January 22, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Tuchangie damu kuokoa maisha ya wanaoihitaji

Judith Ferdinand, TimesMajira Online, Mwanza

Wananchi wa mikoa ya kanda ya ziwa wameombwa kujitokeza kuchangia damu ili kupata damu ya kutosha kwa ajili ya kusaidia wagonjwa mbalimbali wanaohitaji damu na kuokoa maisha yao.

Wito huo umetolewa na Meneja wa Mpango wa taifa wa damu salama kituo cha Kanda ya Ziwa, Dkt.Iragi Ngerageza wakati akizungumza na Timesmajira kwa njia ya simu, ikiwa namna moja wapo ya kuadhimisha siku 14 za siku ya wachangia damu duniani ambayo kilele chake ni Juni 14, mwaka huku ikibeba kauli mbiu ya “Damu salama inaokoa maisha, changia damu okoa maisha”.

Dkt. Ngerageza, ameomba wananchi wote kujitokeza kuchangia damu katika Kituo cha Damu Salama Kanda ya Ziwa, pamoja na vituo vingine vidogo vya kukusanya damu vilivyopo katika halmashauri na mkoa ili waweze kupata damu ya kutosha kwa ajili ya wahitaji.

“Jukumu la kuhakikisha upatikanaji wa damu ya kutosha ni letu sote wanajamii, tujitokeze kuchangia damu ili tuokoe maisha kwani damu salama inaokoa maisha, changia damu okoa maisha,” amesema Dkt. Ngerageza.

Amesema takwimu za ukusanyaji damu kwa mwaka 2019/2020 kitaifa ambapo lengo la Huduma ya Kitaifa ya Kuhamisha Damu (NBTS) ni asilimia 70 ya lengo la Shirika la Afya Duniani(WHO) ambayo ni units 375,000 huku utekelezaji ukiwa ni units 322,693.

Ameongeza kuwa asilimia 86 ya lengo la WHO ni asilimia 1 ya idadi ya  watu ambayo ni units 550,000 huku utendaji ukiwa ni units 322,693 sawa na asilimia 59. Ambapo Kanda ya Ziwa lengo la NBTS ni units 87,660 huku utendaji ukiwa ni units 74,698 sawa na asilimia 92 wakati lengo la WHO ni units 134,904 huku utendaji ukiwa units 74,698 sawa na asilimia 55 na kwa upande wa Kituo cha Kanda ya Ziwa lengo lilikuwa ni kukusanya damu units 26,957 lakini walifanikiwa kupata units 8,346  sawa na asilimia 31.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Taasisi ya Mashujaa wa Sikoseli Tanzania (TASIWA), Pascazia Mazeze, anasema wanahusika na utoaji elimu na kuelewesha jamii kuhusu ugonjwa wa sikoseli ambapo katika siku hizi za maadhimisho ya uchangiaji damu wanatoa elimu ya umuhimu wa damu kwa wagonjwa wa sikoseli kwa kulinganisha na ugonjwa huo kwani ni kundi moja wapo linalo hitaji damu sana hivyo wanahamasisha jamii iweze kuchangia damu ili kusaidia jamii nzima ya watu wenye ugonjwa wa sikoseli.

Aidha Mwenyekiti wa Taasisi ya Mashujaa wa Sikoseli Tanzania Josepha Chokara, wanaomba wananchi wajitokeze kwa wingi kuchangia damu ili waweze kusaidia kuokoa maisha ya mashujaa wao wa sikoseli kwani wanahitaji sana damu pamoja na watu wengine.