January 8, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Twenzetu Makumbusho na ndoto ya Samira

Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online

Ndoto za Samira ni filamu inayoelezea maisha yake na changamoto alizozipata katika malezi yake akiwa mtoto wa kike, ndoa ya utotoni alipitia wakati huo na hatimaye kuweza kutimiza ndoto yake baada ya kuvumilia bila kuchoka.

Alisema haikuwa rahisi kwake akiwa mtoto wa kike aliyefiwa na mama yake katika umri wake mdogo na kuendelea kukimbiza ndoto yake ya kuwa mwalimu. Sasa yeye ni mwalimu kitaaluma na anafanya kazi katika shule ya Sister Island huko Zanzibar kama mkuu wa skuli hiyo.

Nino Tropiano mtayarishaji wa filamu kutoka Italia alianza kuandika maisha yake alipokuwa shule ya sekondari alipokuwa akitafuta mojawapo ya kesi nyingi zinazowapata wasichana wa Zanzibar na Tanzania kwa ujumla.

“Ni filamu inayoelezea kwa kina maisha yangu ya utotoni hasa changamoto nilizokutana nazo kufikia hatua hii kubwa kimaisha, inatoa funzo kubwa kwa vijana hasa wasichana ambao wamedhamiria kuhangaika kufikia ndoto zao,” alisema.

Kwa upande wake Tropiano mtayarishaji wa filamu hiyo alisema kuwa hiyo ni filamu ya kwanza kutengenezwa nchini Tanzania kwa kutumia lugha ya Kiswahili kwa sababu alivutiwa na lugha na mazingira ya kijamii na kiutamaduni ya Tanzania.

Alisema lengo lake si kutengeneza filamu pekee, bali ni kuhakikisha wasanii wa filamu wanapata elimu ya kutosha na kutengeneza filamu zenye elimu ili kuwasaidia wengine.