December 25, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

TYC yawanoa Vijana 50 wajasiriamali,Wabunifu na Wamiliki wa Makampuni.

Na Penina Malundo,TimesMajira,Online

TAKRIBANI  vijana 50 kutoka mikoa mbalimbali ya Tanzania bara na Zanzibar,leo  wameanza kambi maalum mkoani Kilimanjaro kwa lengo la kupanua wigo wa kujifunza na kuongeza ufahamu juu ya masuala ya ujasiriamali na ubunifu.

Kambi hiyo inatarajia kukaa kwa siku tano mkoani humo na kuwajengea uwezo vijana hao kutoka mikoa mbalimbali.

 Mkurugenzi wa Shirika lisilo la Kiserikali linaloshughulikia masuala ya vijana nchini (TYC),Lenin Kazoba amesema kambi hiyo maalum kwa ajili ya kuwakutanisha vijana wanaoleta maendeleo katika jamii zao kupitia miradi ya kibunifu wanayoitekeleza.

Amesema vijana wamekuwa wakifanya jitihada kubwa kupambana na umasikini kujiongezea kipato lakini zaidi kutatua changamoto zinazowakabili ikiwemo Changamoto ya ukosefu wa ajira.

‘’Pamoja na jitihada zote zinazofanywa na vijana zipo changamoto nyingi ambazo zimekuwa zikiwakabili vijana na kuwarudisha nyuma ikiwamo kukosa ushirikiano wa kutosha kutoka katika sekta binafsi hasa uwezeshaji na uwekezaji katika mawazo na kazi za kibunifu zinazofanywa na vijana,’’amesema na kuongeza

‘’kukosekana kwa majukwaa ya kuwakutanisha vijana mara kwa mara waweze kubadilishana uzoefu na kujifunza zaidi pamoja na kukutana na watendaji wa serikali na sekta binafsi,’’amesema

 Kazoba amesema TYC imejijengea utaratibu wa kuandaa kambi ili iweze kupunguza kama si kumaliza changamoto hizo kwa kuwakutanisha vijana na wadau mbalimbali wa maendeleo ya vijana wakiwemo wawakilishi wa serikali,mashirika binafsi na taasisi za kifedha ili iweze kupunguza ama kumaliza kabisa changamoto hizo.

Msajili wa Mashirika yasiyo ya kiserikali ,Vickness Mayao amesema alisema Serikali ina mipango mingi madhubuti ya uwezeshaji wa makundi mbalimbali ikiwemo vijana katika kuhakikisha inaboresha mazingira ya uwezeshaji wa vijana na kuwapatia fursa mbalimbali ikiwemo Mikopo.

“Serikali imekuwa ikishirikiana na wadau mbalimbali wa maendeleo ikiwemo sekta binafsi na mabenki kuwawezesha kufanikisha kupata mikopo na kuendeleza mashirika yao,”amesema Mayao

Mayao amesema kuwepo kambi kama hizi zinasaidia kwa kiasi kikubwa kusaidia vijana kuweza kufikia malengo mbalimbali kwa maendeleo endelevu .