January 23, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

TRA yashauriwa kutumia mbinu mbadala kudhibiti wafanyabiashara wadanganyifu

Na Mwandishi wetu

MKUU wa Wilaya ya Busega Mkoani Simiyu Gabriel Zakariya ameishauri Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kutumia Mbinu mbadala ya kuwadhibiti wafanyabiashara wadanganyifu wanaowashawishi wanunuzi kutokudai risiti kwa madai ya kuwapunguzia bei ya bidhaa wanazonunua na kutoa risiti zenye thamani pungufu.

Ushauri huo ametoa alipotembelewa na ugeni wa Maafisa wa Mamlaka ya mapato Tanzania (TRA) uliongozwa na Meneja wa Elimu kwa Mlipakodi Julius Mjenga kwa lengo la kujitambulisha kwa Mkuu huyo kabla ya kuanza kwa zoezi la elimu ya mlango kwa mlango katika kampeni inayoendelea katika mkoa wa Simiyu.

Kampeni hiyo imelenga kuelimisha wafanyabiashara wa mkoa huo sambamba na kusikiliza changamoto zao ili kuzitafutia ufumbuzi.

Zakariya amesema kuwa katika siku za karibuni kumekuwa na mbinu kadhaa zinazotumiwa na wafanyabiashara katika utoaji wa risiti halali jambo ambalo linasababisha upotevu wa mapato ya serikali.

Amesema mbinu hizo ni pamoja na kutotoa risiti kwa wateja kwa madai ya kuwapunguzia bei ya bidhaa wanazonunua, kuwapa wateja wao risiti pungufu zisizolingana na bei halisi ya bidhaa hizo na kuwatafutia risiti nyengine kabisa zinazonyesha bidhaa nyengine tofauti kabisa na wateja wanazonunua.

Aidha, ametoa rai ya kutumia mbinu za kuiwandishi wa habari za uchunguzi kuwabaini wote wanaofanya mitindo hiyo kwa kuwaweka wazi kwenye vyombo vya habari na kuwachukulia hatua za kisheria ili iwe funzo kwa wengine kwa kufanya hivyo kutapunguza udanganyifu huo na kuwezesha TRA kufikia au kuvuka kabisa ya malengo ya makusanyo.

Pia, amepongeza TRA kwa makusanyo makubwa na jitahda zao na kuendelea kutoa elimu ya Kodi kwa wafanyabiashara pamoja na kusikiliza changamoto zao .

Katika hatua nyingine amewataka TRA kuendelea na jitihada hizo jambo ambalo litaongeza ulipaji wa Kodi kwa hiari na kuchochea zaidi kasi ya ya ukusanyaji wa mapato ya Serikali.

Kwa upande wake Julius Mjenga amesema kuwa zeozi linaendelea vizuri mkoani humo na wamekua wakipokea changamoto na maoni kadhaa kutoka kwa wakuu wa mikoa na wafanyabiashara mkani humo ikiwemo kusongezewa huduma katika maeneo yao ili kurahisisha ulipaji wa kodi kwa hiari na kuwapunguzia gharama za usafiri.

Timu ya maafisa ya TRA inaendelea na Kamapeni yake ya Elimu ya mlango kwa mlango ambapo zoezi hilo linatarajiwa kuhitimishwa wiki wilayani Miatu mkoani Simiyu.