Na Joyce Kasiki, Timesmajira Online
MAMLAKA ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA) imewahimiza wananchi kushiriki kikamilifu katika mapambano dhidi ya dawa bandia, vifaa tiba visivyosajiliwa na bidhaa duni kwa kutoa taarifa kuhusu wahusika, ikisisitiza kuwa hatua hiyo ni muhimu katika kulinda afya ya jamii.
Akizungumza na waandishi wa habari katika banda la TMDA kwenye Maonyesho ya 50 ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam (Sabasaba), Meneja Mawasiliano na Elimu kwa Umma wa TMDA, Gaudensia Simwanza, alisema kaulimbiu ya mwaka huu imeipa mamlaka hiyo fursa ya kuhamasisha wananchi kutambua hatari za matumizi ya dawa bandia na vifaa tiba ambavyo havijasajiliwa.
“Udhibiti wa dawa na vifaa tiba si jukumu la TMDA pekee, bali ni wajibu wa kila mwananchi. Wauzaji wa bidhaa hizi haramu wanaishi ndani ya jamii yetu, hivyo ushirikiano wa wananchi katika kuwafichua ni muhimu ili kulinda afya ya Watanzania,” alisema Simwanza.

Alieleza kuwa TMDA inatekeleza sera ya kulinda watoa taarifa (Whistleblowing Policy), ambayo inahakikisha usiri na usalama wa wananchi wanaotoa taarifa kuhusu watu wanaojihusisha na utengenezaji, uuzaji au usambazaji wa dawa, vifaa tiba na bidhaa nyingine zinazodhibitiwa na mamlaka hiyo.
Simwanza alisema matumizi ya dawa zisizosajiliwa ni hatari kwa kuwa ubora, usalama na ufanisi wake haujathibitishwa na mamlaka husika, hali inayoweza kusababisha mgonjwa kushindwa kupata tiba stahiki au kupata madhara makubwa zaidi kiafya.

Aliongeza kuwa dawa bandia zinaweza kuchelewesha uponaji wa mgonjwa, kupunguza uwezo wake wa kufanya kazi na kuzalisha, kuathiri kipato cha mtu binafsi na taifa, na wakati mwingine kusababisha ulemavu au hata kifo kutokana na kuendelea kwa ugonjwa bila tiba sahihi.
“Tunawaomba wananchi wasikae kimya wanapoona dawa bandia, vifaa tiba visivyosajiliwa au bidhaa duni zikiuzwa. Kutoa taarifa ni hatua ya kulinda maisha yao, familia zao na jamii kwa ujumla,” alisisitiza.

More Stories
Mbunge awataka waendesha bodaboda kulinda amani
Tanzania yatoa wito kuimarisha ushirikiano Kimataifa utawala wa akili unde
Dkt.Nyansaho:Amani yaweka mazingira salama ya maendeleo nchini