Na Muandishi wetu, TimesMajira Online
Mkurugenzi Idara ya Mipango, Sera na Utafiti, Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Bi Daima Mohamed Mkalimoto amesema hatua ya uanzishwaji wa Jukwaa la haki za watoto kwa wadau wanayoshughulikia maendeleo ya watoto itasaidia kuweka pamoja na kuunganisha shughuli za watoa huduma za watoto.
Amesema hayo jana katika ukumbi wa UN Women wakati akifungua mkutano wa wadau wanaoshughulikia masuala ya Watoto kutoka taasisi za umma, binafsi na Washirika wa Maendeleo, ambapo mkutano huo ulilenga uanzishwaji wa Jukwaa la haki za Watoto Zanzibar.
Bi Daima amesema hatua hiyo itasaidia kuwaweka pamoja wadau hao katika uratibu wa utekelezaji wa shughuli zinazogusa Maendeleo ya watoto nchini.
Hivyo amewaomba wadau hao kutoa maoni yao ili yafanyiwe kazi na kuingizwa katika mapendekezo ya kuanzishwa kwa jukwaa hilo.
“Kuna umuhimu wa uratibu na usimamizi wa pamoja wa uanzishwaji wa jukwaa la haki ya watoto ili kuweza kutoa huduma bora za watoto katika mazingira na hali tofauti” Alisema bi Daima.
Akiwasilisha mapendekezo ya kuanzishwa kwa Jukwaa la haki ya watoto kwa wadau wanaoshughulikia Maendeleo ya watoto Zanzibar, Mshauri elekezi kutoka Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Watoto (UNICEF) na Mhadhiri kutoka Chuo Kikuu Huria Tanzania Dkt. Ladislaus Batinoluho ameipongeza Serikali ya Zanzibar kupitia Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa hatua nzuri iliyofikia kutokana na kazi kubwa wanayoifanya katika masuala mazima ya maendeleo ya watoto nchini.
Amesema pamoja na mafanikio hayo, bado watoto wanakabiliwa na changamoto mbali mbali ikiwemo utumikishwaji kwa watoto, kudhalilishwa, na kubakwa, hivyo wazo la UNICEF la kuanzishwa Jukwaa hilo litasaidia kuleta nguvu za pamoja katika kumkomboa mtoto.
Nao washiriki wa mkutano huo, wameshauri kuanza taratibu za kuanzishwa Jukwaa hilo ni vyema kuwashirikisha wadau na taasisi zote zinazoshughulikia watoto akiwemo Wizara ya Elimu, Wizara ya Afya, n.k ili kufikia malengo ya kuanzishwa kwa Jukwaa hilo la haki za watoto Zanzibar.
More Stories
Mjumbe wa Baraza UWT ahimiza wananchi kuwachagua viongozi wa CCM
CCM imejipanga kushinda kwa kishindo
Wanaotumia lugha za matusi,kashfa kwenye kampeni waonywa