Na Mwandishi wetu
KWA sasa Vyama Vya Ushirika nchini vinapita katika kipindi kigumu cha historia kutokana na kuyumba kwa ushirika huo huku baadhi ya watendaji wa vyama hivyo wakijikuta matatani kutokana na tuhuma za kuhusika kwa namna moja ama nyingine na kuanguka na ushirika husika.
Kesi mbalimbali zinaendelea kwenye mahakama nyingi nchini huku baadhi ya watu waliokuwa watendaji wakuu kwenye vyama hivyo wakikabiliwa na tuhuma mbalimbali na wengi wao kufunguliwa kesi za rushwa na kuhujuku uchumi.
Lengo la Nionavyo hii si kujadili msukosuko huo bali ni kuangazia kwa kina chimbuko na baadhi ya mambo ya msingi yaliyochangia kuanguka kwa kiasi kikubwa kwa sekta ya ushirika nchini.
Pamoja na mambo mengi yanayojiri sasa kuna usemi usemao kwamba ni busara zaidi kuangalia wapi ulipojikwaa kuliko pale ulipoangukia.
Vyama vya ushirika vina historia ndefu sana katika uchumi na maendeleo ya taifa letu. Vyama hivi ni matokeo na kielelezo cha harakati za wananchi wa kutoka maeneo mbalimbali nchini kutaka kujiletea maendeleo.
Ushirika ama vyama vya ushirika vilianzishwa katika maeneo mbalimbali ya nchi yetu kutokana na mafungamano ya shughuli za kilimo na uchumi zilizokuwepo kwenye maeneo husika.
Kwa mfano wakazi wa mikoa ya Kaskazini hususani Kilimanjaro walikuwa na chama chao kikuu cha ushirika KNCU kikishughulika zaidi na zao la kahawa, kadhalika wakazi wa mikoa ya kanda ya ziwa Mwanza Nyanza Co-Operative Union) na Shinyanga( SHIRECU) nao walikuwa na vyama hivyo vya Ushirika vikiunganishwa na zao pamba.
Karibu maeneo yote nchini yalikuwa na vyama hivi. Tabora walikuwa na Ushirika wa Tumbaku, Mbinga Songea walikuwa na Ushirika wa Kahawa, Mtwara walikuwa na Ushirika wa Korosho, Tanga Ushirika wa Mkonge, Bukoba Kahawa na kadhalika.
Wakulima katika mikoa na maeneo husika walitegemea sana vyama hivi katika kuuza mazao yao huku wengine wakinufaika kupata pembejeo mbalimbali kuendeleza kilimo chao.
Baada ya nchi yetu kupata uhuru vyama hivi vilikuwa tegemeo na kimbilio kubwa kwa kiuchumi. Ni ukweli ulio dhahiri kwamba vyama hivi vimechangia kwa kiasi kikubwa maendeleo ya taifa letu na kuimarisha huduma mbalimbali za jamii. Katika maeneo mengi yaliyokuwa na ushirika makini hadi leo ukweli unaonekana kwamba ndiyo yaliyopiga hatua kubwa ya kimaendeleo.
Kwa mfano, kutokana na ushirika uliokuwa na nguvu wa mkoa wa Kilimanjaro, maeneo mbalimbali ya mkoa huo yamepiga hatua kubwa ya kimaendeleo. Shule nyingi za msingi, sekondari, vyuo vilijengwa kwenye maeneo hayo, wakazi wa maeneo hayo walipata nafasi ya kuwapeleka watoto wao kupata elimu.
Watu wengi kwenye maeneo hayo wamesoma, huduma zingine za jamii kama afya nazo zimepiga hatua kubwa. Kadhalika katika maeneo mengine yaliyokuwa na ushirika imara kama Bukoba nako watu walifanikiwa kusoma na sekta zingine za kijamii zikapiga hatua.
Kwa ujumla ushirika umekuwa mkombozi wa maisha ya Watanzania kwa kipindi kirefu sasa. Leo hii tunapozungumzia kuanguka kwa vyama vya ushirika kuna mambo mengi tunayopaswa kuyaona ili kuzuia hisia au mtazamo finyu juu ya anguko la vyama vingi vya ushirika.
Ni rahisi kwa sasa kuona kwamba anguko la ushirika limetokana na hujuma na ufisadi wa baadhi ya watendaji wake, pamoja na kwamba kuna asilimia ya ukweli kwenye jambo hili, lakini tukumbuke kwamba anguko kubwa la ushirika ni matokeo ya mtikisiko mkubwa wa kiuchumi duniani uliosababisha kuanguka kwa bei ya mazao mengi ya biashara kwenye soko la dunia.
Historia imeonesha kwamba ushirika ulijengwa kwa kiasi kikubwa na shughuli za kilimo cha mazao ya biashara. Awali bei ya mazao ya biashara kama kahawa na pamba kwenye soko la dunia ilikuwa ya juu.
Hali hii ilifanya wakulima wetu kupata faida kubwa kutokana na bei nzuri za mazao yao, kadhalika vyama vya ushirika vilizidi kustawi na kuimarika. Baada ya anguko kubwa la bei ya mazo kama kawaha, pamba, katani na hata korosho kwenye soko la dunia vyama vya ushirika viliyumba kwa kiasi kikubwa.
Kahawa yetu ilijikuta ikiuzwa kwa bei duni kulingana na ile iliyozalishwa kwenye nchi zingine kama Brazil, kadhalika bei ya mazao kama pamba na mkonge nayo yalijikuta kwenye hali mbaya baada kugundulika kwa teknolojia mbadala na kuwezesha kupatikana nyuzi za kutengenezea nguo. Pia pamba ya kutoka nchi kama India iliuzwa kwa bei ya juu kutoka na ubora wake.
Tukumbuke pia kwamba vyama hivi vya ushirika havikuwa na ruzuku yoyote kutoka Serikali ambayo ingesaidia mapinduzi ya uboreshaji sekta ya kilimo kwa bidhaa walizozalisha na ndo maana mazao yao yaliendelea kukosa ubora uliostahili na kumudu ushindani kwenye soko la dunia.
Hivyo tunapoendelea kuwanyooshea vidole wale tunaodhani ndio chanzo cha kudorora kwa ushirika ni vyema kuangalia historia na mpito mzima wa vyama hvya ushirika nchini. Ni rahisi sana leo kuwataja na kuwanyooshea vidole na hata kuwaadhibu wale tunaodhani wamesababisha anguko hili la ushirika nchini bila kuangalia sababu muhimu zaidi za kuanguka kwa sekta ya ushirika nchini.
Wakati tunanyoosha vidole ni busara pia kuangalia pale ambapo ushirika ulijikwaa na sio ulipoangukia.
More Stories
Elon Musk : Bill Gates atafilisika endapo…
CRDB yazindua matawi Majimoto, Ilula kuwahudumia wananchi
Lina PG Tour yafufua gofu Moshi