Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online
Wafanyakazi wa Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA) wametakiwa kutumia mikutano ya vyama vya wafanyakazi kujadili na kuja na mapendekezo yatakayoleta mabadiliko chanya katika taasisi.
Hayo yameelezwa leo Aprili 29, 2023 na Mkurugenzi wa Udhibiti Uchumi wa TCAA Bw. Daniel Malanga alipomuwakilisha Mkurugenzi Mkuu wa TCAA Bw. Hamza Johari wakati wa kufunguamkutano mkuu wa mwaka wa cha Chama cha Wafanyakazi wa Serikali kuu na Afya (TUGHE) Tawi la Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA).
“Tunatambua umuhimu wa chama cha Wafanyakazi katika kuchagiza mafanikio ya mamlaka, rasilimali watu ni muhimu kwa maendeleo ya taasisi kwahiyo TUGHE ina wajibu wa kuhakikisha inazungumza vyema na watumishi pamoja na kuwa na semina za mara kwa mara kwaajili ya kuwajengea uwezo chanya wanachama wake ,”amesema Bw. Malanga
Kiongozi huyo amepongeza uongozi na wanachama wa TUGHE kwa kuandaa vyema mkutano huu wa mwaka jambo linalowapa fursa ya kujadili kwa mapana taarifa mbalimbali za kiutendaji ndani ya chama na hatimaye kuandaa mapendekezo yatakayoleta tija ndani ya taasisi.
Pia amesema vikao hivi ni muhimu kwa kuwa vinaleta mshikamano na umoja kwa wafanyakazi ikiwemo kujadili changamoto wanazozipata wafanyakazi na kuzitafutia ufumbuzi kwani wao ni kama daraja kati ya utawala na wafanyakazi.
Mbali na hayo, Bw. Malanga aliwataka watumishi wa TCAA kuwasilisha changamoto wanazokumbana nazo kwa mamlaka husika badala ya kusubiri vikao vya TUGHE kueleza changamoto wanazopitia.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa TUGHE Tawi la TCAA Jackline Ngoda, amesema lengo la kufanya kikao hicho ni kuwakumbusha watumishi wajibu wao katika utendaji ikiwa na kauli mbiu isemayo kuchaguza wafanyakazi wa usafiri wa Anga kufanya kazi kwa ufanisi na juhudi kwani hilo ndilo lengo la kuweza kuipaisha mamlaka hiyo.
Akitoa mada katika mkutano huo, Katibu wa TUGHE mkoa wa Morogoro Bw. Anthelmus Tarimo ametoa wito kwa wanachama wa TUGHE tawi la TCAA kuwa mfano wa kuigwa katika eneo la kazi kwa kufanya kazi kwa bidii na kuzingatia miongozo na taratibu za kazi.
“Inapendeza sana kuona wewe mwanachama wa TUGHE unakuwa ndio kioo kinachoonesha taswira njema pale pale kwenye eneo la kazi, ifike mahali watumishi wenzako watamani kuwa wanachama wa TUGHE kwa vile wanavyosadifu mienendo yako” alisema Bw. Tarimo.
More Stories
Airtel yatoa zawadi kwa wateja wake
Mpango ashiriki mazishi ya Mama yake Serukamba
TRA kuongeza idadi ya waendesha uchumi walioidhinishwa