December 28, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

????????????????????????????????????

TSC yaainisha makosa sugu ya walimu nchini

Na Veronica Simba,TimesMajira Online,Dodoma
 
KAIMU Katibu wa Tume ya Utumishi wa Walimu Tanzania (TSC), Moses Chitama ametaja makosa sugu yanayofanywa na baadhi ya walimu nchini kuwa ni utoro, ulevi pamoja na kujihusisha kimapenzi na wanafunzi.

Kaimu Katibu wa Tume ya Utumishi wa Walimu (TSC), Moses Chitama,
akiwasilisha mada kuhusu maadili katika mkutano wa pili wa Umoja wa
Walimu Wakuu wa Shule za Msingi Tanzania Bara (hawapo pichani),
uliofanyika jijini Dodoma

Ameyasema hayo jana mwaka huu,wakati akiwasilisha mada kuhusu maadili, katika Mkutano wa Pili wa Umoja wa Walimu Wakuu wa Shule za Msingi Tanzania Bara, uliofanyika jijini Dodoma.

Chitama amefafanua kuwa,TSC ikiwa ni Mamlaka ya Nidhamu kwa Walimu nchini, imebaini kuwa makosa hayo matatu ndiyo yanaongoza kuripotiwa kwa sasa, miongoni mwa makosa kadhaa yanayohusiana na utovu wa nidhamu katika kada husika.

Mkurugenzi kutoka Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa TAMISEMI), anayesimamia Elimu ya Awali na Msingi, Susan Nussu,akisisitiza kuhusu maadili ya walimu, wakati wa mkutano wa pili wa Umoja wa Walimu Wakuu wa Shule za Msingi Tanzania Bara (hawapo pichani), uliofanyika jijini Dodoma,

Ameendelea kueleza zaidi kuwa, kwa kulitambua hilo, Tume imekuwa ikitumia mbinu mbalimbali katika kuhakikisha suala hilo linatokomezwa ikiwemo kutoa elimu kwa wahusika na kuchukua hatua kali za kinidhamu kwa wanaothibitika kutenda makosa hayo.

Aidha, Kaimu Katibu Chitama ametumia jukwaa hilo kukemea vikali walimu wenye tabia hiyo na kuwataka kuacha mara moja huku akisisitiza kuwa Serikali kupitia Tume husika, haitawavumilia.

Amesema kuwa walimu ndiyo chanzo kikuu cha maendeleo ya nchi kwani ndiyo wamepewa dhamana ya kuwalea kiakili na kimwili watoto, ambao wanategemewa na Taifa kuja kuwa viongozi na wataalamu katika nyanja mbalimbali, hivyo wanapaswa kutimiza wajibu wao ipasavyo.

“Ninyi walimu msiposimamia maadili ya taaluma yenu pamoja na maadili ya watoto mnaowafundisha, tutakuwa na Taifa bovu, lililokosa mwelekeo na lenye mmomonyoko wa maadili.”

Sehemu ya Wajumbe wa Mkutano wa Pili wa Umoja wa Walimu Wakuu wa Shule za Msingi Tanzania Bara (hawapo pichani), wakifuatilia mada mbalimbali zilizokuwa zikiwasilishwa wakati wa mkutano huo.

Akitoa takwimu, Chitama amebainisha kuwa, katika kipindi cha miaka mitano (2016 – 2020), jumla ya walimu 9,819 walifunguliwa mashauri na waajiri wao, ambapo 5,441 kati yao walifukuzwa kazi.

Aidha,ameeleza kuwa, katika kipindi hicho, walimu 1,803 walipewa maonyo na makaripio, 520 walipunguziwa mishahara, 244 walisimamishiwa nyongeza ya mishahara na 403 waliteremshwa vyeo.