Na Allan Kitwe, Timesmajira Online-Tabora
MAMLAKA ya Dawa na Vifaa Tiba nchini (TMDA),imewaonya wanawake kutokubali kudanganywa kuwa kuna dawa ya kuongeza makalio au matiti,kwani suala hilo ni uongo na utapeli.
Onyo hilo limetolewa na Mkurugenzi Mkuu wa TMDA, Dkt.Adam Fimbo,akiongea na waandishi wa habari kutoka Mikoa 3 ya Kigoma, Katavi na Tabora kwenye kikao kazi cha siku moja kilichofanyika mjini Tabora.
Dkt Fimbo,amesema kuwa hamna ukweli wowote kuwa kuna dawa inayosaidia kuongeza ukubwa wa makalio au matiti kwa wanawake,hivyo amewatahadharisha wanawake kutokubaliana na maneno ya kitapeli.
Amesisitiza kuwa hakuna ushahidi wowote wa mtu aliyetumia dawa hizo na kubadilisha maumbile yake akabaki salama, hivyo akawataka kuomba ushauri wa madaktari kabla hawajafanya kitu chochote ili kutojiingiza kwenye matatizo.
‘Ni jukumu la TMDA,kufuatilia dawa na vifaa tiba vyote vinavyozalishwa nchini hapa,na vile vinavyoingizwa kutoka nchi za nje,kutoa taarifa kwa jamii juu ya bidhaa zinazofaa na zisizofaa kwa matumizi yao,” amesema.
Pia amesema ni jukumu la TMDA kuhakikisha bidhaa zote zinazoingizwa sokoni kwa ajili ya matumizi ya binadamu zinafuatiliwa ili kujiridhisha kama zinafaa au la na kuchukua hatua.
Huku akisisitiza wapewe taarifa endapo kuna sawa ambazo TMDA walipiga marufuku kuuzwa nchini hapa lakini bado zinauzwa maeneo mbalimbali ili waweze kuchukua hatua za kisheria.
Meneja wa TMDA Kanda ya Magharibi Christopher Migoha, amesema kuwa wamejipanga kuhakikisha dawa na vifaa tiba vyote vinavyouzwa katika Kanda hiyo vinakuwa na ubora unaotakiwa na kufuatiliwa.
Amesema,ili kudhibiti uingizaji holela wa dawa na vifaa tiba feki,wameendelea kutoa vibali vya uingizaji na usafirishaji nje ya nchi bidhaa hizo na kuongeza ukaguzi wa bidhaa zote katika halmashauri na vituo vyote vya forodha.
Migoha amebainisha kuwa wameongeza timu ya ukaguzi na ufuatiliaji katika maeneo yote na kuanzisha klabu za wanafunzi katika shule mbalimbali.
.

More Stories
Usajili wa Laini za Simu: Jilinde Dhidi ya Kutumiwa Vibaya kwa Utambulisho Wako
TTCL yaadhimisha siku ya Wanawake kwa kutoa msaada JKCI
Wananchi Dodoma washauri TBA kujenga nyumba za kupangisha watu binafsi