Na Jackline Martin, TimesMajira Online
Katika kipindi cha mwezi Julai – Septemba mwaka wa fedha 2024/25, Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imefanikiwa kukusanya kiasi cha Shilingi Trilioni 7.79, sawa na ufanisi wa asilimia 104.9 ya lengo la kukusanya Shilingi Trilioni 7.42, na kuvuka lengo la kila mwezi kwa miezi yote mitatu (Julai- Septemba).
Makusanyo hayo ambayo ni sawa na ukuaji wa asilimia 18.4 ikilinganishwa na kiasi kilichokusanywa mwaka 2023/24, ni ya kiwango cha juu ambacho hakijawahi kufikiwa na TRA kwa miezi ya Julai – Septemba ya mwaka wa fedha, ambayo ni sawa na ukuaji wa asilimia 77.4 ukilinganisha na makusanyo ya kipindi kama hicho katika mwaka 2020/21.
Hayo yalisemwa na Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Yusuph Mwenda Wakati akizungumza na waandishi wa Habari wakati akitoa taarifa ya makusanyo ya kodi kwa kipindi cha robo ya kwanza ya mwaka wa 2024/2025 (Julai-Septemba 2024)
Aidha Mwenda alisema katika kipindi hicho cha miezi mitatu kwa kila mwezi walikuwa na lengo la kukusanya ambapo wameweza kuvuka
Lengo kila mwezi
“Mwezi Julai tumekusanya asilimia 104, Agosti tumekusanya asilimia 104 na mwezi septemba tumekusanya asilimia 105, haya pia ni mafanikio kwamba ndani ya miezi mitatu tumeweza kuvuka lengo”
“ katika miezi hii mitatu, tumeweza kukusanya mwezi wa 9 jumla ya shilingi Trilioni 3.18 ikiwa ni kiwango cha juu kukusanywa tangu TRA kuanzishwa “ alisema
Pia alisema sababu ya kufika hapo ni kutokana na sera nzuri za uwekezaji na maagizo ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ambayo amekuwa akiyatoa na akiwataka wayatekeleze ikiwemo kujenga uhusiano mzuri na walipa kodi, kuwafanya walipa kodi ni watu wao wa karibu nao badala ya maadui, kuwasikiliza na kutatua changamoto zao kwa wakati.
“Hili tumelifanya sana ndani ya miezi mitatu na limekuwa ni moja ya sababu ya sisi kufanya vizuri hivyo tunamshukuru sana Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa uongozi wake na maagizo ambayo amekuwa akitupa”
Mwenda aliwashukuru walipa kodi wa Tanzania na kuhakikisha kwamba wanaendelea kutekeleza maagizo ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kujenga uhusiano na walipa kodi lakini pia kuwasikiliza na kuwafata walipo.
“Kama ambavyo tumetenga siku ya Alhamisi ya kuwasikiliza , tutaendelea kutatua changamoto zao kwa wakati na tutakua washirika wa biashara zao ili kuhakikisha biashara zinaenda na kuongeza walipa kodi na kufanya biashara zisifungwe ila ziongezeke zingine”
Pia alihakikisha kwamba wataweka mazingira sawa ya kufanya biashara kwa kutowapendelea wachache wasilipe kodi wanazostahili kulipa lakini pia kutowaonea wale ambao hawastahili kulipa kodi.
“Kodi hizi ndizo zinachangia maendeleo ya nchi yetu, wapo wengi wanaolipa lakini wapo wachache ambao wanatufanya tusifike pale tunapotaka kufika hivyo niwatake na wao waungane na wengine kulipa kodi na wasipofanya hivyo ili kuleta mazingira yaliyo sawa ya kufanya biashara haiwezekani mmoja alipe na mmoja asilipe, tumejipanga kuimarisha vitengo vyetu vya ukaguzi na uchunguzi na kupata taarifa kwa wakati ili wachache wanaokwepa kulipa kodi tuweze kuchukua hatua kwa mujibu wa sheria”
Kadhalika aliwataka watanzania wote wanapofanya manunuzi, wadai risiti na wanapouza watoe risiti.
More Stories
Amos Lengael Nnko afariki kwa ajali ya gari
Gridi za Tanzania, Kenya kuimarisha upatikanaji wa umeme
Mama Zainab:Watoto yatima ni jukumu la jamii yote