June 15, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

TPTC kuendelea kuendesha kozi ya ulinzi wa amani kwa Watanzania

Na Penina Malundo ,Timesmajira

Mkuu wa Jeshi la Anga, Meja Jenerali Shaban Mani amesema kuwa Chuo cha Ulinzi wa Amani Tanzania (TPTC) kina mpango wa kuendelea kuendesha kozi zitakazosaidia na kuwajengea uwezo watanzania wote wakiwemo wanajeshi, polisi na raia wa kawaida katika kwenda kushiriki kulinda amani ndani na nje ya nchi.

Meja Jenerali Mani ameyasema hayo mwishoni mwa wiki jijini Dar es Salaam wakati akifunga mafunzo ya ulinzi wa amani yaliyotolewa na Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) katika Chuo hicho cha TPTC chini ya ufadhili wa serikali ya Japan na Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNPD).

Amesema mafunzo hayo yaliyotolewa yanalengo la kuwaandaa na kuwawezesha raia kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi na waledi wanapokuwa katika jukumu la ulinzi wa amani ndani na nje ya nchi.

“Mafunzo haya ya mwanzo ni hatua muhimu katika safari ya Tanzania kwenye ulinzi wa amani,yanalenga kuhakikisha kuwa kila anayeshiriki katika misheni anakidhi viwango vya kimataifa.

“Hivyo huu ni mwanzo tu wa mpango mpana zaidi, na kwamba mafunzo mengine yatafuata hivi karibuni kwani chuo cha TPTC kina mpango wa kuwa kituo kikubwa cha kikanda katika kufundisha watu kwenda kulinda amani wakiwemo wanajeshi, polisi na raia wa kawaida,”amesema.

Aidha amesema katika kulinda amani raia wa kawaida wana nafasi muhimu hivyo kupitia Serikali ya Japan na UNDP wameweza kuandaa kozi yao ambayo inashirikisha raia katika ulinzi wa amani.

“Kozi hii inatupa uwezo wa kujijenga zaidi kwa kuhakikisha kwamba kila tunapokwenda kwenye misheni ya kulinda amani tunakuwa tumekamilika katika Idara zote kwa kuwa na watu wenye weledi kwenye kufanya kazi zao kulingana na taratibu na sheria zinazotaka raia aende kufanya.

Kwa Upande wake Mwakilishi Mkaazi wa UNDP, John Rutere amesema shirika lao litaendelea kufanya kazi na serikali ya Tanzania katika kuhakikisha raia wanapata mafunzo hayo ya ulinzi wa amani.

Naye Mwakilishi wa Ubalozi wa Japan, Nomura Hiroyuki amesema Japan inajivunia kusaidia mpango huo kama sehemu ya kujitolea kwake katika kuendeleza amani duniani na kuinua jamii.

“Tunaamini kuwa kwa ushirikiano na dhamira ya pamoja, hata mataifa ya mbali kama Japan yanaweza kuwa na mchango chanya katika maeneo ya ndani kama haya,” amesema.

Mmoja wa watu waliopata mafunzo hayo ambaye ni Ofisa Mambo ya Nje kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Nice Munissy amesema moja ya majukumu waliofundisha ni kuhakikisha wanatekeleza sera ya mambo ya Nje ikiwemo kuimarisha ulinzi wa amani ambayo inagusa maslahi ya watu wote.