December 26, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Tunduma yatenga bilioni 1 kulipa fidia ujenzi bandari kavu

Na Moses Ng’wat,Timesmajira Online,Tunduma.

MKURUGENZI Mtendaji wa Halmashauriya Mji Tunduma, Philemon Magesa, amesema Halmaahauri hiyo imetenga kiasi cha shilingi Bilioni moja kwa ajili ya kulipa fidia kwa wananchi watakaoachia maeneo yao katika eneo la Katenjele, kata ya Mpemba, ili kupisha ujenzi wa bandari kavu .

Alibainisha hayo wakati akizungumza na waandishi wa habari kutoka vyombo mbalimbali ambao walifanya ziara ya siku tatu kwa lengo la kujionea utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo , ikiwemo ile ya kimkakati .

Magesa amesema katika kutekeleza mradi huo wa kimkakati Halmashauri hiyo imetenga kiasi hicho cha fedha kupitia mapato yake ya ndani kwa kipindi cha mwaka wa fedha 2023/2024.

Akifafanua zaidi,amesema mradi  huo utatekelezwa kwa pamoja kati ya Halmashauri hiyo na Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) .

“Tunduma tunampango wa kujenga bandari kavu na tulichokifanya ni kutafuta eneo na kulipa fidia halafu TPA watakapokuja kwa kuwa wao ni wataalam wa bandari ndio watakaoweka miundombinu,”amefafanua Magesa.

Katika hatua nyingine, Halmashauriya Mji Tunduma ipo kwenye mchakato wa kufanya upanuzi wa maegesho (Truck’s Parking) ya magari makubwa yanayovuka mpaka wa Tanzania na Zambia, kutoka magari 120 hadi malori 300 kwa lengo la kusisimua na  kuiongezea halmashauri hiyo mapato ya ndani.

“Manufaa ya kutanuliwa kwa mradi huu wa maegesho kutoka magari makubwa 120 hadi 300 yanayovuka Mpaka wa Tanzania na Zambia (Truck’s Parking) ukikamilika unatarajia kuiongezea halmashauri hii mapato kutoka mapato ya awali ya milioni 100 kwa mwaka hadi kufikia  Shilingi milioni 300,”amesema.

Aidha, Mkurugenzi Mtendaji Magesa amesema katika utanuzi huo kutakuwa na mradi wa ujenzi wa mgahawa wa chakula (Reustaurant), pamoja na  nyumba za kupumzika madereva na wasaidizi wao  (Rest house).