March 29, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akikata utepe kuzindua jengo la Mpanda Plaza ambalo ni kitegauchumi cha Shirika la Taifa la Nyumba (NHC), mjini Mpanda, Julai 4, 2020. Wa pili kulia ni Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi, Mhandisi Isack Kamwelwe, kulia ni Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Angelina Mabula, kushoto ni Mkuu wa Mkoa wa Katavi Juma Homela na wapili kushoto ni Mkurugenzi Mkuu wa NHC, Dkt. Maulid Banyani.

Tuongeze bidii tufikie uchumi wa juu- Majaliwa

Na Mwandishi Wetu

WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa amewataka Watazania waendelee kufanya kazi kwa bidii ili nchi iendelee kukua kiuchumi na kufikia uchumi wa juu kwa kuwa tayari imekuwa ya uchumi wa kati.

“Kama ni mkulima lima kwa bidii, mtumishi wa umma fanya kazi kwa bidii, mlio viwandani fanyeni kazi na mamalishe nanyi pikeni sana ili mzunguko wa fedha uweze kuendelea kuwa mkubwa nchini.”

Ametoa kauli hiyo jana alipozindua jengo la ofisi na biashara la Mpanda Plaza lililojengwa na Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) Mpanda kwa gharama ya sh. bilioni 2.8.

Waziri Mkuu amesema Serikali ya Awamu ya Tano ilipoingia madarakani pato la mwananchi kwa mwaka lilikuwa dogo na baada ya miaka mitano limeongezeka na kufikia sh, milioni mbili.

Amesema ongezeko hilo la pato la mwananchi kwa mwaka limeliwezesha Taifa kuingia katika uchumi wa kati kabla ya matarajio yaliyopendekezwa katika Dira ya Taifa ya Maendeleo.

Dira ya Taifa ya Maendeleo ya Tanzania ililenga kuifikisha Tanzania kuwa nchi ya uchumi wa kati kupitia sekta ya viwanda ifikapo mwaka 2025 lakini nchi imewezeka kufikia uchumi wa kati 2020.

Baada ya kuzindua jengo hilo, Waziri Mkuu alitembelea kijiji cha Kasekese kilichoko wilaya ya Tanganyika mkoani Katavi ambapo alizindua msimu wa ununuzi wa zao la pamba kwa mwaka huu.

Waziri Mkuu amesema lengo la Serikali ni kurudisha ushirika ili uweze kuwa na tija kwa wakulima, aliwataka viongozi wa Vyama vya Msingi vya Ushirika (AMCOS) wawasaidie wanachama wao.

Vilevile, Waziri Mkuu amewaagiza Maafisa Kilimo nchini wawaelimishe viongozi wa vyama vya ushirika namna bora ya uendeshaji wa vyama hivyo ili waweze kutekeleza majukumu yao ipasavyo.

Amewahakikishia wananchi hao kwamba Serikali itaendelea kuwasaidia kwa kuhakikisha Maafisa Ugani wanawafikia katika maeneo yao na kuwapa elimu itakayowawezesha kujiongezea tija.