Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online
Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini, Mhandisi Yahya Samamba amesema kuwa Tume ya Madini imeendelea kubuni mikakati mbalimbali ya kuhakikisha inavuka lengo ililopewa la kukusanya kiasi cha shilingi bilioni 650 kwa mwaka wa fedha 2021-2022 ifikapo Juni mwaka huu ikiwa ni pamoja na kuimarisha usimamizi kwenye shughuli za uchimbaji na biashara ya madini na kuongeza vitendea kazi.
Mhandisi Samamba aliyasema hayo leo kwenye ziara ya Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Msafiri Mbibo kwenye Ofisi za Tume ya Madini Makao Makuu jijini Dodoma ambapo alikutana na viongozi wa Tume kwa lengo la kujifunza majukumu ya Tume na kutatua changamoto mbalimbali.
Alisema kuwa katika kuimarisha Sekta ya Madini nchini hadi kufikia tarehe 23 Februari, 2022 jumla.ya magari saba yalipokelewa na kuongeza kuwa magari mengine 33 yapo njiani ikiwa ni kama mkakati wa kuhakikisha Tume inapata vitendea kazi vya kutosha katika kusimamia Sekta ya Madini.
Alieleza mikakati mingine kuwa ni pamoja na kusogeza huduma karibu na wananchi ikiwa ni pamoja na uanzishwaji wa Ofisi za Maafisa Madini Wakazi wa Mikoa 29, Ofisi za Maafisa Migodi Wakazi 13 pamoja na Maabara moja ya kufanya tathmini ya sampuli za madini, kuchambua na kuthaminisha madini yanayozalishwa iliyopo jijini Dar es salaam.
Aliongeza mikakati mingine kuwa ni pamoja na uanzishwaji wa masoko 42 na vituo vidogo vya ununuzi wa madini 70 nchini, kati ya masoko hayo 27 ni ya madini ya dhahabu, masoko 14 ya madini ya vito na soko moja la madini ya bati.
Katika hatua nyingine akielezea hali ya ukusanyaji wa maduhuli kwa Mwaka wa Fedha 2021-2022, Mhandisi Samamba alisema kuwa kuanzia kipindi cha mwezi Julai 2021 hadi Februari, 2022 Tume imefanikiwa kukusanya kiasi cha shilingi bilioni 412.27 sawa na asilimia 63.4 ya lengo la mwaka husika.
Alisema pia mchango wa Sekta ya Madini kwenye Pato la Taifa mwaka 2020 ulikua hadi kufikia asilimia 6.7 kutoka asilimia 4.8 mwaka 2018.
Katika hatua nyingine, Mhandisi Samamba aliishukuru Wizara ya Madini kupitia viongozi wake kwa msaada mkubwa hususan kwenye utatuzi wa changamoto mbalimbali zinazoikabili Tume.
Naye Mwenyekiti wa Tume ya Madini, Profesa Idris Kikula alisisitiza kuwa Tume ya Madini imejipanga kuhakikisha inafikia lengo la ukusanyaji wa maduhuli lililowekwa na kuwataka watumishi wa Tume kuendelea kuchapa kazi kwa ubunifu na uadilifu mkubwa.
Profesa Kikula sambamba na kupongeza uteuzi wa Naibu Katibu Mkuu aliahidi ushirikiano wa Tume katika kuhakikisha Sekta ya Madini inazidi kuwa na mchango mkubwa kwenye ukuaji wa uchumi wa nchi kupitia ukusanyaji wa maduhuli, usimamizi wa karibu kwenye shughuli za uchimbaji na biashara ya madini na kuhakikisha watanzania wananufaika na uwekezaji kwenye shughuli za madini nchini.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti Makamishna wa Tume ya Madini, Profesa Abdulkarim Mruma na Janeth Reuben Lekashingo walisema Tume ipo tayari kushirikiana na Wizara ya Madini kwenye maboresho ya sheria na kanuni lengo likiwa ni kuhakikisha watanzania wanaendelea kunufaika kwenye Sekta ya Madini.
Kamishna wa Tume ya Madini, Janeth Lekashingo aliongeza kuwa katika kuhakikisha watanzania wanakuwa na uelewa mpana wa fursa zilizopo kwenye Sekta ya Madini, Tume imekuwa ikitoa elimu mikoa mbalimbali kuhusu ushirikishwaji wa watanzania kwenye Sekta ya Madini na kusisitiza zaidi kuwa elimu itaendelea kutolewa katika mikoa mingine yote.
Wakati huohuo Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Msafiri Mbibo amewataka watumishi wa Tume ya Madini kuendelea kuchapa kazi kwa ubunifu na uadilifu mkubwa ili mchango wa Sekta ya Madini kwenye Pato la Taifa uendelee kukua kwa haraka.
“Bado ninaamini Tume ya Madini inaweza kufanya vizuri zaidi ya hapa, endeleeni kuchapa kazi kwa ubunifu na uadilifu huku mkiwa wazalendo katika mazingira ya aina yoyote kama wanajeshi,” alisema Mbibo.
Katika hatua nyingine Mbibo alisema kuwa Serikali kupitia Wizara ya Madini itaendelea kutatua changamoto zilizopo kwenye utendaji wa Tume ya Madini lengo likiwa ni kuweka mazingira mazuri ya utendaji kazi na kuvutia wawekezaji zaidi nchini.
More Stories
Watoto wenye uhitaji wapatiwa vifaa vya shule
Wananchi Kisondela waishukuru serikali ujenzi shule ya ufundi ya Amali
RC.Makongoro ataka miradi itekelezwe kwa viwango