March 7, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

TPDC yatangaza neema kwa watumiaji gesi asilia kwenye magari

Na Agnes Alcardo, Timesmajira Online

SHIRIKA la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), limetangaza neema kwa watumiaji wa gesi asilia katika magari,kwa kuongeza  wigo wa upatikanaji wa huduma hiyo, ikiwemo ujenzi wa vituo vipya vya kujaza nishati hiyo.

Kaimu Mkurugenzi wa Biashara ya Petroli TPDC ambayo inahusisha gesi na mafuta, Mhandisi Emmanuel Gilbert,amebainisha hayo jijini Dar-es- Salaam,wakati akizungumza  na waandishi wa habari katika kituo mama cha gesi asilia iliyoshindiliwa (CNG), kilichopo maeneo ya Chuo Kikuu cha Dar-es-Salaam(UDSM).

Mhandisi Gilbet amesema kituo hicho kinauwezo wa kujaza gesi  magari pia kutoa bidhaa hiyo na kupeleka katika vituo dada ambavyo vipo nje ya mfumo wa maboma yanayosambaza nishati hiyo.

Amesema uzinduzi wa huduma katika kituo hicho ulifanyika mwishoni mwa Mei, mwaka huu na hadi sasa wapo hatua za mwisho za kukabidhiwa kituo na mkandarasi.

Hata hivyo, amewatoa hofu wadau, wateja na wananchi, kwamba matatizo yanayojitokeza katika kituo hicho akisema kuwa ni ya kiufundi na kuwahakikishia kuwa hawawezi kupata msongamano katika utoaji huduma.

Pia amesema, mbali na kituo hicho ambacho kinahudumia magari 600 kwa siku na bajaji kati ya 600 hadi 700, hadi hivi sasa kuna miradi ya vituo vinne vipya ambavyo vipo hatua za ujenzi.

Ameitaja miradi hiyo kuwa ni ya kampuni ya Puma Energy Tanzania ambayo ina vituo vingi vya mafuta, inajenga kituo mama cha CNG eneo la IPTL Tegeta, kitakuwa na uwezo wa kutoa gesi na kupelekwa kituo dada, sanjari na hicho inajenga kituo dada Mabibo External ambapo ataweka gesi asilia katika kituo chake cha mafuta na Mbezi Tangibovu.

“Utekelezaji wa mradi huu kwa mujibu wa Puma itakapofika Novemba mwishoni, mwaka huu, vituo hivyo vyote vitakuwa vinafanya kazi,”amesema.

Huku mradi mwingine ni wa ujenzi wa kituo kipya  barabara ya Cocacola, kinachojengwa na mwekezaji binafsi Energo Tanzania Limited. Amesema mwekezaji huyo ameshapelekewa bomba la gesi na taarifa alizowapa TPDC kufikia mwishoni mwa Agosti, mwaka huu, kituo kitakuwa kinafanya kazi kwa kuwa mitambo yote alishaileta ipo nchini.

Ameongeza mkabala na kituo mama cha TPDC, kampuni ya ‘Master Gas’ imejenga kituo cha CNG ambacho ni cha pili na inaendelea na ujenzi wa cha tatu kitakachojengwa Mbezi Africana, hivi sasa mkandarasi yupo eneo la ujenzi anaendelea na kazi na itakapofikia Desemba, mwaka huu, kitakuwa kinafanya kazi.

Katika kurahisisha upatikanaji wa nishati hiyo, Mhandisi Gilbert amesema katika barabara ya Nyerere, mwekezaji wa kituo cha kujaza mafuta cha Victoria Service Station Limited, ameamua kuweka mitambo ya kuwezesha kujaza gesi asilia katika magari.

Ameongeza vituo vingine vinajengwa maeneo ya Goba, Tabata,Kigamboni, na Kibada, huku kampuni zinazojenga vituo ni Tanzania Natural Gas Holdings na Anric Gas Technology Tanzania Company Limited ambao wanajenga Kigamboni na Kibada.