December 22, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

TPA yadhamiria kung’arisha bandari ya Mwanza Kaskazini

Raphael Okello, Timesmajira

BANDARI ni sehemu muhimu hasa katika nchi ambazo zimezingirwa na maji pande zote au upande mmoja.

Nchi kama hizo hutegemea huduma ya bandari kuwa sehemu au mlango muhimu kwa ajili ya kusafirisha watu au mizigo hivyo kuipatia nchi husika faida inayotokana na ushuru wa bidhaa zinazopitishwa katika bandari hizo.

Tanzania tumezungukwa na maji upande wa Mashariki(Bahari ya Hindi),Kusini- Magharibi( ziwa Nyasa), Magharibi( Ziwa Tanganyika) na Kaskazini Magharibi (Ziwa Victoria).

Tunajua wazi kuwa kuanzia Bahari ya Hindi hadi Ziwa Victoria huduma za bandari zimewekwa kwa ajili ya kusaidia usafirishaji wa watu na mali zao.

Kupitia Bahari ya Hindi Tanzania ina Bandari ya Dar-es-Salaam, Tanga , Mtwara huku katika Ziwa Victoria tunazo bandari za Mwanza, Kemondo na zinginezo na katika makala hii imejikita kuelezea Bandari ya Mwanza Kaskazini.

Meneja wa Mamlaka ya Bandari Tanzania(TPA) Ziwa Victoria,Erasto Lugenge anaeleza kuwa mwaka wa fedha 2023/24 mamlaka hiyo ilitenga kiasi cha bilioni 18.6 kwa ajili ya upanuzi wa Bandari za Ziwa Victoria ikiwemo ya Mwanza Kaskazini.

Ambapo anaeleza kuwa mradi huo wa kimkakati wa uboreshwaji na upanuzi wa bandari hiyo umefikia asilimia 37 na unatarajiwa kukamilika mapema mwaka huu.

Anasema asilimia hizo zilizofikiwa zinajumuisha maegesho ya meli, sakafu ngumu, miundombinu ya kuhifadhia mafuta, mifereji ya maji na miundombinu ya barabara.

Kazi zingine ni pamoja na kuweka miundombinu ya umeme, jengo la ukaguzi wa abiria na mizigo, uzio wa bandari ,kuhamisha miundombinu ya meli na madaraja katika bandari ya Mwanza Kusini na ujenzi wa kingo za mto Mirongo.

Kwa mujibu wa Lugenge mradi huo ni utekelezwaji wa mipango ya serikali kulingana na Ilani ya CCM ya Mwaka 2020- 2025 na maendeleo ya Taifa mwaka 2025-2050 mkoani Mwanza.

Anabainisha kuwa kumalizika kwa mradi huo, kutasaidia kurahisisha usafiri na usafirishaji katika Ziwa Victoria pamoja na kuboresha uchumi wa nchi na Mkoa wa Mwanza kwa ujumla tofauti na siku za nyuma ambapo usafirishaji ulitegemea bandari ya sasa ambayo ni finyu zaidi.

Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Nyamagana, Peter Bega anasisitiza kuwa kukamilika kwa mradi huo kutawezesha meli ya MV. MWANZA ianze kutoa huduma kwa wananchi na kuagiza kazi ifanyike mchana na usiku kwa kuzingatia mkataba wa mradi.

Anaeleza faida ya kukamilika kwa mradi huo kuwa Halmashauri ya Jiji la Mwanza itanufaika lakini serikali kuu itakusanya mapato na ushuru wa bidhaa pindi meli zitakapoanza safari za kibiashara.

Amos Makalla aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, kabla ya kuteuliwa kuwa Katibu wa Itikadi, Mafunzo na Uenezi wa CCM Taifa aliwaagiza wafanyabiashara wa samaki katika eneo la mradi kupisha mara moja ili kuwezesha kazi kuendelea bila kikwazo.

Kutokana na shughuli hiyo ,Mamlaka za Halmashauri ya Jiji la Mwanza zinaagizwa kuwatafutia sehemu za kufanyia shughuli zao wafanyabiashara hao ili wasiweze kuathiriwa na zoezi linaloendelea la upanuzi wa bandari hiyo.

Kwa upande mwingine Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu ilipotembelea mradi huo hivi karibuni iliridhishwa na kazi ya utekelezaji wa ujenzi ,uboreshaji na upanuzi wa bandari ya Mwanza kaskazini.

Mwenyekiti wa Kamati Kudumu ya Bunge ya Miundombinu,Suleiman Kakoso wakati wa ziara ya kamati hiyo ya kutembelea mradi huo wa bandari ya Mwanza Kaskazini anasema nihatua ya makusudi aliyochukua Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan kuhakikisha kuwa Bandari za Ziwa Victoria zinaboreshwa kwa ajili ya usafirishaji.

Kakoso anasema Kamati hiyo ya Bunge imeridhishwa na utekelezwaji wa mradi hiyo pamoja na miradi mingine yote ya TPA iliyotembelewa.

Kwamba hatua hiyo ya serikali kutoa fedha hizo kwa upanuzi wa bandari kanda ya Ziwa inatokana na malengo ya kuboresha miundombinu ya usafirishaji majini.

Ambapo anamtaka Meneja huyo wa TPA Ziwa Victoria kuendelea kusimamia mradi huo na kumalizika kwa wakati ili ulete faida kwa Watanzania na kwamba Bunge haitanyamaza itakapoona fedha hizo za serikali zinapotea bila kukamilisha bandari hiyo ya Mwanza Kaskazini.

Aidha anasisitiza kuwa upanuzi na uboreshwaji wa bandari uendane na dhamira ya ubinafsishaji wa Bandari ya Dar es salaam uliofanywa hivi karibuni.

Anasema kutokana na ahadi ya kukamilika kwa ujenzi wa meli ya MV Mwanza “Hapa Kazi Tu” unaotarajiwa kukamilika Mei mwaka huu inahitajika juhudi za haraka kukamilisha upanuzi wa ghati katika bandari hiyo.