Na Martha Fatael, TimesMajira,Online Moshi
MAMLAKA ya Mapato Tanzania (TRA) mkoani Kilimanjaro imeonya tabia ya baadhi ya watu wanaowasaidia wafanyabiashara kukwepa kulipa kodi kwa njia mbalimbali.
Aidha, Mamlaka hiyo imeomba ushirikiano kwa wakazi wa Mkoa wa Kilimanjaro kufichua baadhi ya wafanyabiashara wasio waaminifu wanaoingiza bidhaa kwa njia za panya ikiwemo wanaokwepa kulipa Kodi.
Onyo hilo limetolewa leo na Meneja wa TRA mkoani hapa, Masawa Masatu, wakati akizungumza kwenye mafunzo kwa waandishi wa habari na walimu ambao ni mabalozi wa kodi wa TRA kutoka shule mbalimba kuhusu mabadiliko ya sheria mbalimbali za kodi zilizobadilisha baadhi ya tozo, ada na kodi.
“Nawaomba tusiwe sehemu ya watu wanaosaidia wafanyabiashara kukwepa kulipa kodi kwa kutodai risiti pindi tunapokwenda kufanya manunuzi mbalimbali. Tunaomba mdai risiti tena za VAT (Kodi ya Ongezeko la Thamani) ili wafanye return halisi,”amesema Masatu.
Ametoa wito kwa wananchi kufikisha taarifa za wasiotoa risiti, wakwepa kodi wa aina zote na wanaoingiza bidhaa nchini kinyume na utaratibu bila kulipia ushuru, ada na tozo mbalimbali.
“Mkoa huu ni miongoni mwa mikoa yenye njia za panya nyingi na hutumika sana katika kuingiza magendo, tunaomba tuwe wazalendo kwa kutoa taarifa za wanaofanya hujuma hizo ili wachukuliwe hatua na Serikkai ipate kodi kwa maendeleo ya wote,” Amesisitiza Masatu.
Akiwasilisha mada katika kikao hicho, Ofisa Elimu na Huduma kwa Mlipa Kodi, Odupoi Papaa amesema kwa mujibu wa bajeti ya nchi iliyowasilishwa bungeni ya mwaka 2021/22 ya sh. trilioni 36.33, mamlaka hiyo pekee inapaswa kukusanya sh. trilioni 22.18 kutoka kwa walipa Kodi hapa nchini.
Awali, Katibu wa Klabu ya Waandishi wa Habari Kilimanjaro, Nakajumo James, ameiomba mamlaka hiyo kuanzisha mpango maalum na kuwahusisha waandishi wa habari wa kuibua masuala ya ukwepaji kodi kwa kutumia njia za panya.
More Stories
CRDB yazindua matawi Majimoto, Ilula kuwahudumia wananchi
Lina PG Tour yafufua gofu Moshi
Kampeni ya Sako kwa Bako yawafikia Kanda ya Kati