Na Judith Ferdinand, TimesMajira Online, Mwanza
MAOFISA Ugani wametakiwa kuwashauri wakulima aina gani ya mazao yanayopaswa kupandwa katika msimu huu kutokana na maeneo mengi ya jiji la Mwanza na Kanda ya Ziwa kutarajiwa kuwa na mvua za chini ya wastani (upungufu wa mvua).
Wito huo umetolewa na Meneja wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania(TMA) Kanda ya Ziwa Augustino Nduganda wakati akiwasilisha taarifa ya mwelekeo wa hali ya hewa katika Mkoa wa Mwanza kwa mvua za vuli kuanzia mwezi huu hadi Januari 2021, kwenye mkutano wa wadau wa kilimo Mkoa wa Mwanza.
Utabiri huo unaonesha eneo lote la Mkoa wa Mwanza linatarajiwa kuwa na mvua za chini ya wastani hadi wastani ikiwa kwa lugha rahisi upungufu wa mvua pamoja na vipindi virefu vya ukavu na kwa sasa mvua zimeishaanza kunyesha ambapo kuanzia Oktoba 1-16 mwaka huu kituo cha Mwanza kimepima jumla ya milimita(mm)22.1.
Amesema, kutokana na hali hiyo upungufu wa unyevunyevu katika udongo unatarajiwa kujitokeza, hali hiyo inatarajia kusababisha ukuaji hafifu wa mazao hivyo Maofisa Ugani wanapaswa kuwashauri wakulima aina ya mazao ya kupandwa katika kipindi hiki pia visumbufu vya mazao na magonjwa vinatarajiwa kuongezeka katika msimu huu huku malisho pamoja na maji kwa ajili ya mifugo vinatarajiwa kupungua hali ambayo inaweza kusababisha migogoro kati ya wakulima na wafugaji.
“Tukiangalia katika maeneo ya Mwanza mvua zimeishaanza, kwa ujumla utabiri tuliotoa TMA inaonyesha kuwa msimu huu wa mvua itakuwa chini ya wastani na tunatarajia upungufu wa mvua katika maeneo ya Kanda ya Ziwa, kutakuwa na hali ya upungufu wa unyevunyevu hali itakayo athiri kwa kiasi kikubwa ukuaji wa mazao katika maeneo haya,sisi kama TMA tunashauri Maofisa ugani waendelee kutoa ushauri kwa wakulima ni aina gani ya mazao ambayo yanaweza kupandwa katika msimu huu wa kilimo kutokana na mvua zitakuwa chache vilevile kutakuwa na visumbufu vya mazao ambavyo vitaathiri pia ukuaji wa mazao maeneo haya ya Kanda ya Ziwa,” amesema Nduganda.
Pia amewashauri wakulima waendelee kufuatilia taarifa za TMA zinazotolewa kila siku ili kujua hali ya hewa inaendeleaje licha ya kuwa wameisha toa muelekea kwa ujumla kuwa hali ya msimu wa mvua na waendelee kupata ushauri kutoka kwa maofisa ugani,pia ni vizuri kutunza chakula cha kutosheleza kwani Kuna uwezekano wa mazao kuathirika kwa kukosa mvua.
Katibu Tawala Mkoa wa Mwanza, Emmanuel Tutuba amesema, kila mdau atekeleze kwa wajibu wake yale yote walio azimia ili kukomboa Sekta ya kilimo ikizingatiwa kuwa mvua za msimu huu na serikali ya Mkoa itaendelea kutangaza fursa zolizopo na kuhamasisha wakulima ili waweze kuzitumia kwa mmoja mmoja na kupitia vyama vya ushirika.
Tutuba amesema, mikakati ya serikali ni kuendelea kujenga mazingira mazuri na miundombinu wezeshi ya fursa ya barabara, ardhi na watu wapewe ujuzi na utaalamu stahiki katika shughuli zao na wataalamu wakati wa kupanga bei ambazo zitafanya watu kuona fursa za kilimo na mikopo.
“Serikali inaendelea kuweka mazingira wezeshi ili watu waweze kupata hizo fursa kwa wakati ambapo na sasa imekuja bima ya kilimo ili kuwasaidia wakulima pembejeo zinapatikana hivyo ionekane namna ya kuwafikia ili kujua kanuni na muongozo wa kufikia fursa hizo hivyo kila mmoja atumie fursa zolizopo ili kukomboa mkulima kutoka kilimo cha kujikimu mpaka cha biashara,” amesema Tutuba.
Akizungumzia zao la pamba Mkurugenzi wa Huduma za Usimamizi Bodi ya Pamba Tanzania (TCB) James Shimbe, amesema zao hilo alitakiwi kuchanganywa na mazao mengine ili kuepusha magonjwa na kuongeza uzalishaji na bodi hiyo hawalitetei suala la kuchanganywa pamba na mazao mengine hivyo wanaendelea kuwaelimisha wakulima.
Ofisa masoko na mauzo Kanda ya Ziwa wa Bodi ya nafaka na mazao mchanganyiko(CPB),Ally Mango,amesema wanakiwanda cha kuchakata zao la alzeti lakini changamoto iliopo ni malighafi kuwa chache hivyo wadau watumie fursa hiyo kufanya kilimo cha alzeti ili kusaidia serikali kuacha kuagiza mafuta ya kula nje ya nchi pia kwa msimu wa 2020/21 bodi hiyo itaanza uchakataji wa zao la mpunga katika kituo chao cha Mwanza.
More Stories
Mjumbe wa Baraza UWT ahimiza wananchi kuwachagua viongozi wa CCM
CCM imejipanga kushinda kwa kishindo
Wanaotumia lugha za matusi,kashfa kwenye kampeni waonywa Â