Na Mwandishi Wetu, Timesmajira Online, Mbeya
TAASISI ya Tulia Trust imesema Tamasha la Ngoma za Asili mwaka 2026 linakuja kwa sura ya kipekee, likilenga kulinda utambulisho, kuhifadhi historia na kuenzi urithi wa kitamaduni wa Tanzania.
Akizungumza na waandishi wa habari Agosti 21, 2026, Afisa Mawasiliano na Uhusiano Taasisi ya Tulia Trust, Joshua Mwakanolo, amesema tamasha hilo litafanyika kuanzia Septemba 24 hadi 26, mwaka huu likiwa ni msimu wa 10 tangu kuanzishwa kwake mwaka 2016.
Mwakanolo amesema tamasha hilo linatarajiwa kufanyika katika uwanja wa Shule ya Msingi Gombe, Jimbo la Uyole, chini ya kaulimbiu “Tuuenzi Utamaduni Wetu”, ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya miaka 10 ya Tulia Trust.
“Tamasha hili tunatarajia lifanyike katika uwanja wa Shule ya Msingi Gombe katika Jimbo la Uyole, likiwa na kaulimbiu ya ‘Tuuenzi Utamaduni Wetu’. Pia ni sehemu ya maadhimisho ya muongo mmoja tangu kuanzishwa kwa taasisi mwaka 2016,” amesema Mwakanolo.
Amefafanua kuwa tamasha hilo halilengi kuwa tukio la burudani pekee, bali litakuwa jukwaa la kuwakutanisha wananchi na wadau wa utamaduni, kuibua vipaji, kuhamasisha vijana kushiriki katika sanaa za asili na kuhakikisha maarifa, mila na desturi za Kitanzania vinaendelezwa kutoka kizazi kimoja hadi kingine.
“Lakini pia kupitia ngoma, mavazi, ala za muziki na sanaa mbalimbali za jadi, washiriki na watazamaji watapata nafasi ya kushuhudia uzuri na utofauti wa utamaduni wa Tanzania,” amesema.
Aidha, Mwakanolo amesema tamasha hilo litakuwa na eneo maalum litakalojulikana kama MKEKA WA BIBI, ambalo litatoa fursa kwa wazee kuonyesha ujuzi na ubunifu wao katika ususi wa mikeka.
Amesema eneo hilo pia litawawezesha wazee kuuza mikeka watakayotengeneza, hivyo kupata kipato na kuchangia katika kuboresha maisha yao.
Kwa upande wake, Chifu Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Chifu Rocket Mwashinga, ametoa shukrani kwa Mkurugenzi wa Tulia Trust, ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Uyole na Rais wa Umoja wa Mabunge Duniani (IPU), Dkt. Tulia Ackson, kwa kuanzisha tamasha hilo linalolenga kuendeleza na kuhifadhi ngoma za asili.
Naye Mwenyekiti wa Madereva Bajaji Jimbo la Uyole, Joseph Jackson, amemshukuru Dkt. Tulia Ackson kwa kuleta tamasha hilo akisema litatoa fursa mbalimbali za kiuchumi, hususan kwa sekta ya usafirishaji.
Jackson amesema madereva bajaji wako tayari kushirikiana na waandaaji kuhakikisha wananchi watakaohudhuria tamasha hilo wanapata huduma ya usafiri wa uhakika wakati wa siku zote za tamasha.
Amesema ujio wa tamasha hilo unatarajiwa kuongeza shughuli za kiuchumi katika eneo la Uyole, huku akiwahimiza wadau mbalimbali kutumia fursa zitakazotokana na tamasha hilo.

More Stories
Rais Samia kuandika historia mpya leo uzinduzi wa JNHPP
Ubunifu wawekwa mbele katika mpango mpya wa Taifa
Ubunifu mwanafunzi UDOM kusaidia Walimu kazini