Na Mwandishi wetu, Timesmajira
Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA),Yusuph Mwenda ameonya uwepo wa wafanyabiasha wasiokuwa waaminifu wanaotengeneza pombe bandia na kuweka Stika za TRA kwa kughushi, kuacha mara moja kwani kufanya hivyo ni kosa la kisheria.
Akiwa mkoani Manyara katika muendelezo wa ziara yake ya kuwashukuru na kuwasikiliza Walipakodi mbalimbali ,Kamishna Mkuu Mwenda alisema kughushi Stika za TRA ni makosa kisheria hivyo watahakikisha wanawasaka wafanyabiasha hao wanaozalisha vinywaji changamshi bandia.
Amesema uzalishaji huo unaenda sambamba na matumizi ya Stika Bandia ili kuwaaminisha watumiaji.”Licha ya kukwepa kulipa kodi wazalishaji hawa wa Pombe bandia wanahatarisha usalama wa afya za watanzania kutokana na vinywaji vyao kutokuwa na viwango,”amesema.
Kabla ya mkutano huo na wafanyabiasha,Kamishna Mwenda alitembelea Kiwanda cha MAT cha Mkoani Manyara kinachozalisha Pombe Kali maarufu kama Vinywaji changamshi na kumpongeza mmiliki wa kiwanda hicho, David Mulokozi kwa kuwa Mlipakodi mzuri anayezingatia sheria.
Amesema wazalishaji wasiokuwa waaminifu wanaokiuka sheria za nchi wamekuwa wakiwanyonya wenzao kwa kushusha bei na kuwafanya washindwe kushindana sokoni.
Katika hatua nyingine Kamishna Mkuu Mwenda alisema miongoni mwa majukumu ya TRA ni kukuza biashara nchini kwa kuondoa vikwazo vinavyowakabili wafanyabiasha ili waweze kuwa na mazingira rafiki ya kufanyia kazi zao na kulipa kodi kwa hiari.
Amesema TRA imetumia msimu wa kuwashukuru Walipakodi kusikiliza changamoto zinaxowakabili na kuzipatia ufumbuzi.
Katika ziara hiyo ya Kamishna Mkuu, Mwenda alimkabidhi zawadi kwa baadhi ya walipakodi akieemo Mkurugenzi wa Kampuni ya Twiga General Traders, Richard Ngalewa ambaye amejipambanua kama mlipakodi anayetoa elimu ya mlipakodi kwa wengine.
“Huyu ni Mlipakodi wa kipekee aliyejipambanua kama mtoa elimu ya Kodi kwa Walipakodi wengine mkoani Manyara hususan hapa kwenye mji wa Babati hivyo kama Mamlaka tunawajibika kumtambua na kumshukuru kwa kuwa balozi wetu mzuri” Alisema Mwenda.
Akizungumza baada ya kupatiwa zawadi Richard Ngalewa alisema anaendelea kutoa elimu kwa walipakodi wengine ili kuongeza idadi ya walipakodi.
Mfanyabiashara huyo aliuomba uongozi wa TRA kuangalia namna bora ya kutoza kidi ya ongezeko la thamani (VAT) ili kuleta usawa na ushindani sokoni jambo ambalo Kamishna Mkuu wa TRA ameahifi kulifanyia kazi.
Kwa upande wake Mmiliki wa Kiwanda cha MAT kinachozalisha Pombe Kali maarufu kama Vinywaji changamshi,David Mulokozi amesema wataendeleza ubora na kusimamia sheria za TRA katika ulipaji wa kodi.
Naye Katibu wa Umoja wa wafanyabiasha mkoa wa Manyara (TCCIA), Zaynab Sadiki ameomba Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kuishauri Serikali iondoe sheria za kodi zilizopitwa na wakati ili kuboresha mazingira ya ufanyaji wa biashara.
Amesema katika mkoa wa Manyara wamekuwa na utaratibu wa kukutana na wafanyabiasha wenzao pamoja na Uongozi wa TRA ili kujadili na kutatua kwa pamoja changamoto zinazowakabili.
Katika msimu wa shukrani wa TRA kwa Mwezi December Kamishna Mkuu wa Mamlaka hiyo na mameneja wa mikoa yote wametoka ofisini na kuwafuata Walipakodi kwa lengo la kuwashukuru na kuwasikiliza huku wakitatua changamoto zao.
More Stories
NIDA yawakumbusha wananchi kuchukua vitambulisho vyao
Dkt.Kafumu:Uteuzi wa Rais Samia umezingatia katiba
Kliniki ya sheria bila malipo yazinduliwa Kilimanjaro