May 6, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

TMDA yamkamata mtuhumiwa wa utengenezaji dawa bandia

Na Mwandishi wetu, timesmajira

MAMLAKA ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA) Kanda ya Mashariki imefanikiwa kumkamata mtuhumiwa wa uhalifu wa utengenezaji na usambazaji wa dawa za binadamu bandia, mkazi wa Kipawa, Ilala, bw Williams Mwangile ambaye amekutwa na vitu mbalimbali ikiwemo dawa, lebo na vifungashio.

Mtuhumiwa huyo ambaye inadaiwa hutengeneza na kusambaza dawa hizo mijini na vijijini na nchi jirani, amekamatwa kufuatia uchunguzi wa TMDA na vyanzo mbalimbali vya kipelelezi kubaini na kumfuatilia mtuhumiwa huyo,

Akielezea katika eneo la tukio, mkaguzi wa dawa wa TMDA Kanda ya Mashariki, Japhari Mtoro amesema kuwa:

“TMDA ilikuwa inamtafuta mtuhumiwa huyo Williams Mwangile umri 39 mkazi wa Matembele Lodge eneo la Kipawa Ilala Dar es Salaam kwa tuhuma za kuzalisha na kusambaza dawa hizo bandia, kwa mfumo wa makopo kinyume cha kifungu cha 76 cha sheria ya dawa na vifaa tiba sura ya 219”.

“Mtuhumiwa amepatikana April 14, 2023 jioni kufuatia kukamatwa kwa baadhi ya dawa ambazo alikuwa tayari amezisambaza.

Lakini pia baadhi ya washirika wake, TMDA ilishawakamata pamoja na baadhi ya dawa na kwa hiyo tulikuwa tunamfuatilia Williams Mwangile na baada ya kukamatwa tulimfanyia uchunguzi katika nyumba yake na nyumba ya wazazi wake” Amesema Japhari Mtoro

Ambapo amebainisha kuwa, TMDA na Jeshi la Polisi na serikali ya mtaa wamefanya upekuzi huo na kufanikiwa kupata vitu mbalimbali.

“Nyumbani kwake tulibahatika kupata lebo 537 ambazo zina majina ya dawa mbalimbali, (printed labels)
Lakini pia tulikuta Makopo 12 tupu ambayo pia yanatumika kufungasha dawa,

Pia tulikuta viroba vitatu, kiroba kimoja Unga wa njano na viwili Unga mweupe.” Amesema Japhari

Hata hivyo baada ya kukamilika upekuzi nyumbani kwa mtuhumiwa, usiku wa manane waliweza pia kupekua nyumbani kwa wazazi wake ambapo walibaini uwepo wa vitu mbalimbali ikiwemo vufungashio vitupu ya dawa aina ya rangi mbili ‘capsule’

“Lakini pia nako tumekuta lebo, jumla ya lebo 142 Nyumbani kwa wazazi wake, ambao inafanya jumla ya lebo zilizokamatwa kuwa 679, kwa hiyo baada ya kumpata mtuhumiwa huyu ataunganishwa na wale waliokamatwa kwa ajiri ya kufikishwa kwenye vyombo vya Sheria,

Japhari amesema tukio hilo ni la uhalifu dhidi ya binadamu kwani ni la unyama na ukatili wa hali ya juu kwani mtu anazalisha dawa bandia, dawa ambazo pengine hamna kitu humo ndani, mtu anatumia dawa anategemea atapona, lakini anakutana na dawa bandia na uwezekano wa kupoteza maisha ni mkubwa.”

Ambapo amesema hatua kali za kisheria zitachukuliwa kwa dhidi ya atakayethibitika kujihusisha na uzalishaji na usambazaji wa dawa bandia,

“Lakini pia nitumie fursa hii kuwashukuru sana wadau mbalimbali na viongozi wa serikali ya mtaa, jeshi la Polisi, wananchi kwa ushirikiano mkubwa walioutoa kwa kukamatwa kwa mtuhumiwa huyu, kwani tulikuwa tunamtafuta tangu mwezi wa Tatu mwaka huu, hadi leo tumemkamata” amesema Japhari.

Kwa upande wake Marygrory Mambo ambaye ni Mjumbe wa shina namba 6 mtaa huo wa Matembele ya kwanza maarufu Matembele Lodge,
aliyekuwa akishirikiana na TMDA na jeshi la Polisi kwenye upekuzi huo, ameomba wananchi waendelee kushirikiana kutoa taarifa kwa TMDA kufichua hali kama hiyo ya watu wanaofanya ama kutengeneza dawa bandia.