilo yamepungua kwa asilimia 28 kutoka matukio 15,870 mwaka 2020 hadi matukio 11,499 mwaka 2021.
Dkt.Gwajima amesema,mafanikio mengine ni kuanzishwa kwa vituo vya mkono kwa mkono ambavyo hadi Aprili 2022, jumla ya Vituo 21
vya Mkono kwa Mkono (One Stop Centers) vimeanzishwa katika Hospitali mbalimbali za Serikali kwenye Mikoa 12 ikilinganishwa
na Vituo 14 vilivyoanzishwa hadi kufikia mwaka 2020/21.

Amesema,lengo la vituo hivyo ni  kuwezesha utoaji wa huduma hizo katika eneo moja ili kuepusha usumbufu, ucheleweshaji wa huduma, kuharibu au kupoteza ushahidi.

Waziri huyo alisema,Serikali kwa kushirikiana na Wadau itaendelea kuratibu uanzishwaji wa Vituo vya Mkono kwa Mkono katika Mikoa ambayo haijaanzisha Vituo hivyo ikiwemo Mikoa ya Dodoma,
Singida, Tanga, Geita, Katavi, Rukwa, Mtwara, Lindi, Ruvuma, Mara, Kagera, Njombe, Songwe na Manyara.

“Vituo hivi vinarahisisha huduma kwa kumpa fursa manusura kufika katika kituo na kupata huduma za unasihi, utoaji taarifa kwa Afisa
wa Polisi na kupata matibabu lakini pia  vinarahisisha upatikanaji wa haraka wa ushahidi unaotokana na vipimo vya kitabibu unaowasilishwa katika Mahakama. “

Akizungumzia hali hiyo ya matukio mengi ya ukatili ,Danson Kaijage mkazi wa Ilazo jijini Dodoma  amesema,matukio hayo ya ulawiti ,ubakaji hususan wa watoto  yamekuwa yakitokea kwa wingi kutokana na ukosefu wa maadili na watu kutokuwa na hofu ya Mungu hali inayofanya jamii kukimbilia kwenye ushirikina ili kujipatia mali kirahisi badala ya kufanya kazi.

“Kinachotakiwa serikali iendelee kutoa elimu zaidi mashuleni kuwajengea uwezo wa kujieleza watoto kuanzia darasa la awali kwani matukio haya huwakumba hata watoto walio chini ya miaka mitano .”amesema Kaijage