Na Iddy Lugendo, Timesmajira Online DSM
CHAMA cha Wafanyakazi wa Viwanda, Biashara, Taasisi za Fedha, Huduma na Ushauri (TUICO) wametoa msaada wa vitu mbalimbali katika gereza la wanawake Segerea ikiwa ni sehemu ya kuelekea maadhimisho ya siku ya wanawake duniani ambayo huadhimishwa kila mwaka ifikapo machi 8.
Akizungumza baada ya kutoa misaada hiyo leo Jumamosi, Machi 04 mwaka 2023 jijini Dar es Salaam, Mwenyekiti Kamati ya Wanawake TUICO Temeke na mjumbe wa baraza kuu la TUICO Magdalena Lucas Samkumbi amesema wameamua kuungana na wanawake wengine duniani kusherehekea nafasi ya mwanamke katika jamii ikiwa ni Mwezi wenye Siku ya Wanawake Duniani.
“Tumekuja hapa gereza la wanawake Segerea kwa ajili ya kutoa misaada kutokana na kuelekea siku ya Wanawake Duniani. Tumekuja kuleta vifaa kwa ajili ya wafungwa, Tumeona hii siku tuitumie kwa namna hiyo ikiwa ni moja ya njia za kukitangaza Chama,”
“Wafanyakazi tupo na tunawatetea na katika huduma za kijamii tupo. Huu ni mwendelezo na tunategemea wakati mwingine tutakuwa sehemu nyingine. Kila mwaka tunakuwa na tukio maalumu,” amesema Samkumbi
Kwa upande wake Kaimu Mkuu wa Gereza la Segerea, Abu Seke amesema kuwa watahakikisha misaada hiyo inawafikia wanufaika waliokusudiwa huku akiwaasa wadau na taasisi mbalimbali nchini kuunga mkono juhudi hizo katika kuwakumbuka wafungwa waliopo magerezani.
More Stories
Maghorofa Kariakoo mikononi mwa Tume
ITA chatakiwa kutoa mafunzo ya viwango vya juu na kasi ya maendeleo ya Kisayansi
Wagombea CHADEMA wakipewa ridhaa,watakuwa wawazi