December 12, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

TRA yapandisha ujumbe wa kodi kilele cha Mlima Kilimanjaro

Na Mwandishi wetu, Timesmajira

Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imepandisha ujumbe wake wa Kodi katika Kilele cha Mlima Kilimanjaro ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya miaka 63 ya Uhuru wa Tanganyika na kuongeza hamasa kwa walipakodi.

Akizungumza baada ya zoezi la kupanda Mlima Kilimanjaro kukamilika Meneja wa TRA mkoa wa Kilimanjaro,James Jilala amesema lengo la kushiriki kupanda Mlima ni kupeleka kileleni ujumbe wa kuhamasisha ulipaji wa kodi kwa hiari kwa kuzingatia sheria za kodi na kuongeza mapato ya serikali kwa maendeleo ya taifa letu.

“Zoezi hili la kujumuika na wapandaji wengine kwenda kwenye kilele cha mlima kilimanjaro, ni jambo la makusudi kuiweka TRA karibu na walipakodi, Utalii ni moja ya sekta inayoingizia serikali mapato kwa wingi ikiwa ni pamoja na kodi inayokusanywa na TRA. Hii ni kuonyesha pia kuwa TRA iko karibu sana na sekta ya utalii na itaendelea kuweka mazingira na mifumo rafiki ya ulipaji wa kodi” amesema Jilala.

Ameutaja ujumbe uliopandishwa kileleni ukiambatana na picha ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kuwa ni “Tuwajiibike kulipa kodi kwa maendeleo ya Taifa letu “.

Jilala amesema sekta ya utalii ni miongoni mwa maeneo yanayoingiza mapato mengi ya kodi kwa TRA hivyo ushiriki wa Mamlaka hiyo katika kupanda Mlima Kilimanjaro kupitia Kampeni ya Twende Zetu Kileleni ni kuitambua sekta ya utalii kama mlipakodi mzuri.

Amesema ujumbe mwingine uliobebwa na wafanyakazi wa TRA waliopanda Mlima Kilimanjaro ni kuhusu Kulipa kodi kwa hiari na kwa mujibu wa sheria ili Tanzania iwe kinara katika masuala ya uchumi kwa kuwa na uchumi imara.

Aidha Meneja huyo wa TRA mkoa wa Kilimanjaro ametoa rai kwa wananchi kulipa kodi kwa wakati kabla ya kufika December 31 ambao ndiyo mwisho wa mwaka wa biashara ili kuepuka adhabu.

Jilala amesema wamewekeza nguvu kubwa katika mwezi Disemba kwasababu wafanyabiasha wengi wanafunga mapato yao na kwa TRA kodi yote ya awamu ya nne inapaswa kukusanywa mpaka kufikia Disemba 31/2024.

Kwa upande wa wafanyakazi wa TRA waliopanda Mlima Kilimanjaro na kuweka Bendera ya TRA kileleni wamesema wanajivunia kutekeleza jukumu hilo la kizalendo linaloonyesha uhusiano baina ya Mamlaka hiyo na sekta ya utalii katika kuenzi Uhuru wa Tanganyika.

“Kwetu sisi imekuwa fahari kwa kufanya jambo hili la kizalendo kwa nchi yetu kuhamasisha ulipaji kodi kwa hiari kwa maendeleo ya taifa letu. Na tunamshukuru sana Kamishina Mkuu kwa kutuamini na kufanikisha. Tunaamini kuwa mwaka ujao tutakuwa wengi zaidi” amesema Yusuph Said Mwahi Kiongozi wa timu kutoka TRA.

Wafanyakazi nane wa TRA waliopanda Mlima ni pamoja na Yusuph Said Mwahu ambaye ni kiongozi wa timu, Jeremiah Peter Sarungi, Shabani Rashid Mwanga, George Fumbuka Mathias, Lilian Geofrey Dulley, Emmanuel Expedito Ngungulu, Daudi Msimbe Said na Polient Christopher Shayo.