Na Mwandishi wetu
KATIBU Mkuu Wizara ya Uchukuzi, Prof. Godius Kahyarara ameiagiza Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) kuhakikisha wanatangaza mafanikio ya taasisi yanayopatikana kikanda, kimataifa pamoja na mafanikio yanayopatikana katika utekelezaji wa majukumu ya Taasisi ili watanzania waweze kufahamu.
Ameyasema hayo Jana wakati akitembelea banda la maonesho la TMA katika Mkutano wa 16 wa Wadau wa Sekta ya Uchukuzi kuhusu Ufuatiliaji na Tathmini (16th JTSR) unaofanyika jijini Arusha, yaliyoanza Disemba 5 hadi 8,2023.
Amesema TMA imekuwa ikifanya vizuri hivyo ni wakati sasa, jamii ikatambua mafanikio ya TMA kikanda na kimataifa na kuona ni namna gani inavyozidi kufanya vizuri katika kufanya kazi zake za utoaji wa utabiri wa Hali ya hewa na elimu kwa jamii juu ya matumizi yake.
“Taasisi hii inafanya kazi nzuri inayoonekana, ni vyema kujipanga kuwa na vipindi katika televisheni na kueleza mafanikio hayo”,amesema Prof. Kahyarara, wakati akitembelea mabanda ya maonesho ya wadau wa sekta ya Uchukuzi.
Amesema TMA ni taasisi inayofanya kazi nzuri na yenye mafanikio kitaifa na kimataifa hivyo Wizara ya Uchukuzi inapaswa kusimamia program ya kutangaza mafanikio ya Taasisi zilizo chini ya Wizara yake ambapo inatapaswa kuanza na TMA.
Naye, Mwakilishi wa Mkurugenzi Mkuu TMA ambaye pia ni Mkurugenzi wa Huduma za Miundombinu na Ufundi, Dkt. Pascal Waniha, ameeleza kuwa TMA imekuwa kielelezo bora katika ukanda wa Afrika Mashariki pamoja na nje ya Kanda.
“Kazi kubwa imeendelea kufanyika katika kuiwakilisha nchi vizuri kwenye masuala ya hali ya hewa kimataifa na kueleza kuwa imeteuliwa na WMO kuwa muandaaji wa mafunzo ya rada katika Kanda ya Afrika yanayoratibiwa na Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO),”Amesema Dkt. Waniha.
Amesema fursa hii imepatikana kutokana na uwekezaji mkubwa wa miundombinu ya hali ya hewa unaoendelea kufanywa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Mafanikio mengine yaliyoelezwa mbele ya Katibu Mkuu kupitia mabango ni pamoja na maendeleo katika shughuli za uangazi, ununuzi wa vifaa na mitambo ya hali ya hewa, udhibiti wa huduma za hali ya hewa pamoja na njia mbalimbali zinazotumika katika kusambaza taarifa za hali ya hewa kwa jamii na kwa sekta mahsusi.
More Stories
Bei za mafuta Novemba 2024,zaendelea Kushuka
TARURA yaomba Mkandarasi aitwe
Ilemela yakusanya bilioni 3.7.robo ya kwanza