Na Veronica Simba-TSC
WATENDAJI wa Tume ya Utumishi wa Walimu (TSC) wamehamasishwa kubuni mbinu zitakazowafanya walimu waache kukiuka maadili ya kazi yao, suala ambalo husababisha wengi kupata adhabu mbalimbali ikiwemo kufukuzwa kazi.
Wito huo umetolewa leo na Afisa Elimu wa Mkoa wa Mwanza, Mwalimu Martin Nkwabi wakati akifungua mafunzo kwa kamati za wilaya za TSC zilizoko Kanda ya Ziwa kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa huo.
“TSC hakipaswi kuwa chombo cha kusubiri mashauri. Lazima muwe na utaratibu wa kuhakikisha walimu hawafanyi makosa yanayosababisha kuondolewa kazini,”amesisitiza.
Kuhusu suala la maadili, Mwalimu Nkwabi ameishauri TSC kuzifikia shule zote kwa lengo la kuhakikisha walimu wanazingatia maadili ya kazi yao kwa kuwalea vema wanafunzi ili wawe raia wema.
Amesema kuwa, ni wajibu wa walimu kusimamia maadili na makuzi ya wanafunzi hivyo TSC ikiwa ni Mamlaka yao ya Nidhamu, inapaswa kuhakikisha wajibu huo unatekelezwa kikamilifu.
Afisa Elimu huyo amekemea tabia ya baadhi ya walimu kuwachukulia wanafunzi kama wateja wao hivyo hawashughuliki na malezi yao wakiamini kuwa mteja hakemewi kwani ndiye anawawezesha kupata mshahara.
“Siku walimu wote wakiwaangalia wanafunzi kama watoto wao wa kuzaa, tunaweza kuondokana na tatizo hili,”amesema.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa TSC, Prof. Willy Komba akitoa neno la kumkaribisha mgeni rasmi, amewaasa watendaji wa tume hiyo kuhakikisha wanatenda haki kwa walimu kwa kuzingatia sheria na taratibu zilizopo ili nao waweze kuwalea wanafunzi vema.
“Walimu bora ndiyo watazaa elimu bora. Walimu bora lazima wahudumiwe vizuri. Bila kuwahudumia walimu vizuri watakuwa na manung’uniko na kero na hawatafanya kazi vizuri. Ndiyo maana Serikali ikatuamini sisi tuwahudumie,” amesisitiza Prof. Komba.
Akitoa neno la utangulizi, Katibu wa TSC, Mwalimu Paulina Nkwama alitoa shukrani kwa Mungu na Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan kwa kumwamini na kumteua kushika wadhifa huo, hivyo aliahidi kuitumikia nafasi hiyo kwa uadilifu na weledi ili asimwangushe Rais.
Akizungumzia mafunzo husika, Mwalimu Nkwama alieleza kuwa ni zoezi endelevu ambalo litaendelea katika Kanda zote saba zinazohudumiwa na TSC kwa lengo la kuwajengea uwezo Wajumbe wa Kamati husika waweze kutimiza majukumu yao kwa ufanisi.
“Ni matarajio yetu kuwa baada ya mafunzo haya, Wajumbe wa Kamati husika wataenda kutatua kero na changamoto mbalimbali zinazowakabili walimu, ili kuwawezesha kutimiza majukumu yao ya kuwalea wanafunzi ipasavyo kimwili na kiroho,”alisema.
Mafunzo hayo ya siku mbili yameshirikisha Wajumbe kutoka Wilaya zote za Mikoa ya Kanda ya Ziwa, ambazo ni Mara, Geita, Simiyu, Shinyanga na Mwanza.
More Stories
Watoto wenye uhitaji wapatiwa vifaa vya shule
Wananchi Kisondela waishukuru serikali ujenzi shule ya ufundi ya Amali
RC.Makongoro ataka miradi itekelezwe kwa viwango