July 7, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mbunge awataka waendesha bodaboda kulinda amani

Na Mwandishi Wetu, TimesMajira Online, Mbarali

MBUNGE wa Jimbo la Mbarali mkoani Mbeya, Bahati Ndingo, amewataka waendesha bodaboda wilayani humo kuwa walinzi wa amani kwa kukataa kushawishiwa na watu wanaotaka kuvuruga amani na utulivu.

Ndingo ametoa kauli hiyo Julai 6, 2026, alipokutana na waendesha bodaboda wa Wilaya ya Mbarali, akisisitiza kuwa kundi hilo lina nafasi kubwa ya kulinda usalama na mshikamano katika jamii.

“Msikubali kuwapokea wanaokuja kuwaambia mkachome biashara za wenzenu au mfanye vitendo vya uharibifu. Wakataeni kabisa,” amesema Ndingo.

Amesema baadhi ya watu wenye nia ovu wamekuwa wakijaribu kulitumia kundi la waendesha bodaboda kuchochea vurugu, hivyo akawataka waendelee kuwa mfano wa uzalendo kwa kulinda amani.

Mbunge huyo ameongeza kuwa kukosekana kwa amani husababisha hasara kubwa kwa wananchi, huzuia shughuli za kiuchumi, hupunguza uwekezaji na kudhoofisha maendeleo ya jamii.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodaboda Wilaya ya Mbarali ,Justin Minga alimhakikishia Mbunge huyo kuwa waendesha bodaboda wataendelea kufanya kazi zao kwa amani na hawatakubali kutumika katika vitendo vinavyoweza kuhatarisha usalama wa wananchi.

“Sisi hatuwezi kukubali kutumika kwa vitendo vya vurugu. Tutaendelea na shughuli zetu za uzalishaji kama kawaida na tutakuwa mfano wa kulinda amani, mshikamano na utulivu katika Taifa letu,” amesema Minga.