Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online
Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), imezindua rasmi Kampeni ya Tuwajibike inayolenga kuwahamasisha walipakodi na wananchi kwa ujumla kuhusu wajibu wao wa kutoa na kudai risiti sahihi za EFD.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam wakati wa uzinduzi wa kampeni hiyo, Mkurugenzi wa Huduma na Elimu kwa Mlipakodi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Richard Kayombo amesema kampeni hiyo inayoanza mwezi huu Mei, 2023 ni endelevu.
“Kampeni hii ya Tuwajibike ni endelevu na inaanza rasmi mwezi huu wa tano ikiwa na malengo yafuatayo; kuwakumbusha na kuwasisitiza wauzaji wa bidhaa na watoa huduma nchi nzima kuwajibika kwa kutoa risiti halali ya EFD kila wanapouza bidhaa au kutoa huduma mbalimbali, kuwakumbusha na kuwahamasisha wanunuzi wa bidhaa na huduma kote nchini kuwajibika kudai risiti halali ya EFD pamoja na kuzikagua ili kujiridhisha kuwa inakidhi vigezo vyote muhimu, amesema Bw. Kayombo.
Malengo mengine ya Kampeni Kwa mujibu wa Kayombo ni kufuatilia utoaji wa risiti halali za EFD nchi nzima pamoja na kuchukua hatua kwa wauzaji wasiofuata sheria katika utoaji wa risiti halali za EFD ikiwemo kutokutoa risiti ya EFD na kutoa risiti yenye kiwango cha chini kulingana na thamani halisi ya bidhaa au huduma, wafanyabiashara tofauti kutumia risiti moja wakati wa kusafirisha mizigo pamoja na kuuza risiti pasipokuwa na manunuzi yoyote.
Akizungumzia suala la risiti halali ya EFD, Kayombo amesema kuwa risiti halali inatakiwa kukidhi vigezo vikuu vinne ambavyo ni Jina la biashara, tarehe halisi ya mauzo, kiwango halisi cha pesa kilichotolewa kwa bidhaa au huduma na jina au TIN ya mnunuzi au vyote kwa pamoja.
“Ukiachilia mbali vigezo hivyo vya risiti halali, napenda kuwakumbusha kuwa, adhabu ya mfanyabiashara atakaebainika kutokutoa risiti halali ya EFD au kufanya udanganyifu atatozwa faini ya shilling 3,000,000 mpaka shilling 4,500,000 au kifungo kisichozidi miaka mitatu au vyote kwa pamoja,” alifafanua Bw. Kayombo na kuongeza kuwa, kwa upande wa mnunuzi atakayebainika kufanya manunuzi bila ya kudai risiti halali ya EFD atatozwa faini ya shillingi 30,000 mpaka 1,500,000.
“Faini hizo zipo kisheria na kazi yetu ni kusimamia sheria hivyo natoa wito kwa wafanyabishara wote kuwajibika kwa kutoa risiti halali za EFD bila ya kushurutishwa na wanunuzi nao wanatakiwa kudai risiti halali za EFD kwa kila manunuzi watakayoyafanya ili kuepuka usumbufu usio wa lazima,” alisema Mkurugenzi Richard Kayombo.
More Stories
FDH yaanza kutekeleza mradi wa kuwajengea uwezo wanawake wenye ulemavu
Airtel yatoa zawadi kwa wateja wake
Mpango ashiriki mazishi ya Mama yake Serukamba