Fresha Kinasa,TimesMajiraOnline,Mara.
MKUU wa Mkoa wa Mara, Kanali Evans Mtambi, ameitaka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) mkoani humo kuendeleza ushirikiano na wafanyabiashara pamoja na kuwapa elimu ili kuwajengea uwezo wa kibiashara.
Amesema hatua hiyo itachochea ufanisi katika shughuli zao, kuimarisha uaminifu, na kukuza uzalendo wa kulipa kodi kwa hiari kwa maendeleo ya mtu binafsi na taifa kwa ujumla.
Kanali Mtambi ametoa wito huo Septemba 12, 2025, wakati wa uzinduzi wa Dawati Maalum la Uwezeshaji Biashara kwa Mkoa wa Mara, hafla iliyofanyika katika ofisi za TRA zilizopo Manispaa ya Musoma.
“Kupitia dawati hili, TRA sogezeni huduma kwa wafanyabiashara wasio katika sekta rasmi ili kuwapa elimu ya jinsi ya kuzirasimisha biashara zao. Vilevile, muimarishe uhusiano na sekta binafsi ili kujenga uwezo wa kibiashara kwa Watanzania,” alisema Kanali Mtambi.

Aidha, amewataka maafisa wa TRA kulitumia dawati hilo kubaini na kutatua changamoto zinazowakabili wafanyabiashara wote wa sekta rasmi na isiyo rasmi kwa lengo la kukuza biashara zao.
“Endeleeni kuwahudumia kwa moyo wa dhati wanapofika ofisini ama mnapowaendea. Elimu bora ya kodi na huduma rafiki kwa mlipa kodi ndicho kitawasukuma kulipa Kodi kwa hiari,” amesisitiza.
Aidha, Mtambi ameipongeza TRA Mkoa wa Mara kwa mafanikio katika ukusanyaji wa kodi kwa mwaka wa fedha 2024/2025, ambapo ukusanyaji ulifanyika kwa ufanisi bila kuwepo kwa migongano na wafanyabiashara. Aliwahimiza pia watumishi wa TRA kuendelea kutoa huduma bora kwa weledi na uzalendo ili kuongeza tija.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Wamachinga Mkoa wa Mara, Charles Waitara, ameipongeza TRA kwa kuanzisha dawati hilo Mkoani humo, huku akisema hatua hiyo italeta majibu kwa changamoto mbalimbali zinazowakabili wafanyabiashara.
“Zamani Wamachinga walikuwa wakifukuzana na TRA, lakini sasa hali hiyo haipo kabisa. Mahusiano ni mazuri sana. Naomba wafanyabiashara waendelee kulipa kodi kwa hiari, kwa sababu hakuna nchi duniani inayoendeshwa bila kodi. Kodi ndiyo msingi wa maendeleo yetu,” amesema Waitara.
Waitara pia amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuwawezesha Wamachinga kwa kuwatengea maeneo ya kufanyia biashara na kutoa mkopo wa Shilingi Bilioni 18.5 unaowasaidia kukopeshana na kukuza biashara zao.
Awali, Meneja wa TRA Mkoa wa Mara, Nasoro Ndemo, ameeleza kuwa kwa mwaka wa fedha 2024/2025 walipangiwa kukusanya Shilingi Bilioni 190.1, ambapo walivuka lengo kwa kukusanya Shilingi Bilioni 194.62, sawa na ufanisi wa asilimia 102. Amesema mafanikio hayo yalichangiwa kwa kiasi kikubwa na ushirikiano mzuri pamoja na ulipaji wa hiari wa wafanyabiashara
“Kupitia dawati hili tutawatambua wafanyabiashara, kuwawezesha, kusikiliza changamoto zao na kuzitatua. Lengo ni kusogeza huduma karibu na walipo, kuwasaidia kuunganishwa na huduma nyingine, kuwajengea mahusiano na kuwapa elimu ya biashara,” amesema Ndemo.
Baadhi ya wafanyabiashara waliohudhuria uzinduzi huo wamesema kuwa uwepo wa dawati hilo utawawezesha kufanya biashara katika mazingira bora, ya kirafiki na yenye ushirikiano mzuri na serikali, hali itakayowahamasisha kulipa kodi kwa hiari.
Dawati hilo ni sehemu ya utekelezaji wa maelekezo ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuimarisha sekta ya biashara nchini.Ambapo Kamishna Mkuu wa TRA, Yusuph Mwenda, alilizindua kitaifa Agosti 16, 2025, mkoani Morogoro.
Sekta ya biashara hapa nchini, imeendelea kukua na kuchangia kwa kiasi kikubwa maendeleo ya uchumi wa Taifa na kuwezesha miradi mbalimbali ya maendeleo kutekelezwa.


More Stories
Bilioni 7 kuwainua vijana 308 sekta ya uvuvi
Clara:Miaka 50 ya Sabasaba fursa mpya za Biashara na Uwekezaji
Usajili wa Laini za Simu: Jilinde Dhidi ya Kutumiwa Vibaya kwa Utambulisho Wako