November 8, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Tume huru ya uchaguzi na Katiba mpya vinakwenda sambamba

Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online

Katibu Mkuu wa ACT Wazalendo Ndugu Ado Shaibu amebainisha kuwa harakati ya kupigania Tume Huru ya Uchaguzi na Katiba Mpya vinapaswa kwenda pamoja.

Ndugu Ado ameyasema hayo akizungumza na viongozi na Wanachama wa ACT Wazalendo wa Kata ya Zingiziwa (Jimbo la Ukonga) kwenye uzinduzi wa programu ya kusajili wa wanachama kwa mtandao (ACT Kiganjani) kwenye Kata hiyo.

“ACT Wazalendo tunataka Tume Huru ya Uchaguzi kuelekea Katiba Mpya. Harakati za kudai Tume Huru ya Uchaguzi na Katiba Mpya vinapaswa kwenda pamoja. Pamoja na mambo mengine, Tume Huru ya Uchaguzi itahakikisha kuwa kura ya maoni ya Katiba Mpya inafanyika kwa haki na Chaguzi za Serikali ya Mitaa 2024 na Uchaguzi Mkuu 2025 zitafanyika kwa haki na uhuru”-alisema Ndugu Ado Shaibu.

Katika hatua nyingine Katibu Mkuu ameitaka Serikali kushughulikia masuala ya Wamachinga na bodaboda kwa umakini na tahadhari.

“Tunayo Kamati ya Wasemaji wa Kisekta inayoshughulikia kero za Wananchi. Kuhusu hili la Panya road mlilotulalamikia, tumeshalitolea kauli. Mbali ya kuitaka Serikali kuchukua hatua za haraka Kushughulikia suala hilo, lakini katika hatua za muda mrefu, tunapaswa kushughulikia masuala ya Wamachinga , Bodaboda na ajira kwa vijana kwa ujumla kwa umakini mkubwa. Kama Wamachinga watazuiwa kufanya shughuli zao kwenye masoko ya uhakika, bodaboda wakabughudhiwa na vijana wakawa hawana ajira, tatizo la Panya road haliwezi kuisha”-alisisitiza Ndugu Ado.

Awali, Ndugu Ado aliwapongeza Wanachama wa Kata ya Zingiziwa kwa kujitokeza kwa wingi na kujisajili kwenye ACT Kiganjani na kuwataka viongozi na Wanachama kote Nchini kuendelea kujisajili.