Na Esther Macha,TimesmajiraOnline,Mbeya
MTOTO mwenye ulemavu wa miguu Doreen Myuki (12)Mwanafunzi wa darasa la Saba Shule ya Msingi Mwasote kata ya Itezi Jijini Mbeya ameshindwa kujizuia kwa kumwaga machozi kwa kueleza machungu aliyopotia kipindi chote cha kusaka elimu kutokana na ulemavu aliokuwa nao.
Akizungumzia leo,Machi 11,2024 shuleni hapo huku akitokwa na machozi wakati akikabidhiwa kiti Mwendo kitakachomsaidia katika mahitaji yake na elimu na Taasisi ya Tulia Trust ,mtoto Doreen amesema kuwa kutokana na hali yake amekuwa akipata changamoto mbalimbali ikiwemo kwenda shule na wakati wa kwenda chooni kujisaidia.
“Ilikuwa shida kubwa kwangu kufika shule kutokana na hali yangu ya ulemavu nilionao nashukuru sana kwa msaada huu wa baiskeli itanisaidia wakati wa kwenda shule na mahitaji mengine”amesema.
Bibi anayemlea mtoto huyo ,Metelina Mwasote (50)mkazi wa Gombe amesema kuwa toka alipoanza darasa la kwanza mjukuu wake amekuwa na changamoto nyingi kutokana na ulemavu alionao wa miguu kwani asubuhi wakati wa kwenda shule hulazimika kumbeba mgongoni mpaka shule na wakati wa kurudi hupata msaada wa kusaidiwa na watoto wenzie hivyo hivyo hata wakati wa kwenda kujisaidia chooni hulazimika kumsaidia.
“Kutokana na tatizo hili la ulemavu la mjukuu wangu tumefanya jitihada za kumpeleka hospitali mbalimbali ikiwemo hospitali Rufaa kanda ya Mbeya kwa ajili ya matibabu kitengo cha mazoezi ya viungo kwa miaka (8) lakini bado ilishindikana hivyo mwaka 2022 tulichukua jukumu la kumpeleka Jijini Dar es salaam kwa ajili ya upasuaji wa mfupa kwenye kisigino kwa kudhani kuwa labda anaweza kutembea”amesema Bibi wa mtoto huyo.
Aidha Mwasote aliomba Serikali impangie shule ya jirani anapomaliza darasa la saba na kuingia kidato cha kwanza ili awe karibu na nyumbani kwani hivi Sasa yupo darasa la Saba.
Kwa upande wake Ofisa habari na mawasiliano wa Taasisi ya Tulia Trust, Joshua Mwakanolo amesema kuwa katika zoezi hilo wametoa kiti Mwendo kimoja lakini wakiwa wanaendelea na zoezi hilo alipatikana mtoto Doreen Myuki mwenye ulemavu wa miguu ambaye nae alipatiwa kiti Mwendo na daftari 12.
Aidha Mwakanolo amesema zoezi hilo litaendelea kwa kata zote 36 za Jiji la Mbeya pia amesema kutokana na ulemavu wa mtoto Doreen mama mzazi wa mtoto huyo atakuwa miongoni mwa wanufaika wa kupewa msaada ambao hutolewa bure na Spika wa Bunge na Mbunge wa Jimbo la Mbeya Mbeya na Rais wa IPU Dkt.Tulia Ackson.
Hata hivyo amesema kila mwaka Dkt.Tulia hutoa fedha kwa wanawake kwa ajili ya kuwawesha kiuchumi .
More Stories
TAG yampongeza Rais Samia
CCM Tabora yamfariji mjane wa kada anayedaiwa kujiua
FDH yaanza kutekeleza mradi wa kuwajengea uwezo wanawake wenye ulemavu