March 11, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

TMA yatoa tahadhari uwepo wa Kimbunga “JUDE”

Na Mwandishi wetu,Timesmajira

Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) inatoa taarifa ya uwepo wa kimbunga “JUDE” katika Bahari ya Hindi eneo la Rasi ya Msumbiji.

Uchambuzi wa mifumo ya hali ya hewa unaonesha kuwa kimbunga hicho kitaingia nchi kavu katika eneo la Msumbiji mchana wa leo tarehe 10 Machi 2024 na kupungua nguvu yake. Hata hivyo, Kimbunga “JUDE” kinatarajiwa kurejea tena baharini na kuimarisha nguvu yake katika kipindi cha kati ya tarehe 13 hadi 15 Machi 2025.

Aidha, kutokana na mwelekeo na umbali wake Kimbunga “JUDE” hakitarajiwi kuwa na athari za moja kwa moja hapa nchini. Hata hivyo, uwepo wa kimbunga hicho katika eneo la Rasi ya Msumbiji unatarajiwa kuchagiza mifumo ya hali ya hewa hapa nchini na kusababisha ongezeko la mvua katika maeneo mbalimbali. Vilevile, uwepo wa kimbunga hicho unaendana sambamba na kuanza kwa msimu wa mvua za Masika, 2025 katika maeneo yapatayo misimu miwili ya mvua kwa mwaka kama ilivyotabiriwa awali na taarifa kutolewa kwa Umma mnamo tarehe 31 Januari 2025.

USHAURI: Watumiaji wa bahari na jamii kwa ujumla wanashauriwa kuendelea kufuatilia na kuzingatia taarifa za utabiri kutoka Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania pamoja na kupata ushauri na miongozo ya wataalam wa kisekta.

Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) inaendelea kufuatilia mwenendo wa kimbunga “JUDE” na athari zake kwa mifumo ya hali ya hewa hapa nchini na itaendelea kutoa taarifa kila inapobidi.

https://www.instagram.com/p/DHA8ky6idiZ/?igsh=a2ZpNzh5dDk5MnYy