January 11, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

TSB yahamasisha kilimo cha mkonge

Na Yusuph Mussa, Timesmajira Online, Mbeya

BODI ya Mkonge Tanzania (TSB) inawahamasisha wananchi wa mikoa inayostawi zao la mkonge, kulima zao hilo, kwani lina faida nyingi ikiwemo kuzalisha bidhaa mbalimbali kama singa baada ya kuchakatwa hivyo kuinua uchumi wa taifa.

Ofisa Masoko wa TSB David Maghali (kulia) akionesha baadhi ya bidhaa zinazotokana na mkonge ikiwemo kamba na brashi (singa) katika banda la TSB kwenye maonesho ya Kimataifa ya Kilimo (Nane Nane) yaliyofanyika kwenye Viwanja vya John Mwakangale jijini Mbeya.

Hayo yamesemwa Agosti 8, 2023 na wataalamu wa TSB kwa nyakati tofauti wakiwa kwenye banda la TSB katika maonesho ya Kimataifa ya Kilimo (Nane Nane) yanayofanyika kwenye Viwanja vya John Mwakangale jijini Mbeya.

Ofisa Masoko wa TSB David Maghali amesema kilimo cha mkonge kimekuwa na tija baada ya wananchi wazawa kukifanya zao la biashara, tofauti na miaka ya nyuma, ambapo mkonge ulikuwa unalimwa na wawekezaji kutoka nje ya nchi.

“Kwa sasa kilimo cha mkonge ni zao kuu la biashara kwa Mkoa wa Tanga baada ya wananchi wengi kulima kama zao kuu la biashara ambalo limewasaidia kupata kipato na kubadilisha kabisa maisha yao.

“Zamani mkonge wakati unalimwa, ilikuwa kwa ajili ya kuzalisha singa (nyuzi), hivyo asilimia 98 ya jani la katani lilikuwa linatupwa, lakini sasa kila kitu kilichopo kwenye jani hilo lina faida,sasa hivi mkonge unatengenezasinga, magunia, kamba, pombe kali, mazulia, vikapu, vibegi, vifaa vya kutengeneza magari, sukari ya mkonge na mbolea,”amesema Maghali.

Ofisa Masoko wa TSB David Maghali (katikati) akimuonesha mteja baadhi ya bidhaa zinazotokana na mkonge, ambapo kuna kiti cha uvivu, meza, mikoba ya wanawake na wanaume na busati kwenye banda la TSB lililokuwa katika Maonesho ya Kimataifa ya Kilimo (Nane Nane) yaliyofanyika kwenye Viwanja vya John Mwakangale jijini Mbeya.

Maghali amesema soko la mkonge lipo ndani na nje ya nchi kama Bodi ya zao hilo wanawaunganisha wakulima na wanunuzi huku wakulima wadogo waliopo kwenye mfumo wa SISO, wanauza mkonge wao kwa mnada, hivyo kuwa na uhakika wa soko.

“Tumekuja kwenye maoneaho ya Nane Nane kufanya uhamasishaji na kutangaza fursa zilizopo kwenye kilimo cha mkonge, tunaunganisha wakulima na wanunuzi wale wakulima waliopo kwenye Mfumo wa SISO” amesema Maghali.

Naye Ofisa Kilimo wa TSB Emmanuel Lutego amesema Serikali inaendelea kutoa hamasa kwa mikoa ambayo kilimo cha mkonge kinastawi na nia yake ni kuona zao hilo liinasambaa nchi nzima na kuwanufaisha wananchi wengi.

“Tumekuja kuwaelimisha wananchi kulima zao la mkonge, na baadhi ya mikoa zao hilo linastawi ikiwa ni pamoja na Tanga, Morogoro, Kilimanjaro, Pwani, Simiyu, Singida, Shinyanga, Mara na Manyara ambapo wakulima wa mkonge watapatiwa mbegu bure,” amesema Lutego.

Baadhi ya bidhaa zinazotokana na mkonge, ambapo kuna kiti cha uvivu, meza, mikoba ya wanawake na wanaume, na busati kwenye banda la TSB lililokuwa katika maonesho ya Kimataifa ya Kilimo (Nane Nane) yaliyofanyika kwenye Viwanja vya John Mwakangale jijini Mbeya

Lutego amesema Serikali inaendelea kuboresha miundombinu ya mkonge kwa kuanzia na ukarabati wa korona iliyopo Shamba la Mkonge Kibaranga lililopo Wilaya ya Muheza, na itaweka korona mpya Wilaya ya Handeni.