November 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Tuwanusuru watoto wetu kwa kupiga vita vitendo vya uvutaji bangi na dawa za kulevya

Na Suleiman Abeid, TimesMajira Online

BANGI, Kokain, Heroin na Miraa vyote hivi ni miongoni madawa ya kulevya yenye madhara makubwa kwa binadamu na mara nyingi husababisha magonjwa kama vile mapafu na kuharibu mtindio wa ubongo.

Mpaka hivi sasa kuna maelfu ya watu hapa nchini tayari wameishaathiriwa kwa kiasi kikubwa na matumizi ya madawa ya kulevya na sehemu kubwa ya waathirika hawa ni vijana na kundi chipukizi la watoto ambalo ni matarajio ya “nguvu kazi ya Taifa” miaka ijayo.Kwa kawaida dawa za kulevya hutumiwa kwa njia nyingi ikiwemo kuvuta kama sigara na bangi, kula mfano wa mtu anayekula peremende, kumeza kama tembe, kunusia kwa upande wa dawa za kulevya zenye mfano wa ungaunga.

Lakini pia kuna njia ya kutafuna na kumeza maji yake kisha kutupa mabaki hasa kwa watumiaji wa mirungi (miraa), kujidunga sindano na nyingine hutumiwa kwa njia ya kupikia ndani ya chakula au vinywaji.

Matumizi ya dawa za kulevya husababisha mtumiaji alewe na ajisikie huru au kuwa upeo mwingine kuliko kawaida.

Hali hii humfanya mtu awe mtovu wa nidhamu au kufanya mambo ambayo hata mwenyewe atashtuka pindi anapokuwa hajatumia dawa hizo.

Kwa upande wa kiafya, watumiaji wengi wa dawa za kulevya afya zao huathirika, mfano wavutaji wa bangi moyo hudunda kwa haraka haraka isivyo kawaida yake, kinywa kukauka, macho kuwa mekundu, kusahau kwa haraka na kupata uchu mkubwa wa chakula.

Mara nyingi uvutaji wa bangi huathiri mapafu, ini na ubongo na wakati mwingine mvutaji anaweza kuwa mwendawazimu na kwa wanawake wajawazito wanaovuta au kutumia bangi huweza kuharibu mimba bila kukusudia au kujifungua mtoto ambaye hakukomaa vizuri.

Kutokana na madhara mbalimbali yanayosababishwa na utumiaji wa dawa za kulevya, kuna kila sababu jamii kuunganisha nguvu kwa ushirikiano na vyombo vya dola kupambana na watu wanaotumia dawa hizi ambazo matumizi yake katika miaka ya hivi karibuni inadaiwa yameongezeka zaidi hapa nchini.

Makala hii kwa leo itajikita kwenye kutoa wito kwa vyombo vya dola na Jamii kwa ujumla kujikita katika kuwaokoa watoto waishio Kata ya Ndembezi Manispaa ya Shinyanga na maeneo mengine ambao wengi wao wanatajwa kujiingiza kwenye janga la uvutaji wa bangi.

Hali hii imeibuliwa kwenye moja ya mikutano ya wakazi wa Mtaa wa Dome kata ya Ndembezi Manispaa ya Shinyanga ambapo wazazi na walimu wamelalamikia kuibuka kwa wimbi kubwa la watoto wanaovuta bangi.

Ni hali iliyomsikitisha kila mzazi aliyekuwa kwenye mkutano huo kusikia taarifa za vijana wadogo wenye rika la utoto kuvuta bangi tena katika maeneo ambayo ni ya shule za msingi hali inayoweza kuathiri watoto wengi iwapo na wao watateleza na kujifunza uvutaji huo haramu wa bangi.Alex Juma ni mwalimu mkuu wa shule ya msingi Bugoyi “A” na Elisiana Kimasso ambaye pia ni mwalimu mkuu wa Shule ya Msingi Bugoyi “B” wameeleza wazi kukithiri kwa vijana na watoto wadogo wanaovuta bangi katika maeneo ya shule zao.

Walimu hao wanasema hali hiyo isipodhibitiwa haraka kuna hatari ya watoto wengi kuangamia kutokana na uvutaji wa bangi na utumiaji wa madawa mengine ya kulevya hali inayoweza kuwa na athari pia kwa Taifa kutokana na kupoteza nguvu kazi ya Taifa.

“Kituo cha kuvutia bangi ni shule ya msingi Bugoyi “A” na nafikiri na mashahidi wapo, ukifika pale siku za Jumamosi na Jumapili utafikiri pale pana soko, ni vijana wadogo wadogo wanaostahili kuwa “form one” na “form two”, na wengi wao hawa wanatokea pale Mazinge Sekondari,”

“Hawa pale wanavuta bangi mpaka wanaanguka, tumeishafanya jitihada za kila aina za kuwasaidia imekuwa shida, mfano wiki mbili zilizopita tuliweka walinzi eneo hilo, lakini wale vijana waliwatimua wale walinzi mpaka Polisi ikaingilia kati, bahati nzuri wawili walikamatwa, ni vijana wetu,” anaeleza Alex.

Mwalimu huyo anasema kutokana na hali hiyo kuonesha dalili za kukithiri kuna kila sababu ya Serikali kupitia vyombo vyake vya dola ishirikiane na jamii kuwadhibiti watoto hao ili kuweza kuwajengea watoto hao maisha mazuri ya hapo baadae.

Kwa upande wake mwalimu Elisiana anasema hali ya uvutaji wa bangi katika maeneo ya kata ya Ndembezi kwenye shule mbili za msingi za Bugoyi “A” na Bugoyi “B” imekithiri kiasi cha kusikitisha na wanaovuta ni watoto wadogo sana ambapo kuna wakati hawaogopi, wanadiriki kuvuta bangi hizo nyakati za mchana.

“Suala la uvutaji wa bangi linasikitisha, maana watoto wanaovuta ni watoto wadogo sana, pale Bugoyi “A” ndiyo wamefanya kituo chao cha kuvutia, kuna banda la jiko, wameling’oa mabati wanatumia kuvutia humo ndani, wengi ni wahitimu wa darasa la saba mwaka jana, tayari wameingia kwenye dimbwi la uvutaji wa bangi,” anaeleza mwalimu Elisiana.

Hata hivyo mwalimu huyu anawalaumu wazazi na walezi ambao wanashindwa kuwasimamia watoto wao kwa kufuatilia mienendo yao na kwamba ipo hatari watakuja kujutia baada ya watoto kuwa tayari wameathiriwa na uvutaji wa bangi.Mkuu wa Shule ya Sekondari Mazinge iliyopo kata ya Ndembezi Manispaa ya Shinyanga, James Msimba anasema hali ya watoto wadogo kuvuta bangi inachangiwa kwa kiasi kikubwa na wazazi na walezi ambao wameshindwa kufuatilia nyendo za watoto wao wanapotoka nyumbani.

“Mimi niwape tu pole, niwambie watoto wote waliochaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza mwaka huu, pale Mazinge Sekondari, kama wanavuta bangi waache mara moja. Wazazi tumefika mahala tumewaacha watoto wetu wajiongoze wenyewe hii ni hatari, mfano mtoto ananyoa kiduku, na wewe mzazi humkatazi,”

“Miongoni mwa mambo tunayozuia kwa wanafunzi ni kunyoa viduku, sasa wakija shule tukiwafukuza mnasema walimu tuna roho mbaya hatutaki watoto wenu wasome, mtoto kuanzia asubuhi mpaka mchana hujui anakoshinda, lakini akirudi humuulizi, unampa chakula anakula anapotea tena, hapana haya si malezi,” anaeleza James.

Mwenyekiti wa Serikali ya mtaa wa Dome Kata ya Ndembezi, Solomon Nalinga anasema kuanzia sasa watashirikiana na jamii pamoja na Jeshi la Polisi kufanya misako katika maeneo yote yanayodaiwa kuwa ni maficho yanayotumiwa na watoto kuvutia bangi.

Solomon anasema Serikali ya Mtaa wa Dome inapiga marufuku vitendo vya uvutaji wa bangi na madawa ya kulevya na watoto wanaopata maambukizi ya kufundishwa tabia mbaya ya kuvuta bangi waache mara moja na watakaobainika sheria itachukua mkondo wake bila kujali ni mvulana ama msichana.

Mchungaji wa Kanisa la Batheli Churchship lililopo kata ya Ndembezi Manispaa ya Shinyanga, Festo Mgasi anasema matumizi ya madawa ya kulevya, bangi na ukahaba ni matokeo ya wazazi kutowapeleka watoto wao kwenye imani na kwamba madhara ya bangi ni mabaya na mwisho wake ni kuishia Jela.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Shinyanga, ACP Janeth Magomi anakiri kuwepo na malalamiko ya jamii kuhusiana na kuwepo kwa ongezeko la vitendo vya vijana wadogo na watoto kujiingiza kwenye uvutaji wa bangi na matumizi ya madawa ya kulevya.

Kamanda Magomi anasema tayari Jeshi la Polisi limejipanga kuendesha msako wa mtaa hadi mtaa kuwasaka wale wote wanaojihusisha na uvutaji wa bangi na utumiaji wa madawa ya kulevya na mirungi na kwamba wazazi wanapaswa kutoa ushirikiano wa kukamatwa kwa watuhumiwa wote badala ya kuwakingia vifua.

“Hili si jukumu la Jeshi la Polisi peke yake, bali sote tushirikiane ili tuweze kuwabaini watoto wote wanaojihusisha na vitendo hivi vichafu, tunakemea sana bangi, mirungi, madawa ya kulevya na matendo yote ya kiuhalifu, sasa tumejipanga kuhakikisha wote wanakamatwa na kufikishwa mahakamani,” anaeleza Kamanda Magomi.

Baadhi ya wakazi wa mtaa wa Dome, kata ya Ndembezi Manispaa ya Shinyanga wakiwa kwenye mkutano uliohusu kuzungumzia maandalizi ya kuanza kwa muhula mpya wa masomo na changamoto ya uvutaji bangi kwa watoto. (Picha zote na Suleiman Abeid)
Mchungaji wa kanisa la Batheli Churchship katika kata ya Ndembezi Manispaa ya Shinyanga akielezea madhara ya bangi kwa vijana kwenye mkutano wa Serikali ya Mtaa.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Shinyanga, ACP Janeth Magomi.
Bangi na msokoto wa bangi.