May 18, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

TRA yabaini ukwepaji kodi mkubwa viwandani

Na Mwandishi wetu, Timesmajira

Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Bw. Yusuph Juma Mwenda leo tarehe 17.05.2025 amefanya ziara ya kushitukiza kwenye baadhi ya Viwanda vilivyopo wilayani Mkuranga mkoani Pwani na kubaini kuwepo kwa ukwepaji mkubwa wa Kodi unaofanywa na wamiliki wa Viwanda hivyo.

Akiwa katika kiwanda cha kuzalisha viatu vya Plastiki maarufu kama Yeboyebo cha DOLIN Investment Company Ltd na Kiwanda cha nondo cha Fujian Hexingwang Industry Tanzania Ltd vyote vikiwa vinamilikiwa na wageni, Kamishna Mkuu Mwenda amesema TRA itafanya uchunguzi wa kiwango Cha Kodi kilichokwepwa ambacho kitalipwa sambamba na Riba pamoja na adhabu.

Kamishna Mkuu Mwenda amesema walipata taarifa kutoka kwa wasamalia wema pamoja na Watumishi wa TRA kwenda kujiridhisha kuhusu kuwepo ukwepaji Kodi na alipofika amebaini kuwepo kwa hali hiyo hivyo Kodi yote ambayo haijalipwa, itapaswa kulipwa na Riba pamoja na adhabu.

“Watumishi wa TRA watakuwepo kwenye hivi Viwanda kwa mwezi mmoja kufanya uchambuzi na ufuatiliaji ili kupata thamani halisi ya Kodi ambayo inapaswa kulipwa” amesema Mwenda.

Kamishna Mkuu Mwenda amewaonya wote wenye tabia ya kukwepa Kodi kujisalimisha maana ukwepaji wa Kodi una athari kubwa na mwisho wa siku ni lazima ilipwe, hivyo amesema Kukwepa Kodi kwa sasa ni kuchelewesha kuilipa tu.

Aidha amewapongeza wamiliki wa Viwanda kwa kufanya Uwekezaji mkubwa na kuwaajiri Watanzania.