Na Allan Vicent, TimesMajira Online, Tabora
WENYEVITI wa Chama Cha Mapinduzi (CCM ) wa Wilaya zote za Mkoa wa Tabora wameeleza kuridhishwa na kazi nzuri inayofanywa na Mwenyekiti wa Taifa wa Chama hicho na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt Samia Suluhu Hassan ya kuwaletea maendeleo Watanzania.
Wakiongea katika kilele cha maadhimisho ya miaka 47 ya kuzaliwa kwa CCM hivi karibuni Mkoani hapa wameeleza bayana kuwa Rais Samia ameonesha uwezo mkubwa na uliotukuka wa kuongoza Chama hicho kikubwa chenye heshima ndani na nje ya nchi na amepanua zaidi wigo wa ushirikiano baina yake na vyama tawala vingine.
Aidha wameeleza kuridhishwa na kasi yake ya utendaji, ushupavu na utulivu usio na shaka katika kutoa maamuzi yenye tija kwa chama na taifa kwa ujumla, na kubainisha kuwa wanaCCM na wasio na wanaCCM wana imani kubwa kwake.
Mwenyekiti wa CCM wilaya ya Uyui, Lubasha Makoba amesema kuwa Rais Samia ni zaidi ya mama, Mwenyezi Mungu amemkirimia hekima, busara na uwezo wa kuongoza, ndiyo maana amekuwa kioo na mfano wa kuigwa na viongozi wengine.
‘WanaCCM tunajivunia kuwa na Kiongozi mwadilifu, shupavu, mwenye maono makubwa ya maendeleo, anayejali ustawi wa wananchi na asiyependa makuu, hakika hatuna mashaka naye’, amesema.
Mohamed Katete, Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Tabora Mjini amesema kuwa katika kipindi cha miaka 2 tu tangu aingie madarakani CCM imeimarika zaidi, umoja na mshikamano baina ya viongozi na wanachama umeendelea kudumishwa.
Aidha amesisitiza kuwa Rais Samia amebeba maono ya watangulizi wake wote na ameyasimamia kwa vitendo, ndiyo maana miradi mikubwa yote iliyoanzishwa na watangulizi wake ameendelea kuitekeleza kwa kasi kubwa na kubuni mipya.
Amebainisha kuwa weledi na kasi ya utendaji wa Rais Samia Suluhu Hassan imewezesha ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi ya mwaka 2020-2025 kutekelezwa kwa asilimia 100 katika Mkoa huo na Mikoa yote hapa nchini, KAZI IENDELEE.
Mwenyekiti wa CCM Wilayani Sikonge Anna Chambala amepongeza utaratibu wa chama hicho kuwaamini wanawake na kuwapa nafasi za uongozi ndani ya chama na serikalini, na kubainisha kuwa Rais Samia ni matunda ya malezi mazuri ya chama hicho kwa viongozi wanawake.
‘Akinamama tunaweza, tunaomba chama kiendelee kutuamini na kutupa nafasi za kugombea nafasi mbalimbali katika chaguzi zote ikiwemo uchaguzi wa Serikali za Mitaa na Uchaguzi Mkuu wa mwakani, tuna imani kubwa na Rais Samia’, amesema
Naye Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Kaliua, Seleman Onesmo amempongeza Rais kwa kumwaga mabilioni ya fedha katika Wilaya hiyo kwa ajili ya miradi mbalimbali katika sekta za elimu, afya, barabara, maji na nishati ya umeme vijijini.
Amefafanua kuwa kasi ya utekelezaji miradi ya maendeleo inayoendelea kufanywa na serikali ya awamu ya 6 chini ya uongozi wa Rais Samia haijawahi kutokea, na haya ndiyo yanayowafanya wanaCCM kutembea kifua mbele.
Maganga Sengerema, Mwenyekiti wa CCM Wilayani Nzega amebainisha kuwa Viongozi wa chama na wanaCCM wote wana imani kubwa na Mwenyekiti wao wa Taifa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Amesisitiza kuwa mwaka 2025 hawana mashaka yoyote na ushindi wa Chama Cha Mapinduzi, anaamini Watanzania wote watampa kura za kishindo Rais Samia atakapowania nafasi hiyo tena ili kumalizia miaka yake 5.
Katibu wa Siasa na Uenezi wa CCM Mkoa wa Tabora Idd Moshi amefafanua kuwa Rais Samia amekiheshimisha chama na taifa kwa ujumla ndani na nje ya nchi, hivyo akatoa wito kwa wanaCCM kushikamana ili kupeperusha vizuri bendera yao katika uchaguzi ujao wa Serikali za Mitaa.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Mkoa wa Chama hicho Mzee Hassan Wakasuvi ameeleza wazi kuwa chini ya Uongozi wa Dkt Samia Suluhu Hassan CCM haina mpinzani, na nchi iko katika mikono salama.
Amesisitiza kuwa kila mwanaCCM ana haki ya kutembea kifua mbele kwa sababu ya kazi nzuri inayofanywa na Rais Samia, hivyo akawataka vijana, wanawake na wazee kujitokeza kugombea nafasi katika uchaguzi ujao wa Serikali za Mitaa.
More Stories
RC Chalamila awataka ndugu,Jamaa na marafiki kuwa wavumilivu zoezi la uokoaji likiendelea
Baraza la Madiwani lafukuza watumishi wawili idara ya afya
Wanasheria waombwa kusaidia kusimamia sheria, sera ulinzi wa taarifa